Isaya 51:1-8 - Compare All Versions
Isaya 51:1-8 BHN (Biblia Habari Njema)
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nisikilizeni enyi mnaotaka kukombolewa, nyinyi mnaonitafuta mimi Mwenyezi-Mungu. Utazameni mwamba mlimochongwa, chimbo la mawe mlimochimbuliwa. Mkumbukeni Abrahamu babu yenu, na Sara aliyewazaa nyinyi. Abrahamu alikuwa hana mtoto wakati nilipomwita, lakini nilimbariki na kumfanya kuwa na wengi. “Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji mji wa Siyoni, nitaparekebisha mahali pake pote palipoharibika. Nyika zake nitazifanya kama bustani ya Edeni, majangwa yake kama bustani ya Mwenyezi-Mungu. Kwake kutapatikana furaha na shangwe, na nyimbo za shukrani zitasikika humo. “Nisikilizeni enyi watu wangu, nitegeeni sikio enyi taifa langu. Sheria na haki zitatoka kwangu mimi; nazo zitakuwa mwanga wa mataifa. Nitaleta ukombozi hima; wokovu nitakaoleta waanza kutokea. Mimi mwenyewe nitayatawala mataifa. Wakazi wa nchi za mbali wananingojea, wanaitegemea nguvu yangu. Inueni macho mzitazame mbingu, kisha tazameni dunia huko chini. Mbingu zitatoweka kama moshi, dunia itachakaa kama vazi, na wakazi wake watakufa kama wadudu. Lakini wokovu niuletao wadumu milele; ukombozi wangu kamwe hautakoma. “Nisikilizeni enyi mjuao mambo ya haki, ambao sheria zangu zimo mioyoni mwenu. Msiogope dharau za watu, wala kufadhaishwa na masimango yao. Maana wataliwa na nondo kama vile vazi; viwavi watawala kama walavyo nguo ya sufu. Lakini ukombozi niletao mimi utadumu milele; wokovu wangu hautakuwa na mwisho.”
Isaya 51:1-8 SRUV (Swahili Revised Union Version)
Nisikilizeni, ninyi mnaoifuatia haki; ninyi mnaomtafuta BWANA; uangalieni mwamba ule ambao mlitolewa kwa kuchongwa, na tundu la shimo ambalo mlitolewa kwa kuchimbuliwa. Mwangalieni Abrahamu, baba yenu, na Sara, aliyewazaa; kwa maana alipokuwa mmoja tu nilimwita, nikambariki, nikamfanya kuwa wengi. Maana BWANA ameufariji Sayuni; amepafariji mahali pake palipokuwa ukiwa; amefanya nyika yake kuwa kama bustani ya Edeni, na jangwa lake kama bustani ya BWANA; shangwe na furaha zitaonekana ndani yake, kushukuru, na sauti ya kuimba. Nisikilizeni mimi, enyi watu wangu; nisikieni, taifa langu; maana sheria itatoka kwangu, na kutoa haki yangu iwe nuru ya mataifa. Haki yangu i karibu, wokovu wangu umekuwa wazi, na mikono yangu itawahukumu makabila ya watu; visiwa vitaningoja, navyo vitautumainia mkono wangu. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na ukombozi wangu hautakoma kamwe. Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope masuto ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao. Maana nondo atawala kama vazi, na funza atawala kama sufu; bali haki yangu itakuwa ya milele, na wokovu wangu hata vizazi vyote.
Isaya 51:1-8 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)
Nisikilizeni, ninyi mnaoifuatia haki; ninyi mnaomtafuta BWANA; uangalieni mwamba ule ambao mlitolewa kwa kuchongwa, na tundu la shimo ambalo mlitolewa kwa kuchimbuliwa. Mwangalieni Ibrahimu, baba yenu, na Sara, aliyewazaa; kwa maana alipokuwa mmoja tu nalimwita, nikambariki, nikamfanya kuwa wengi. Maana BWANA ameufariji Sayuni; amepafariji mahali pake palipokuwa ukiwa; amefanya jangwa lake kuwa kama bustani ya Edeni, na nyika yake kama bustani ya BWANA; furaha na kicheko zitaonekana ndani yake, kushukuru, na sauti ya kuimba. Nisikilizeni mimi, enyi watu wangu; nisikieni, taifa langu; maana sheria itatoka kwangu, nami nitaistarehesha hukumu yangu iwe nuru ya mataifa. Haki yangu i karibu, wokovu wangu umekuwa wazi, na mikono yangu itawahukumu kabila za watu; visiwa vitaningoja, navyo vitautumainia mkono wangu. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka. Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao. Maana nondo itawala kama vazi, na funza atawala kama sufu; bali haki yangu itakuwa ya milele, na wokovu wangu hata vizazi vyote.
Isaya 51:1-8 NEN (Neno)
“Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki na mnaomtafuta BWANA: Tazameni mwamba ambako mlichongwa, na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa; mwangalieni Abrahamu, baba yenu, na Sara, ambaye aliwazaa. Wakati nilimwita alikuwa mmoja tu, nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi. Hakika BWANA ataifariji Sayuni, naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote; atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni, nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani ya BWANA. Shangwe na furaha zitakuwa ndani yake, shukrani na sauti za kuimba. “Nisikilizeni, watu wangu; nisikieni, taifa langu: Sheria itatoka kwangu; haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa. Haki yangu inakaribia mbio, wokovu wangu unakuja, nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa. Visiwa vitanitegemea na kungojea mkono wangu kwa matumaini. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame dunia chini; mbingu zitatoweka kama moshi, dunia itachakaa kama vazi, na wakazi wake kufa kama inzi. Bali wokovu wangu utadumu milele, haki yangu haitakoma kamwe. “Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa, ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu: Msiogope mashutumu ya wanadamu wala msitiwe hofu na matukano yao. Kwa maana nondo atawala kama vazi, nao funza atawatafuna kama sufu. Lakini haki yangu itadumu milele, wokovu wangu kwa vizazi vyote.”