Isaya 62:1-5
Isaya 62:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa ajili ya Siyoni sitakaa kimya, kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, mpaka kuokolewa kwake kuchomoze kama umeme, wokovu wake utokeze kama mwenge. Mataifa watauona wokovu wako, wafalme wote watauona utukufu wako. Nawe utaitwa kwa jina jipya, jina atakalokupa Mwenyezi-Mungu mwenyewe. Utakuwa taji zuri mkononi mwa Mwenyezi-Mungu; kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako. Hutaitwa tena: “Aliyeachwa”, wala nchi yako haitaitwa: “Ukiwa”. Bali utaitwa: “Namfurahia,” na nchi yako itaitwa: “Aliyeolewa.” Maana Mwenyezi-Mungu amependezwa nawe, naye atakuwa kama mume wa nchi yako. Maana kama kijana mwanamume amwoavyo msichana, ndivyo aliyekujenga atakavyokuwa mume wako. Kama bwana arusi afurahivyo juu ya bibi arusi, ndivyo Mungu atakavyofurahi juu yako.
Isaya 62:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha BWANA. Nawe utakuwa taji la uzuri katika mkono wa BWANA, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako. Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefziba; na nchi yako Beula; kwa kuwa BWANA anakufurahia, na nchi yako itaolewa. Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.
Isaya 62:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha BWANA. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa BWANA, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako. Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa BWANA anakufurahia, na nchi yako itaolewa. Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.
Isaya 62:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hadi haki yake itakapoangaza kama mapambazuko, wokovu wake kama mwanga wa moto. Mataifa wataona haki yako, nao wafalme wote wataona utukufu wako; wewe utaitwa kwa jina jipya lile ambalo kinywa cha BWANA kitatamka. Utakuwa taji la fahari mkononi mwa BWANA, taji la kifalme mkononi mwa Mungu wako. Hawatakuita tena Aliyeachwa, wala nchi yako kuiita Ukiwa. Bali utaitwa Hefsiba, nayo nchi yako itaitwa Beula, kwa maana BWANA atakufurahia, nayo nchi yako itaolewa. Kama vile kijana aoavyo mwanamwali, ndivyo Mwashi wako atakavyokuoa; kama bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi wake, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.