Waamuzi 13:20-24
Waamuzi 13:20-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, wakati Manoa na mkewe walipokuwa wanatazama miali ya moto ikipanda juu mbinguni kutoka madhabahuni, walimwona malaika katika miali hiyo akipanda kwenda mbinguni. Basi Manoa na mkewe wakasujudu. Manoa akajua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu. Malaika hakumtokea tena Manoa na mkewe. Basi, Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, maana tumemwona Mungu.” Lakini mkewe akamjibu, “Kama Mwenyezi-Mungu angetaka kutuua hangepokea sadaka yetu ya kuteketezwa na ya nafaka; wala hangetuonesha mambo hayo wala kutuambia maagizo.” Kisha mkewe Manoa akajifungua mtoto wa kiume, naye Manoa akampa jina Samsoni. Mtoto huyo akakua naye Mwenyezi-Mungu akambariki.
Waamuzi 13:20-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana, ikawa, mara huo muali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa BWANA akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakaanguka kifudifudi. Lakini malaika wa BWANA hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa BWANA. Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemuona Mungu. Lakini mkewe akamwambia, Kama BWANA angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu. Basi yule mwanamke akamzaa mtoto wa kiume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, BWANA akambariki.
Waamuzi 13:20-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa BWANA akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi. Lakini malaika wa BWANA hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa BWANA. Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemwona Mungu. Lakini mkewe akamwambia, Kama BWANA angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonyesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu. Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, BWANA akambarikia.
Waamuzi 13:20-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mwali wa moto kutoka hapo madhabahuni ulipowaka kuelekea mbinguni, malaika wa BWANA akapaa ndani ya huo mwali. Manoa na mkewe, kwa kuona jambo hili, wakaanguka kifudifudi. Malaika wa BWANA hakumtokea tena Manoa na mkewe. Ndipo Manoa akatambua kuwa huyo alikuwa malaika wa BWANA. Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, kwa kuwa tumemwona Mungu.” Lakini mkewe akamwambia, “Ikiwa BWANA alikuwa amekusudia kutuua, hangepokea sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya unga kutoka mikononi mwetu, wala hangetuonesha mambo haya yote wala kututangazia mambo haya wakati huu.” Yule mwanamke akazaa mtoto wa kiume, akamwita jina Samsoni. Kijana akakua, naye BWANA akambariki.