Isaya 9:1-6
Isaya 9:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini nchi ile iliyokuwa imekumbwa na huzuni haitabaki daima katika giza hilo kuu. Hapo awali Mungu alizifedhehesha nchi za Zebuluni na Naftali, lakini siku za usoni ataifanikisha sehemu hii ya baharini na nchi iliyo ngambo ya Yordani na hata Galilaya wanamoishi watu wa mataifa. Watu waliotembea gizani wameona mwanga mkubwa. Watu walioishi katika nchi ya giza kuu, sasa mwanga umewaangazia. Wewe, ee Mungu, umelikuza taifa, umeiongeza furaha yake. Watu wanafurahi mbele yako, wana furaha kama wakati wa mavuno, kama wafurahivyo wanaogawana nyara. Maana nira nzito walizobeba, nira walizokuwa wamefungwa, na fimbo ya wanyapara wao, umezivunjavunja kama wakati wa Wamidiani. Viatu vyote vya washambulizi vitani na mavazi yote yenye madoa ya damu yatateketezwa kama kuni za kuwasha moto. Maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto wa kiume. Naye atapewa mamlaka ya kutawala. Ataitwa: “Mshauri wa Ajabu”. “Mungu Mwenye Nguvu”, “Baba wa Milele”, “Mfalme wa Amani”.
Isaya 9:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo awali aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa. Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza. Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno, Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani. Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyovingirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni. Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto wa kiume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.
Isaya 9:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo kwanza aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa. Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza. Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno, Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani. Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyofingirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni. Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.
Isaya 9:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hata hivyo, hakutakuwa huzuni tena kwa wale waliokuwa katika dhiki. Hapo awali aliidhili nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, lakini katika siku zijazo ataipa heshima Galilaya ya Mataifa, karibu na njia ya bahari, ngʼambo ya Yordani: Watu wanaotembea katika giza wameona nuru kuu, wale wanaoishi katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewazukia. Umelikuza taifa, na kuzidisha furaha yao, wanafurahia mbele zako, kama watu wanavyofurahia wakati wa mavuno, kama mashujaa wanavyofurahia wakigawanya nyara. Kama vile siku ya kushindwa kwa Wamidiani, umevunja nira iliyowalemea, ile gongo mabegani mwao na fimbo ya aliyewadhulumu. Kila kiatu cha shujaa kilichotumiwa vitani, na kila vazi lililovingirishwa katika damu vitawekwa kwa ajili ya kuchomwa, vitakuwa kuni za kuwasha moto. Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto wa kiume, nao utawala utakuwa begani mwake. Naye ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.