Isaya 49:13-26
Isaya 49:13-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Imbeni kwa furaha, enyi mbingu! Shangilia ewe dunia. Pazeni sauti mwimbe enyi milima, maana Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake, naam, atawaonea huruma watu wake wanaoteseka. Wewe Siyoni wasema: “Mwenyezi-Mungu ameniacha; hakika Bwana wangu amenisahau.” Lakini Mwenyezi-Mungu asema: “Je, mama aweza kumsahau mwanawe anayenyonya, asimwonee huruma mtoto wa tumbo lake? Hata kama mama aweza kumsahau mwanawe, mimi kamwe sitakusahau. Nimekuchora katika viganja vyangu; kuta zako naziona daima mbele yangu. Watakaokujenga upya wanakuja haraka, wale waliokuharibu wanaondoka. Inua macho uangalie pande zote; watu wako wote wanakusanyika na kukujia. Naapa kwa nafsi yangu mimi Mwenyezi-Mungu, watu wako watakuwa kwako kama mapambo, utawafurahia kama afanyavyo bibi arusi na utaji wake. “Kweli umekumbana na uharibifu, makao yako yamekuwa matupu, na nchi yako imeteketezwa. Lakini sasa itakuwa ndogo mno kwa wakazi wake; na wale waliokumaliza watakuwa mbali. Wanao waliozaliwa uhamishoni, watakulalamikia wakisema: ‘Nchi hii ni ndogo mno; tupatie nafasi zaidi ya kuishi.’ Hapo ndipo utakapojiuliza mwenyewe: ‘Nani aliyenizalia watoto wote hawa? Nilifiwa na wanangu bila kupata wengine. Nilipelekwa uhamishoni na kutupwa mbali; nani basi aliyewalea watoto hawa? Mimi niliachwa peke yangu, sasa, hawa wametoka wapi?’” Bwana Mungu asema hivi: “Nitayapungia mkono mataifa; naam, nitayapa ishara, nayo yatawabeba watoto wenu wa kiume, kadhalika na watoto wenu wa kike na kuwarudisha kwako. Wafalme watakushughulikia, na malkia watakutengenezea chakula. Watakusujudia na kukupa heshima, na kuramba vumbi iliyo miguuni pako. Hapo utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu; wote wanaonitegemea hawataaibika.” Watu wa Yerusalemu walalamika: “Je, shujaa aweza kunyanganywa nyara zake? Au mateka wa mtu katili waweza kuokolewa?” Mwenyezi-Mungu ajibu: “Naam! Hata nyara za shujaa zitachukuliwa, mateka wa mtu katili wataokolewa. Mimi mwenyewe nitawakabili maadui zako, mimi mwenyewe nitawaokoa watoto wako. Nitawafanya wanaokukandamiza watafunane; watalewa damu yao wenyewe kama divai. Hapo binadamu wote watatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mwokozi wako, mimi ni Mkombozi wako, Mwenye Nguvu wa Yakobo.”
Isaya 49:13-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; Pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake, Naye atawahurumia watu wake walioteswa. Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima. Watoto wako wafanya haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako. Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema BWANA, hakika utajivika hao wote kama pambo, nawe utajipamba kwao kama bibi arusi. Maana kuhusu mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao waliokumeza watakuwa mbali. Watoto ulionyang'anywa watasema masikioni mwako, Mahali hapa ni pembamba, hapanitoshi; nipe nafasi nipate kukaa. Ndipo utasema moyoni mwako, Ni nani aliyenizalia watoto hawa, na mimi nimefiwa na watoto wangu, nami niko peke yangu, nimehamishwa, ninatangatanga huko na huku? Tena ni nani aliyewalea hawa? Tazama, niliachwa peke yangu; hawa je! Walikuwa wapi? Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainulia mataifa mkono wangu, na kuwainulia makabila ya watu bendera yangu; nao wataleta wana wako vifuani mwao, na binti zako watachukuliwa mabegani mwao. Na wafalme watakuwa baba zako walezi, na malkia zao mama zako walezi; watainama mbele yako kifudifudi, na kuramba mavumbi ya miguu yako; nawe utajua ya kuwa mimi ni BWANA, tena waningojeao hawatatahayarika. Je! Aliye hodari aweza kunyang'anywa mateka wake, au mateka wa mtu katili kuokoka? Naam, BWANA asema hivi, Hata mateka wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka wake aliye katili wataokoka; kwa maana nitapambana na yeye abishanaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu. Na hao wanaokuonea nitawalisha nyama yao wenyewe, nao watalewa kwa kuinywa damu yao wenyewe, kama kwa mvinyo mpya; na watu wote watajua ya kuwa mimi, BWANA, ni mwokozi wako, na Mkombozi wako ni Mwenye enzi wa Yakobo.
Isaya 49:13-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; Pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake, Naye atawahurumia watu wake walioteswa. Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima. Watoto wako wafanya haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako. Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema BWANA, hakika utajivika na hao wote, kama kwa uzuri, nawe utajifungia hao, kama bibi arusi. Maana katika habari za mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao waliokumeza watakuwa mbali. Watoto ulionyang’anywa watasema masikioni mwako, Mahali hapa ni pembamba, hapanitoshi; nipe nafasi nipate kukaa. Ndipo utasema moyoni mwako, Ni nani aliyenizalia watoto hawa, na mimi nimefiwa na watoto wangu, nami ni peke yangu, nimehamishwa, ninatanga-tanga huko na huku? Tena ni nani aliyewalea hawa? Tazama, naliachwa peke yangu; hawa je! Walikuwa wapi? Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainulia mataifa mkono wangu, na kuwatwekea kabila za watu bendera yangu; nao wataleta wana wako vifuani mwao, na binti zako watachukuliwa mabegani mwao. Na wafalme watakuwa baba zako za kulea, na malkia zao mama zako za kulea; watainama mbele yako kifudifudi, na kuramba mavumbi ya miguu yako; nawe utajua ya kuwa mimi ni BWANA, tena waningojeao hawatatahayarika. Je! Aliye hodari aweza kunyang’anywa mateka yake, au jeshi lao waliofungwa halali wataokoka? Naam, BWANA asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka; kwa maana nitateta na yeye atetaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu. Na hao wanaokuonea nitawalisha nyama yao wenyewe, nao watalewa kwa kuinywa damu yao wenyewe, kama kwa mvinyo mpya; na wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, BWANA, ni mwokozi wako, na Mkombozi wako ni Mwenye enzi wa Yakobo.
Isaya 49:13-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu; furahi, ee dunia; pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima! Kwa maana BWANA anawafariji watu wake, naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa. Lakini Sayuni alisema, “BWANA ameniacha, Bwana amenisahau.” “Je, mama aweza kumsahau mtoto aliye matitini mwake akinyonya, wala asiwe na huruma juu ya mtoto aliyemzaa? Ingawa anaweza kusahau, mimi sitakusahau wewe! Tazama, nimekuchora kama muhuri katika vitanga vya mikono yangu, kuta zako zi mbele yangu daima. Wana wako wanaharakisha kurudi, nao wale waliokuteka wanaondoka kwako. Inua macho yako ukatazame pande zote: wana wako wote wanakusanyika na kukujia. Kwa hakika kama vile niishivyo, utawavaa wote kama mapambo, na kujifunga nao kama bibi arusi,” asema BWANA. “Ingawa uliangamizwa na kufanywa ukiwa, na nchi yako ikaharibiwa, sasa nafasi itakuwa finyu kwa ajili ya watu wako, nao wale waliokuangamiza watakuwa mbali sana. Watoto waliozaliwa wakati wa msiba wako bado watakuambia, ‘Mahali hapa ni finyu sana kwetu, tupe eneo kubwa zaidi la kuishi.’ Ndipo utasema moyoni mwako, ‘Ni nani aliyenizalia hawa? Nilikuwa nimefiwa, tena tasa; nilikuwa nimehamishwa na kukataliwa. Ni nani aliyewalea hawa? Niliachwa peke yangu, lakini hawa wametoka wapi?’ ” Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: “Tazama, nitawaashiria watu wa Mataifa, nitainua bendera yangu kwa mataifa; watawaleta wana wako mikononi yao, na kuwabeba binti zenu juu ya mabega yao. Wafalme watakuwa baba zenu wa kuwalea, na malkia wao watakuwa mama zenu wa kuwalea. Watasujudu mbele yako nyuso zao zikigusa chini; wataramba mavumbi yaliyo miguuni mwako. Ndipo utajua ya kuwa Mimi ndimi BWANA; wale wanaonitumaini mimi hawataaibika.” Je, nyara zaweza kuchukuliwa kutoka kwa mashujaa wa vita, au mateka kuokolewa kutoka kwa watu wakali? Lakini hili ndilo asemalo BWANA: “Naam, mateka watachukuliwa kutoka kwa mashujaa, na nyara zitapokonywa kutoka kwa watu wakali. Nitashindana na wale wanaoshindana nawe, nami nitawaokoa watoto wako. Nitawafanya wanaokudhulumu wale nyama yao wenyewe; watalewa kwa damu yao wenyewe, kama vile kwa mvinyo. Ndipo wanadamu wote watajua ya kuwa Mimi, BWANA, ni Mwokozi wako, Mkombozi wako, niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo.”