Yakobo 2:14-26
Yakobo 2:14-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa? Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula. Yafaa kitu gani nyinyi kuwaambia hao: “Nendeni salama mkaote moto na kushiba,” bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha? Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa. Lakini mtu anaweza kusema: “Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!” Haya! Nioneshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonesha imani yangu kwa matendo yangu. Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu. Mpumbavu wee! Je, wataka kuoneshwa kwamba imani bila matendo imekufa? Je, Abrahamu babu yetu alipataje kukubaliwa kuwa mwadilifu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa tambiko mwanawe Isaka juu ya madhabahu. Waona, basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake. Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: “Abrahamu alimwamini Mungu, na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki ya Mungu.” Mnaona, basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake, na si kwa imani peke yake. Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine. Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa.
Yakobo 2:14-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mmoja wenu akawaambia, Nendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya kimwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai? Je! Baba yetu Abrahamu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu? Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale. Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Abrahamu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu. Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake. Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine? Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.
Yakobo 2:14-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai? Je! Baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu? Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale. Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu. Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake. Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine? Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.
Yakobo 2:14-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, naye mmoja wenu akamwambia, “Nenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? Vivyo hivyo, imani peke yake, kama haikuambatana na matendo, imekufa. Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.” Nioneshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonesha imani yangu kwa matendo. Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani wanaamini hivyo na kutetemeka. Ewe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu? Je, Abrahamu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaka madhabahuni? Unaona jinsi imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda. Kwa njia hiyo likatimizwa andiko lisemalo, “Abrahamu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu. Mnaona kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake. Vivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba: je, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine? Kama vile mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.