Waamuzi 13:1-25
Waamuzi 13:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye akawaacha watawaliwe na Wafilisti kwa miaka arubaini. Kulikuwa na mtu mmoja huko Sora, wa kabila la Dani, jina lake Manoa. Mke wake alikuwa tasa. Siku moja, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea huyo mwanamke, akamwambia, “Wewe ni tasa, huna watoto. Lakini utapata mimba na kumzaa mtoto wa kiume. Kwa hiyo uwe mwangalifu, usinywe divai au kileo wala usile kitu chochote kilicho najisi, kwa maana utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Nywele za mtoto huyo kamwe zisinyolewe, maana atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake. Naye ataanza kuwakomboa Waisraeli mikononi mwa Wafilisti.” Mwanamke huyo akaenda kumwambia mume wake, “Mtu wa Mungu ambaye sura yake ilikuwa kama ya malaika wa Mungu alinijia. Sikumwuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake. Lakini aliniambia kwamba nitachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Aliniamuru nisinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi, maana mtoto huyo atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake mpaka atakapokufa.” Kisha Manoa akamwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Nakuomba ee Mwenyezi-Mungu, umtume tena yule mtu wako uliyemtuma ili atufundishe mambo tunayopaswa kumtendea huyo mtoto atakayezaliwa.” Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi la Manoa, na yule malaika wa Mungu akamwendea tena yule mwanamke alipokuwa ameketi shambani. Lakini mumewe, Manoa, hakuwa pamoja naye. Mwanamke akakimbia upesi, akamwambia mumewe, “Tazama! Yule mtu aliyenijia siku ile amenitokea tena.” Manoa akafuatana naye mpaka kwa mtu huyo, akamwuliza, “Je, wewe ni yule mtu aliyezungumza na mwanamke huyu?” Yule mtu akamjibu, “Ni mimi.” Kisha Manoa akasema, “Sasa maneno yako yatakapotimia ni mambo gani tutakayofuata kwa ajili ya huyo mtoto? Tutafanya nini kwa ajili yake?” Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Manoa, “Mkeo atapaswa kushika yote niliyomwambia: Asionje mazao yoyote ya mzabibu, wala asinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi. Yote niliyomwamuru, ayafuate.” Manoa akamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, “Tafadhali, ukae kidogo tukutayarishie mwanambuzi.” Yule malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Manoa, “Hata kama mkinilazimisha kukaa sitakula chakula chenu. Lakini kama ukipenda, tayarisha sadaka ya kuteketezwa, mtolee Mwenyezi-Mungu.” Manoa hakujua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu. Basi, Manoa akamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, “Tuambie jina lako ili tukuheshimu wakati maneno yako yatakapotimia.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa nini unataka kujua jina langu, kwa kuwa jina langu ni la ajabu?” Hapo Manoa akatayarisha mwanambuzi na tambiko, akaviweka juu ya mwamba amtolee Mwenyezi-Mungu afanyaye maajabu. Basi, wakati Manoa na mkewe walipokuwa wanatazama miali ya moto ikipanda juu mbinguni kutoka madhabahuni, walimwona malaika katika miali hiyo akipanda kwenda mbinguni. Basi Manoa na mkewe wakasujudu. Manoa akajua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu. Malaika hakumtokea tena Manoa na mkewe. Basi, Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, maana tumemwona Mungu.” Lakini mkewe akamjibu, “Kama Mwenyezi-Mungu angetaka kutuua hangepokea sadaka yetu ya kuteketezwa na ya nafaka; wala hangetuonesha mambo hayo wala kutuambia maagizo.” Kisha mkewe Manoa akajifungua mtoto wa kiume, naye Manoa akampa jina Samsoni. Mtoto huyo akakua naye Mwenyezi-Mungu akambariki. Roho ya Mwenyezi-Mungu ikaanza kumsukuma akiwa huko Mahane-dani, kati ya Sora na Eshtaoli.
Waamuzi 13:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya BWANA, BWANA akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arubaini. Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. Malaika wa BWANA akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto wa kiume. Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti. Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake, akisema, Mtu wa Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, Umetoka wapi? Wala hakuniambia jina lake; lakini aliniambia, Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto wa kiume; basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni, hadi siku ya kufa kwake. Ndipo huyo Manoa akamwomba BWANA, akisema, Ee Bwana, nakuomba, yule mtu wa Mungu uliyemtuma na aje kwetu mara ya pili, atufundishe hayo yatupasayo kumfanyia huyo mtoto atakayezaliwa. Mungu akasikia sauti ya Manoa; naye malaika wa Mungu akamwendea yule mwanamke tena alipokuwa anaketi shambani; lakini mumewe, Manoa, hakuwapo pamoja naye. Basi huyo mwanamke akaenda haraka, akapiga mbio, na kumwambia mumewe, akisema, Tazama, huyo mtu amenitokea, huyo aliyenijia siku ile. Basi Manoa akainuka, akamfuata mkewe, na kumfikia mtu huyo, akamwuliza, Je! Wewe ndiwe mtu yule aliyenena na huyu mwanamke? Akasema, Ndio, ni mimi. Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia, je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani, na kazi yake itakuwa ni nini? Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, “Hebu huyo mwanamke ajihadhari na yote niliyomwambia.” Asile kitu chochote kitokacho katika mzabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu chochote kilicho najisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze. Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako. Lakini malaika wa BWANA akamwambia Manoa, “Ijapokuwa unanizuia, sitakula chakula chako; lakini kama unataka kuandaa sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsogezea BWANA”. Kwa kuwa Manoa hakujua ya kwamba yeye ni malaika wa BWANA. Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza? Huyo malaika wa BWANA akamwambia, Kwa nini unaniuliza jina langu, na jina hilo ni la ajabu? Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, akamtolea BWANA hapo juu ya mwamba; huyo malaika akatenda la ajabu; Manoa na mkewe wakaangalia. Kwa maana, ikawa, mara huo muali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa BWANA akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakaanguka kifudifudi. Lakini malaika wa BWANA hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa BWANA. Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemuona Mungu. Lakini mkewe akamwambia, Kama BWANA angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu. Basi yule mwanamke akamzaa mtoto wa kiume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, BWANA akambariki. Roho ya BWANA ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.
Waamuzi 13:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya BWANA, BWANA akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arobaini. Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. Malaika wa BWANA akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti. Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake, akisema, Mtu wa Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, Umetoka wapi? Wala hakuniambia jina lake; lakini aliniambia, Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni, hata siku ya kufa kwake. Ndipo huyo Manoa akamwomba BWANA, akisema, Ee Bwana, nakuomba, yule mtu wa Mungu uliyemtuma na aje kwetu mara ya pili, atufundishe hayo yatupasayo kumfanyia huyo mtoto atakayezaliwa. Mungu akasikiza sauti ya Manoa; naye malaika wa Mungu akamwendea yule mwanamke tena alipokuwa anaketi shambani; lakini mumewe, Manoa, hakuwapo pamoja naye. Basi huyo mwanamke akaenda haraka, akapiga mbio, na kumwambia mumewe, akisema, Tazama, huyo mtu amenitokea, huyo aliyenijilia siku ile. Basi Manoa akainuka, akamwandama mkewe, na kumfikilia mtu huyo, akamwuliza, Je! Wewe ndiwe mtu yule aliyenena na huyu mwanamke? Akasema, Naam, ni mimi. Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia, je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani, na kazi yake itakuwa ni nini? Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, Katika hayo yote niliyomwambia huyo mwanamke na ajihadhari. Asile kitu cho chote kitokacho katika mzabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu cho chote kilicho najisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze. Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako. Lakini malaika wa BWANA akamwambia Manoa, Ujapokuwa wanizuia, sitakula katika mkate wako; na kwamba wataka kufanya tayari sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsongezea BWANA. Kwa kuwa Manoa hakujua ya kwamba yeye ni malaika wa BWANA. Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza? Huyo malaika wa BWANA akamwambia, Kwani wewe kuniuliza jina langu, kwa kuwa jina hilo ni la ajabu? Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, akamtolea BWANA hapo juu ya mwamba; huyo malaika akatenda la ajabu; Manoa na mkewe wakaangalia. Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa BWANA akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi. Lakini malaika wa BWANA hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa BWANA. Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemwona Mungu. Lakini mkewe akamwambia, Kama BWANA angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonyesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu. Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, BWANA akambarikia. Roho ya BWANA ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.
Waamuzi 13:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Waisraeli wakafanya maovu tena mbele za BWANA. Hivyo BWANA akawatia mikononi mwa Wafilisti kwa muda wa miaka arobaini. Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, aliyeitwa Manoa, wa ukoo wa Wadani, naye alikuwa na mke aliyekuwa tasa, asiyeweza kuzaa watoto. Malaika wa BWANA akamtokea huyo mwanamke na kumwambia, “Wewe ni tasa na huna mtoto, lakini utachukua mimba na utamzaa mtoto wa kiume. Lakini ujihadhari sana usinywe divai wala kileo kingine chochote, wala usile kitu chochote kilicho najisi, kwa kuwa utachukua mimba na utamzaa mtoto wa kiume. Wembe usipite kwenye kichwa chake, kwa kuwa huyo mwana atakuwa Mnadhiri aliyetengwa kwa Mungu tangu tumboni mwa mama yake. Naye atawaongoza na kuwaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wafilisti.” Ndipo huyo mwanamke akamwendea mumewe na kumwambia, “Mtu wa Mungu alinijia. Alionekana kama malaika wa Mungu, wa kutisha sana. Sikumuuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake. Lakini aliniambia, ‘Utachukua mimba na utazaa mtoto wa kiume. Basi sasa, usinywe divai wala kileo kingine chochote, wala usile kitu kilicho najisi, kwa kuwa huyo mtoto atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yake hadi kufa kwake.’ ” Ndipo Manoa akamwomba BWANA, akasema: “Ee Bwana, nakusihi huyo mtu wa Mungu uliyemtuma kwetu aje tena, ili atufundishe jinsi ya kumlea huyo mwana atakayezaliwa.” Mungu akamsikia Manoa, naye malaika wa Mungu akamjia tena huyo mwanamke alipokuwa shambani; lakini mumewe Manoa hakuwa naye. Basi yule mwanamke akaenda haraka na kumwambia mumewe, “Tazama mtu yule aliyenitokea siku ile yupo hapa!” Manoa akainuka akaandamana na mkewe. Alipomfikia yule mtu akamuuliza, “Je, wewe ndiwe ulisema na mke wangu?” Akasema, “Ni mimi.” Basi Manoa akamuuliza, “Maneno yako yatakapotimia, je, masharti ya maisha ya mtoto huyu yatakuwa ni yapi, na kazi yake itakuwa ni ipi?” Malaika wa BWANA akamjibu, “Mke wako hana budi kufanya yale yote niliyomwambia. Kamwe asile kitu chochote kitakachotoka katika mzabibu, wala asinywe divai yoyote wala kileo chochote, wala asile kitu chochote kilicho najisi. Hana budi kufanya kila kitu nilichomwagiza.” Manoa akamjibu yule malaika wa BWANA, “Twakuomba usubiri kwanza ili tuweze kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.” Malaika wa BWANA akamjibu, “Hata kama utanizuia, sitakula chochote kwako. Lakini ukitaka kuandaa sadaka ya kuteketezwa, mtolee BWANA.” (Manoa hakumtambua kuwa huyu alikuwa malaika wa BWANA.) Kisha Manoa akamuuliza yule malaika wa BWANA, “Jina lako ni nani, ili tuweze kukupa heshima wakati maneno uliyonena yatakapotimia?” Malaika wa BWANA akamjibu, “Kwa nini unauliza jina langu? Ni jina la ajabu.” Ndipo Manoa akamchukua mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, naye akamtolea BWANA dhabihu hapo juu ya mwamba. Naye yule malaika wa BWANA akafanya jambo la ajabu wakati Manoa na mkewe wakiwa wanaangalia: Mwali wa moto kutoka hapo madhabahuni ulipowaka kuelekea mbinguni, malaika wa BWANA akapaa ndani ya huo mwali. Manoa na mkewe, kwa kuona jambo hili, wakaanguka kifudifudi. Malaika wa BWANA hakumtokea tena Manoa na mkewe. Ndipo Manoa akatambua kuwa huyo alikuwa malaika wa BWANA. Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, kwa kuwa tumemwona Mungu.” Lakini mkewe akamwambia, “Ikiwa BWANA alikuwa amekusudia kutuua, hangepokea sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya unga kutoka mikononi mwetu, wala hangetuonesha mambo haya yote wala kututangazia mambo haya wakati huu.” Yule mwanamke akazaa mtoto wa kiume, akamwita jina Samsoni. Kijana akakua, naye BWANA akambariki. Roho wa BWANA akaanza kumpa msukumo alipokuwa huko Mahane-Dani, kati ya Sora na Eshtaoli.