Isaya 5:1-8
Isaya 5:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Nitaimba juu ya rafiki yangu, wimbo wa rafiki yangu na shamba lake la mizabibu: Rafiki yangu alikuwa na shamba la mizabibu juu ya kilima chenye rutuba nyingi. Alililima vizuri na kuondoa mawe yote, akaotesha humo mizabibu iliyochaguliwa; alijenga mnara wa ulinzi katikati yake, akachimba kisima cha kusindikia divai. Kisha akangojea lizae zabibu, lakini likazaa zabibu chungu. Kwa hiyo rafiki yangu anasema hivi: “Enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda, amueni tafadhali kati yangu na shamba langu. Ni kitu gani nilichokosa kulifanyia shamba langu? Na nilipotazamia lizae zabibu nzuri, mbona basi, likazaa zabibu chungu? “Na sasa nitawaambieni nitakavyolifanya hilo shamba langu. Nitauondoa ua wake, nalo litaharibiwa. Nitaubomoa ukuta wake, nalo litakanyagwakanyagwa. Nitaliacha liharibiwe kabisa, mizabibu yake haitapogolewa wala kupaliliwa. Litaota mbigili na miiba. Tena nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.” Naam! Shamba la mizabibu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi ni jumuiya ya Waisraeli, na mizabibu mizuri aliyoipanda ni watu wa Yuda. Yeye alitazamia watende haki, badala yake wakafanya mauaji; alitazamia uadilifu, badala yake wakasababisha kilio! Ole wao wanaonunua nyumba baada ya nyumba, wanaoongeza mashamba juu ya mashamba yao, mpaka kila sehemu inakuwa mali yao, na hamna nafasi kwa wengine nchini.
Isaya 5:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu kuhusu shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana; Akachimba handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibumwitu. Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. Je! Ni kazi gani iliyohitajika kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibumwitu? Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa ua wake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa; nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake. Kwa maana shamba la mizabibu la BWANA wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio. Ole wao waongezao nyumba baada ya nyumba, na kuweka shamba karibu na shamba, hadi ikawa hapana nafasi tena, nanyi ikawa hamna budi kukaa peke yenu katikati ya nchi!
Isaya 5:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana; Akafanya handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibu-mwitu. Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu? Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa; nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake. Kwa maana shamba la mizabibu la BWANA wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio. Ole wao waongezao nyumba baada ya nyumba, na kuweka shamba karibu na shamba, hata hapana nafasi tena, nanyi hamna budi kukaa peke yenu kati ya nchi!
Isaya 5:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nitaimba wimbo kwa mpenzi wangu, wimbo kuhusu shamba lake la mizabibu: Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu kwenye kilima chenye rutuba. Alililima na kuondoa mawe na akaliotesha mizabibu bora sana. Akajenga mnara wa ulinzi ndani yake, na kutengeneza shinikizo la kukamulia zabibu pia. Kisha akatazamia kupata mazao ya zabibu nzuri, lakini lilizaa matunda mabaya tu. “Basi enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda, hukumuni kati yangu na shamba langu la mizabibu. Ni nini zaidi ambacho kingefanyika katika shamba langu la mizabibu kuliko yale niliyofanya? Nilipotazamia kupata zabibu nzuri, kwa nini lilizaa zabibu mbaya tu? Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea shamba langu la mizabibu: Nitaondoa uzio wake, nalo litaharibiwa, nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa. Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu, halitakatiwa matawi wala kulimwa, nayo michongoma na miiba itamea huko, nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.” Shamba la mzabibu la BWANA wa majeshi ni nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni bustani yake ya kumpendeza. Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu; alitazamia uadilifu, lakini akasikia vilio vya taabu. Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba na kuunganisha mashamba baada ya mashamba hadi hakuna nafasi iliyobaki, nanyi mnaishi peke yenu katika nchi.