Yakobo 3:6-12
Yakobo 3:6-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Hali kadhalika ulimi ni kama moto. Umejaa maovu chungu nzima, unayo nafasi yake katika miili yetu na hueneza ubaya katika nafsi zetu zote. Huteketeza maisha yetu yote kwa moto utokao Jehanamu kwenyewe. Binadamu anaweza kuwafuga wanyama, na amefaulu kufuga viumbe vyote – wanyama wa mwituni, ndege, nyoka na viumbe vya baharini. Lakini hakuna mtu aliyefaulu kuufuga ulimi. Ulimi ni kitu kiovu, hakitawaliki, na kimejaa sumu inayoua. Kwa ulimi sisi twamshukuru Bwana na Baba yetu. Kwa ulimi huhuo twawalaani watu, watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu. Maneno ya kubariki na ya kulaani hutoka katika kinywa kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapaswi kuwa hivyo. Je, chemchemi moja yaweza kutoa maji matamu na maji machungu pamoja? Ndugu zangu, je, mtini waweza kuzaa zeituni? Au, mzabibu waweza kuzaa tini? Chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.
Yakobo 3:6-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfululizo wa maumbile, nao huwashwa moto na Jehanamu. Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu. Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo tunamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo unwawalaani wanadamu walioumbwa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo. Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu? Ndugu zangu, Je! Mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu.
Yakobo 3:6-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum. Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu. Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo. Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu? Ndugu zangu, Je! Mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu.
Yakobo 3:6-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ulimi pia ni moto, ndio ulimwengu wa uovu kati ya viungo vya mwili. Ulimi huutia mwili wote wa mtu unajisi na kuuwasha moto mfumo mzima wa maisha yake, nao wenyewe huchomwa moto wa Jehanamu. Kwa maana kila aina ya wanyama, ndege, wanyama watambaao na viumbe vya baharini hufugika na hufugwa na binadamu, lakini hakuna mtu awezaye kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa ulimi tunamhimidi Bwana na Baba yetu, na kwa huo twawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haistahili kuwa hivyo. Je, chemchemi moja inaweza kutoa katika tundu moja maji matamu na maji ya chumvi? Je, ndugu zangu, mtini unaweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Wala chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.