Isaya 50:4-11
Isaya 50:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Bwana Mungu amenipa ufasaha wa lugha, niwatie moyo wale waliochoka. Kila asubuhi hunipa hamu ya kusikiliza anayotaka kunifunza. Bwana Mungu amenifanya msikivu, nami sikuwa mkaidi wala kugeuka mbali naye. Mgongo wangu niliwaachia walionipiga, mashavu yangu waliozingoa ndevu zangu; walioniaibisha na kunitemea mate, sikujificha mbali nao. Bwana Mungu hunisaidia, kwa hiyo siwezi kufadhaika. Uso wangu nimeukaza kama jiwe; najua kwamba sitaaibishwa. Mtetezi wangu yuko karibu. Ni nani atakayepingana nami? Na aje tusimame mahakamani. Adui yangu ni nani? Na ajitokeze mbele basi. Tazama Bwana Mungu hunisaidia. Ni nani awezaye kusema nina hatia? Maadui zangu wote watachakaa kama vazi, nondo watawatafuna. Nani kati yenu amchaye Mwenyezi-Mungu? Nani anayetii maneno ya mtumishi wake? Kama yupo atembeaye gizani bila taa, amtumainie Mwenyezi-Mungu, na kumtegemea Mungu wake. Lakini nyinyi mnaowasha moto, na kujifanyia silaha za mienge, tembeeni kwa mwanga wa moto huo, miali ya moto mliowasha nyinyi wenyewe. Mtakachopata kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ni hiki: Nyinyi mtalala chini na mateso makali.
Isaya 50:4-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bwana MUNGU amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana MUNGU amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Niliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang'oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama jiwe, nami najua ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi. Tazama, Bwana MUNGU atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mwenye hatia? Tazama hao wote watachakaa kama vazi; nondo atawala. Ni nani miongoni mwenu amchaye BWANA, aitiiye sauti ya mtumishi wake? Yeye aendaye katika giza, wala hana nuru, naye alitumainia jina la BWANA, na kumtegemea Mungu wake. Tazama, ninyi nyote mwashao moto, mjifungiao hiyo mienge; endeni ninyi katika muali wa moto wenu, na katikati ya mienge mliyoiwasha. Mtayapata haya kwa mkono wangu; mtalala kwa huzuni.
Isaya 50:4-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bwana MUNGU amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana MUNGU amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi. Tazama, Bwana MUNGU atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa? Tazama hao wote watachakaa kama vazi; nondo atawala. Ni nani miongoni mwenu amchaye BWANA, aitiiye sauti ya mtumishi wake? Yeye aendaye katika giza, wala hana nuru, naye alitumainia jina la BWANA, na kumtegemea Mungu wake. Tazama, ninyi nyote mwashao moto, mjifungiao hiyo mienge; endeni ninyi katika mwali wa moto wenu, na katikati ya mienge mliyoiwasha. Mtayapata haya kwa mkono wangu; mtalala kwa huzuni.
Isaya 50:4-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA Mwenyezi amenipa ulimi uliofundishwa, ili kujua neno limtegemezalo aliyechoka. Huniamsha asubuhi kwa asubuhi, huamsha sikio langu lisikie kama mtu afundishwaye. BWANA Mwenyezi amezibua masikio yangu, nami sikuwa mwasi, wala sikurudi nyuma. Niliwapa mgongo wangu wale wanipigao, mashavu yangu wale wangʼoao ndevu zangu; sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha na kutemewa mate. Kwa sababu BWANA Mwenyezi ananisaidia, sitatahayarika. Kwa hiyo nimekaza uso wangu kama jiwe la gumegume, nami ninajua sitaaibika. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu. Ni nani basi atakayeleta mashtaka dhidi yangu? Tukabiliane uso kwa uso! Mshtaki wangu ni nani? Ni nani aliye mshtaki wangu? Ni BWANA Mwenyezi anisaidiaye mimi. Ni nani huyo atakayenihukumu? Wote watachakaa kama vazi, nondo watawala wawamalize. Ni nani miongoni mwenu amchaye BWANA, na kulitii neno la mtumishi wake? Yeye atembeaye gizani, yeye asiye na nuru, na alitumainie jina la BWANA, na amtegemee Mungu wake. Lakini sasa, ninyi nyote mnaowasha mioto, na kupeana mienge iwakayo ninyi kwa ninyi, nendeni, tembeeni katika nuru ya moto wenu na ya mienge mliyoiwasha. Hili ndilo mtakalolipokea kutoka mkononi mwangu: Mtalala chini kwa mateso makali.