Isaya 51:4-8
Isaya 51:4-8 Biblia Habari Njema (BHN)
“Nisikilizeni enyi watu wangu, nitegeeni sikio enyi taifa langu. Sheria na haki zitatoka kwangu mimi; nazo zitakuwa mwanga wa mataifa. Nitaleta ukombozi hima; wokovu nitakaoleta waanza kutokea. Mimi mwenyewe nitayatawala mataifa. Wakazi wa nchi za mbali wananingojea, wanaitegemea nguvu yangu. Inueni macho mzitazame mbingu, kisha tazameni dunia huko chini. Mbingu zitatoweka kama moshi, dunia itachakaa kama vazi, na wakazi wake watakufa kama wadudu. Lakini wokovu niuletao wadumu milele; ukombozi wangu kamwe hautakoma. “Nisikilizeni enyi mjuao mambo ya haki, ambao sheria zangu zimo mioyoni mwenu. Msiogope dharau za watu, wala kufadhaishwa na masimango yao. Maana wataliwa na nondo kama vile vazi; viwavi watawala kama walavyo nguo ya sufu. Lakini ukombozi niletao mimi utadumu milele; wokovu wangu hautakuwa na mwisho.”
Isaya 51:4-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nisikilizeni mimi, enyi watu wangu; nisikieni, taifa langu; maana sheria itatoka kwangu, na kutoa haki yangu iwe nuru ya mataifa. Haki yangu i karibu, wokovu wangu umekuwa wazi, na mikono yangu itawahukumu makabila ya watu; visiwa vitaningoja, navyo vitautumainia mkono wangu. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na ukombozi wangu hautakoma kamwe. Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope masuto ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao. Maana nondo atawala kama vazi, na funza atawala kama sufu; bali haki yangu itakuwa ya milele, na wokovu wangu hata vizazi vyote.
Isaya 51:4-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nisikilizeni mimi, enyi watu wangu; nisikieni, taifa langu; maana sheria itatoka kwangu, nami nitaistarehesha hukumu yangu iwe nuru ya mataifa. Haki yangu i karibu, wokovu wangu umekuwa wazi, na mikono yangu itawahukumu kabila za watu; visiwa vitaningoja, navyo vitautumainia mkono wangu. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka. Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao. Maana nondo itawala kama vazi, na funza atawala kama sufu; bali haki yangu itakuwa ya milele, na wokovu wangu hata vizazi vyote.
Isaya 51:4-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Nisikilizeni, watu wangu; nisikieni, taifa langu: Sheria itatoka kwangu; haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa. Haki yangu inakaribia mbio, wokovu wangu unakuja, nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa. Visiwa vitanitegemea na kungojea mkono wangu kwa matumaini. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame dunia chini; mbingu zitatoweka kama moshi, dunia itachakaa kama vazi, na wakazi wake kufa kama inzi. Bali wokovu wangu utadumu milele, haki yangu haitakoma kamwe. “Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa, ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu: Msiogope mashutumu ya wanadamu wala msitiwe hofu na matukano yao. Kwa maana nondo atawala kama vazi, nao funza atawatafuna kama sufu. Lakini haki yangu itadumu milele, wokovu wangu kwa vizazi vyote.”