Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yakobo 1:16-27

Yakobo 1:16-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike! Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe katika nafasi ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake. Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini si mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika. Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea lile neno lililopandwa mioyoni mwenu, ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu. Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo. Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya. Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe. Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.

Shirikisha
Soma Yakobo 1

Yakobo 1:16-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike. Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. Kwa mapenzi yake mwenyewe alituzaa kwa neno la kweli, kusudi tuwe kama mazao ya kwanza katika viumbe vyake vyote. Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika. Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu. Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu. Basi kuweni watendaji wa Neno, wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu. Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na husahau upesi jinsi alivyo. Lakini yeye anayeangalia kwa makini katika sheria kamilifu iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau, bali akatenda alichosikia, basi atabarikiwa katika kile anachofanya. Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake haifai kitu. Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu Baba yetu, ndiyo hii: ni kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.

Shirikisha
Soma Yakobo 1

Yakobo 1:16-27

Yakobo 1:16-27 BHNYakobo 1:16-27 BHNYakobo 1:16-27 BHNYakobo 1:16-27 BHNYakobo 1:16-27 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima