Waamuzi 13:1-5
Waamuzi 13:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye akawaacha watawaliwe na Wafilisti kwa miaka arubaini. Kulikuwa na mtu mmoja huko Sora, wa kabila la Dani, jina lake Manoa. Mke wake alikuwa tasa. Siku moja, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea huyo mwanamke, akamwambia, “Wewe ni tasa, huna watoto. Lakini utapata mimba na kumzaa mtoto wa kiume. Kwa hiyo uwe mwangalifu, usinywe divai au kileo wala usile kitu chochote kilicho najisi, kwa maana utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Nywele za mtoto huyo kamwe zisinyolewe, maana atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake. Naye ataanza kuwakomboa Waisraeli mikononi mwa Wafilisti.”
Waamuzi 13:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya BWANA, BWANA akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arubaini. Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. Malaika wa BWANA akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto wa kiume. Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.
Waamuzi 13:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya BWANA, BWANA akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arobaini. Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. Malaika wa BWANA akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.
Waamuzi 13:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Waisraeli wakafanya maovu tena mbele za BWANA. Hivyo BWANA akawatia mikononi mwa Wafilisti kwa muda wa miaka arobaini. Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, aliyeitwa Manoa, wa ukoo wa Wadani, naye alikuwa na mke aliyekuwa tasa, asiyeweza kuzaa watoto. Malaika wa BWANA akamtokea huyo mwanamke na kumwambia, “Wewe ni tasa na huna mtoto, lakini utachukua mimba na utamzaa mtoto wa kiume. Lakini ujihadhari sana usinywe divai wala kileo kingine chochote, wala usile kitu chochote kilicho najisi, kwa kuwa utachukua mimba na utamzaa mtoto wa kiume. Wembe usipite kwenye kichwa chake, kwa kuwa huyo mwana atakuwa Mnadhiri aliyetengwa kwa Mungu tangu tumboni mwa mama yake. Naye atawaongoza na kuwaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wafilisti.”