Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 58:1-12

Isaya 58:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu asema: “Piga kelele, wala usijizuie; paza sauti yako kama tarumbeta. Watangazie watu wangu makosa yao, waambie wazawa wa Yakobo dhambi zao. Siku hata siku wananijia kuniabudu, wanatamani kujua mwongozo wangu, kana kwamba wao ni taifa litendalo haki, taifa lisilosahau sheria za Mungu wao. Wananitaka niamue kwa haki, na kutamani kukaa karibu na Mungu. “Nyinyi mnaniuliza: ‘Mbona tunafunga lakini wewe huoni? Mbona tunajinyenyekesha, lakini wewe hujali?’ “Ukweli ni kwamba wakati mnapofunga, mnatafuta tu furaha yenu wenyewe, na kuwakandamiza wafanyakazi wenu! Mnafunga, na kugombana na kupigana ngumi. Mkifunga namna hiyo maombi yenu hayatafika kwangu juu. Mfungapo, nyinyi mnajitaabisha; mnaviinamisha vichwa vyenu kama unyasi, na kulalia nguo za magunia na majivu. Je, huo ndio mnaouita mfungo? Je, hiyo ni siku inayokubaliwa nami? “La! Mfungo ninaotaka mimi ni huu: Kuwafungulia waliofungwa bila haki, kuziondoa kamba za utumwa, kuwaachia huru wanaokandamizwa, na kuvunjilia mbali udhalimu wote! Mfungo wa kweli ni kuwagawia wenye njaa chakula chako, kuwakaribisha nyumbani kwako maskini wasio na makao, kuwavalisha wasio na nguo, bila kusahau kuwasaidia jamaa zenu. “Mkifanya hivyo mtangara kama pambazuko, mkiwa wagonjwa mtapona haraka. Matendo yenu mema yatawatangulia, nami nitawalindeni kutoka nyuma kwa utukufu wangu. Ndipo mtakapoomba, nami Mwenyezi-Mungu nitawaitikia; mtalia kwa sauti kuomba msaada, nami nitajibu, ‘Niko hapa!’ “Kama mkiiondoa dhuluma kati yenu, mkiacha kudharau wengine na kusema maovu, mkiwapa chakula kwa ukarimu wenye njaa, mkitosheleza mahitaji ya wenye dhiki, mwanga utawaangazia nyakati za giza, giza lenu litakuwa kama mchana. Mimi Mwenyezi-Mungu nitawaongozeni daima, nitatosheleza mahitaji yenu wakati wa shida. Nitawaimarisha mwilini, nanyi mtakuwa kama bustani iliyomwagiliwa maji, kama chemchemi ya maji ambayo maji yake hayakauki kamwe. Magofu yenu ya kale yatajengwa; mtajenga upya juu ya misingi iliyoachwa zamani. Nanyi mtaitwa watu waliotengeneza upya kuta, watu waliozifanya barabara za mji zipitike tena.

Shirikisha
Soma Isaya 58

Isaya 58:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubirie watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mnafunga ili mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Kufunga kama huku kwa siku ya leo hakutafanya sauti zenu zisikike juu. Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na BWANA? Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usikose kumsaidia mtu aliye jamaa yako. Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na uponyaji wako utatokea punde; na haki yako itakutangulia; utukufu wa BWANA utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na BWANA ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimpa mtu mwenye njaa chakula chako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye BWANA atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui. Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejesha njia za kukaa.

Shirikisha
Soma Isaya 58

Isaya 58:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na BWANA? Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa BWANA utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na BWANA ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye BWANA atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui. Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia.

Shirikisha
Soma Isaya 58

Isaya 58:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Piga kelele, usizuie. Paza sauti yako kama tarumbeta. Watangazieni watu wangu uasi wao, na kwa nyumba ya Yakobo dhambi zao. Kwa maana kila siku hunitafuta, wanaonekana kutaka kujua njia zangu, kana kwamba walikuwa taifa linalotenda lililo sawa, na ambalo halijaziacha amri za Mungu wake. Hutaka kwangu maamuzi ya haki, nao hutamani Mungu awakaribie. Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona? Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’ “Lakini katika siku ya kufunga kwenu, mnafanya mnavyotaka na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote. Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano, na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu. Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu. Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua, siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza? Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete, na kwa kujilaza juu ya nguo ya gunia na majivu? Je, huo ndio mnaouita mfungo, siku iliyokubalika kwa BWANA? “Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua: kufungua minyororo ya udhalimu, na kufungua kamba za nira, kuwaweka huru walioonewa, na kuvunja kila nira? Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi, unapomwona aliye uchi, umvike, wala si kumkimbia mtu wa nyama na damu yako mwenyewe? Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko na uponyaji wako utatokea upesi; ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako, na utukufu wa BWANA utakuwa mlinzi nyuma yako. Ndipo utaita, naye BWANA atajibu, utalia kuomba msaada, naye atasema: Mimi hapa. “Kama ukiiondoa nira ya udhalimu, na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu, nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu na kutosheleza mahitaji ya walioonewa, ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani, nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri. BWANA atakuongoza siku zote, atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame, naye ataitia nguvu mifupa yako. Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri, kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe. Watu wako watajenga tena magofu ya zamani na kuinua misingi ya kale; utaitwa Mwenye Kukarabati Kuta Zilizobomoka, Mwenye Kurejeza Barabara za Makao.

Shirikisha
Soma Isaya 58

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha