Isaya 6:1-13
Isaya 6:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo mwaka aliofariki mfalme Uzia, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi kilicho juu na cha fahari. Pindo la vazi lake lilienea hekaluni mote, na juu yake walikuwa wamekaa malaika. Kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Mawili ya kufunika uso, mawili ya kufunika mwili na mawili ya kurukia. Waliitana kila mmoja na mwenzake hivi: “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu, ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi! Dunia yote imejaa utukufu wake.” Sauti yao iliitikisa misingi ya milango ya hekalu, nalo likajaa moshi. Basi, mimi nikasema, “Ole wangu! Mimi nimeangamia, maana, midomo yangu ni najisi, na watu ninaoishi nao ni najisi kama mimi. Hata hivyo, kwa macho yangu mwenyewe, nimemwona Mfalme, Mwenyezi-Mungu wa majeshi.” Basi, mmoja wa hao malaika akaruka kunijia, akiwa ameshika mkononi koleo lililokuwa na kaa la moto alilolitwaa madhabahuni. Naye akinigusa nalo mdomoni, akasema: “Tazama, kaa hili limekugusa mdomo; umeondolewa hatia yako, umesamehewa dhambi yako.” Kisha nikamsikia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekuwa mjumbe wetu?” Nami nikajibu, “Niko hapa! Nitume mimi.” Naye akaniambia, “Nenda ukawaambie watu hawa: ‘Mtasikiliza sana, lakini hamtaelewa; mtatazama sana, lakini hamtaona.’” Kisha akaniambia, “Zipumbaze akili za watu hawa, masikio yao yasisikie, macho yao yasione; ili wasije wakaona kwa macho yao, wakasikia kwa masikio yao, wakaelewa kwa akili zao, na kunigeukia, nao wakaponywa.” Mimi nikauliza, “Bwana, mpaka lini?” Naye akanijibu, “Mpaka hapo miji itakapobaki tupu bila wakazi, nyumba bila watu, na nchi itakapoharibiwa kabisa. Nami Mwenyezi-Mungu nitawapeleka watu mbali, na kuifanya nchi yote kuwa mahame. Hata wakibaki watu asilimia kumi, nao pia watateketezwa. Hao watakuwa kama mvinje au mwaloni ambao kisiki chake kimebaki baada ya kukatwa.” (Kisiki hicho ni mbegu takatifu ya chanzo kipya.)
Isaya 6:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi. Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa. Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi. Naye akaniambia, Nenda, ukawaambie watu hawa, Endeleeni kusikia, lakini msifahamu; endeleeni kutazama, lakini msione. Zifanye akili za watu hawa zipumbae, na uyatie uzito masikio yao, na uyafumbe macho yao; wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa mioyo yao, na kurejea na kuponywa. Ndipo nilipouliza, Ee Bwana, hata lini? Naye akanijibu, Hadi miji itakapokuwa ukiwa, haina wenyeji, na nyumba zitakapokuwa hazina watu, na nchi hii itakapokuwa ganjo kabisa; hadi BWANA atakapowahamisha watu waende mbali sana, na mahame yatakapokuwa mengi ndani ya nchi. Na ijapokuwa imebaki sehemu moja katika sehemu kumi ndani yake, italiwa hii nayo; kama mvinje na kama mwaloni, ambao shina lake limebaki, ingawa imekatwa; kadhalika mbegu takatifu ndiyo shina lake.
Isaya 6:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi. Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa. Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi. Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione. Uunoneshe moyo wa watu hawa, ukayatie uzito masikio yao, ukayafumbe macho yao; wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa mioyo yao, na kurejea na kuponywa. Ndipo nilipouliza, Ee Bwana, hata lini? Naye akanijibu, Hata miji itakapokuwa ukiwa, haina wenyeji, na nyumba zitakapokuwa hazina watu, na nchi hii itakapokuwa ganjo kabisa; hata BWANA atakapowahamisha watu waende mbali sana, na mahame yatakapokuwa mengi ndani ya nchi. Na ijapokuwa imebaki sehemu moja katika sehemu kumi ndani yake, italiwa hii nayo; kama mvinje na kama mwaloni, ambao shina lake limebaki, ingawa imekatwa; kadhalika mbegu takatifu ndiyo shina lake.
Isaya 6:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwaka ule Mfalme Uzia alikufa, nilimwona Bwana ameketi kwenye kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu. Juu yake walikuwa maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao, na kwa mawili walikuwa wakiruka. Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.” Kwa sauti zao, miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi. Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi kati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi.” Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni. Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa, nayo dhambi yako imesamehewa.” Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayeenda kwa ajili yetu?” Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!” Akasema, “Nenda ukawaambie watu hawa: “ ‘Mtaendelea daima kusikiliza, lakini kamwe hamtaelewa; mtaendelea daima kutazama, lakini kamwe hamtatambua.’ Fanya mioyo ya watu hawa kuwa migumu, fanya masikio yao yasisikie, na upofushe macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, nao wakageuka, wakaponywa.” Ndipo nikasema, “Hadi lini, Ee Bwana?” Naye akanijibu: “Hadi miji iwe imeachwa magofu na bila wakazi, hadi nyumba zitakapobaki bila watu, na mashamba yatakapoharibiwa na kuangamizwa, hadi BWANA atakapokuwa amekwisha kumpeleka kila mmoja mbali sana, na nchi itakapokuwa imeachwa kabisa. Hata kama sehemu ya kumi ya watu watabaki katika nchi, itaharibiwa tena. Lakini kama vile mvinje au mwaloni ubakizavyo visiki unapokatwa, ndivyo mbegu takatifu itakavyokuwa kisiki katika nchi.”