Yakobo 5:11-15
Yakobo 5:11-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Tunawaita hao wenye heri kwa sababu walivumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wa Yobu, na mnajua jinsi Bwana alivyomtendea mwishoni. Maana Bwana amejaa huruma na rehema. Zaidi ya hayo yote, ndugu zangu, msiape kwa mbingu, wala kwa dunia, wala kwa kitu kingine chochote. Semeni “Ndiyo” kama maana yenu ni ndiyo, na “La” kama maana yenu ni la, na hapo hamtahukumiwa na Mungu. Je, pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. Je, yuko mgonjwa kati yenu? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa, nao watamwombea na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Wakiomba kwa imani mgonjwa ataponyeshwa; Bwana atampatia nafuu, na dhambi alizotenda zitaondolewa.
Yakobo 5:11-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Angalieni, twawaita heri wao waliostahimili. Mmesikia habari za kustahimili kwake Ayubu, kuona mwisho Bwana aliyomtendea, jinsi Bwana alivyo mwingi wa rehema na mwenye huruma. Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali “ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, msije mkaanguka katika hukumu. Kuna mtu miongoni mwenu anayeteseka? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa mgonjwa? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.
Yakobo 5:11-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma. Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu. Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.
Yakobo 5:11-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kama mnavyojua, tunawahesabu wale waliovumilia kuwa wabarikiwa. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu, na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma, na amejaa rehema. Zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, iwe kwa mbingu au kwa dunia, au kwa kitu kingine chochote. “Ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, la sivyo mtahukumiwa. Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu. Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua, na kama ametenda dhambi, atasamehewa.