Isaya 9:6-7
Isaya 9:6-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto wa kiume. Naye atapewa mamlaka ya kutawala. Ataitwa: “Mshauri wa Ajabu”. “Mungu Mwenye Nguvu”, “Baba wa Milele”, “Mfalme wa Amani”. Utawala wake utastawi daima, amani ya ufalme wake haitakoma. Atachukua wadhifa wa mfalme Daudi na kutawala juu ya ufalme wake; ataustawisha na kuuimarisha, kwa haki na uadilifu, tangu sasa na hata milele. Hayo atayafanya Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
Isaya 9:6-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto wa kiume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani. Mamlaka ya enzi yake yatakuzwa daima, Na kutakuwa na amani isiyo na mwisho, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.
Isaya 9:6-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.
Isaya 9:6-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto wa kiume, nao utawala utakuwa begani mwake. Naye ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani. Kuongezeka kwa utawala wake na amani hakutakuwa na mwisho. Atatawala kwenye kiti cha utawala cha Daudi na juu ya ufalme wake, akiuthibitisha na kuutegemeza kwa haki na kwa adili, tangu wakati huo na hata milele. Wivu wa BWANA wa majeshi utatimiza haya.