Yakobo 5:1-9
Yakobo 5:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Na sasa sikilizeni enyi matajiri! Lieni na kuomboleza kwa sababu ya taabu zitakazowajieni. Mali zenu zimeoza, na nguo zenu zimeliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha vimeota kutu, na kutu hiyo itakuwa ushahidi dhidi yenu, nayo itakula miili yenu kama vile moto. Nyinyi mmejirundikia mali katika siku hizi za mwisho! Hamkuwalipa mishahara watumishi waliofanya kazi katika mashamba yenu. Sikilizeni malalamiko yao! Kilio cha hao wanaovuna mashamba yenu kimefika masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmeishi duniani maisha ya kujifurahisha na ya anasa. Mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. Mmemhukumu na kumuua mtu asiye na hatia, naye hakuwapingeni! Basi, ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima anavyongoja kwa subira mimea yake itoe mavuno ya thamani. Yeye hungojea kwa subira mvua za masika na za vuli. Nanyi pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake Bwana inakaribia. Ndugu zangu, msinung'unikiane nyinyi kwa nyinyi msije mkahukumiwa na Mungu. Hakimu yu karibu, tayari kuingia.
Yakobo 5:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige mayowe kwa sababu ya mateso yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliokosa kuwalipa kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejinenepesha mioyo yenu kama kwa siku ya kuchinjwa. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi. Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango.
Yakobo 5:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi. Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu, msinung’unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango.
Yakobo 5:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. Utajiri wenu umeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu, nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho. Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu, na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe; mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. Mmewahukumu na kuwaua watu wenye haki, waliokuwa hawapingani nanyi. Kwa hiyo, ndugu zangu, vumilieni hadi kuja kwake Bwana. Tazameni jinsi mkulima angojavyo ardhi itoe mavuno yake yaliyo ya thamani, na jinsi anavyovumilia kwa ajili ya kupata mvua ya kwanza na ya mwisho. Ninyi nanyi vumilieni, tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana kumekaribia. Ndugu zangu, msinungʼunikiane, msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni!