Isaya 49:1-26
Isaya 49:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Nisikilizeni, enyi nchi za mbali, tegeni sikio, enyi watu wa mbali! Mwenyezi-Mungu aliniita kabla sijazaliwa, alitaja jina langu nikiwa tumboni mwa mama yangu. Aliyapa ukali maneno yangu kama upanga mkali, alinificha katika kivuli cha mkono wake; aliufanya ujumbe wangu mkali kama ncha ya mshale, akanificha katika podo lake. Aliniambia, “Wewe ni mtumishi wangu; kwako, Israeli, watu watanitukuza.” Lakini mimi nikafikiri, “Nimeshughulika bure, nimetumia nguvu zangu bure kabisa.” Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu atanipa haki yangu; tuzo la kazi yangu liko kwa Mungu. Lakini asema sasa Mwenyezi-Mungu, ambaye aliniita tangu tumboni mwa mama yangu ili nipate kuwa mtumishi wake; nilirudishe taifa la Yakobo kwake, niwakusanye wazawa wa Israeli kwake. Mwenyezi-Mungu amenijalia heshima mbele yake. Mungu wangu amekuwa ndiye nguvu yangu. Yeye asema: “Haitoshi tu wewe kuwa mtumishi wangu, uyainue makabila ya Yakobo, na kurekebisha watu wa Israeli waliobaki. Nitakufanya uwe mwanga wa mataifa, niwaletee wokovu watu wote duniani.” Mwenyezi-Mungu, Mkombozi na Mtakatifu wa Israeli, amwambia hivi yule anayedharauliwa mno, yule anayechukiwa na mataifa, na ambaye ni mtumishi wa watawala: “Wafalme watakuona nao watasimama kwa heshima, naam, wakuu watainama na kukusujudia kwa sababu yangu mimi Mwenyezi-Mungu ambaye hutimiza ahadi zangu; kwa sababu yangu mimi Mtakatifu wa Israeli ambaye nimekuteua wewe.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nilikujibu ombi lako; wakati wa wokovu nilikusaidia. Nimekuweka na kukufanya uwe kiungo cha agano langu na mataifa yote: Kuirekebisha nchi iliyoharibika, na kuwarudishia wenyewe ardhi hiyo; kuwaambia wafungwa, ‘Tokeni humo gerezani’, na wale walio gizani, ‘Njoni nje mwangani!’ Kila mahali watakapokwenda watapata chakula hata kwenye vilima vitupu watapata malisho. Hawataona tena njaa wala kuwa na kiu. Upepo wa hari wala jua havitawachoma, mimi niliyewahurumia nitawaongoza na kuwapeleka kwenye chemchemi za maji. Milima yote nitaifanya kuwa njia, na barabara zangu kuu nitazitengeneza. Watu wangu watarudi kutoka mbali, wengine kutoka kaskazini na magharibi, wengine kutoka upande wa kusini.” Imbeni kwa furaha, enyi mbingu! Shangilia ewe dunia. Pazeni sauti mwimbe enyi milima, maana Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake, naam, atawaonea huruma watu wake wanaoteseka. Wewe Siyoni wasema: “Mwenyezi-Mungu ameniacha; hakika Bwana wangu amenisahau.” Lakini Mwenyezi-Mungu asema: “Je, mama aweza kumsahau mwanawe anayenyonya, asimwonee huruma mtoto wa tumbo lake? Hata kama mama aweza kumsahau mwanawe, mimi kamwe sitakusahau. Nimekuchora katika viganja vyangu; kuta zako naziona daima mbele yangu. Watakaokujenga upya wanakuja haraka, wale waliokuharibu wanaondoka. Inua macho uangalie pande zote; watu wako wote wanakusanyika na kukujia. Naapa kwa nafsi yangu mimi Mwenyezi-Mungu, watu wako watakuwa kwako kama mapambo, utawafurahia kama afanyavyo bibi arusi na utaji wake. “Kweli umekumbana na uharibifu, makao yako yamekuwa matupu, na nchi yako imeteketezwa. Lakini sasa itakuwa ndogo mno kwa wakazi wake; na wale waliokumaliza watakuwa mbali. Wanao waliozaliwa uhamishoni, watakulalamikia wakisema: ‘Nchi hii ni ndogo mno; tupatie nafasi zaidi ya kuishi.’ Hapo ndipo utakapojiuliza mwenyewe: ‘Nani aliyenizalia watoto wote hawa? Nilifiwa na wanangu bila kupata wengine. Nilipelekwa uhamishoni na kutupwa mbali; nani basi aliyewalea watoto hawa? Mimi niliachwa peke yangu, sasa, hawa wametoka wapi?’” Bwana Mungu asema hivi: “Nitayapungia mkono mataifa; naam, nitayapa ishara, nayo yatawabeba watoto wenu wa kiume, kadhalika na watoto wenu wa kike na kuwarudisha kwako. Wafalme watakushughulikia, na malkia watakutengenezea chakula. Watakusujudia na kukupa heshima, na kuramba vumbi iliyo miguuni pako. Hapo utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu; wote wanaonitegemea hawataaibika.” Watu wa Yerusalemu walalamika: “Je, shujaa aweza kunyanganywa nyara zake? Au mateka wa mtu katili waweza kuokolewa?” Mwenyezi-Mungu ajibu: “Naam! Hata nyara za shujaa zitachukuliwa, mateka wa mtu katili wataokolewa. Mimi mwenyewe nitawakabili maadui zako, mimi mwenyewe nitawaokoa watoto wako. Nitawafanya wanaokukandamiza watafunane; watalewa damu yao wenyewe kama divai. Hapo binadamu wote watatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mwokozi wako, mimi ni Mkombozi wako, Mwenye Nguvu wa Yakobo.”
Isaya 49:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi makabila ya watu mlio mbali sana; BWANA ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha; akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina BWANA, na thawabu yangu ina Mungu wangu. Na sasa BWANA asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya BWANA, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuyainua makabila ya Yakobo, na kuwarejesha watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia. BWANA, mkombozi wa Israeli, Mtakatifu wake, amwambia hivi yeye anayedharauliwa na wanadamu; yeye anayechukiwa na taifa hili; yeye aliye mtumishi wao watawalao; Wafalme wataona, watasimama; wakuu nao watasujudu; kwa sababu ya BWANA aliye mwaminifu, Mtakatifu wa Israeli aliyekuchagua. BWANA asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; joto halitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza. Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia zangu zote kuu zitainuliwa. Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya Sinimu. Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; Pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake, Naye atawahurumia watu wake walioteswa. Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima. Watoto wako wafanya haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako. Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema BWANA, hakika utajivika hao wote kama pambo, nawe utajipamba kwao kama bibi arusi. Maana kuhusu mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao waliokumeza watakuwa mbali. Watoto ulionyang'anywa watasema masikioni mwako, Mahali hapa ni pembamba, hapanitoshi; nipe nafasi nipate kukaa. Ndipo utasema moyoni mwako, Ni nani aliyenizalia watoto hawa, na mimi nimefiwa na watoto wangu, nami niko peke yangu, nimehamishwa, ninatangatanga huko na huku? Tena ni nani aliyewalea hawa? Tazama, niliachwa peke yangu; hawa je! Walikuwa wapi? Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainulia mataifa mkono wangu, na kuwainulia makabila ya watu bendera yangu; nao wataleta wana wako vifuani mwao, na binti zako watachukuliwa mabegani mwao. Na wafalme watakuwa baba zako walezi, na malkia zao mama zako walezi; watainama mbele yako kifudifudi, na kuramba mavumbi ya miguu yako; nawe utajua ya kuwa mimi ni BWANA, tena waningojeao hawatatahayarika. Je! Aliye hodari aweza kunyang'anywa mateka wake, au mateka wa mtu katili kuokoka? Naam, BWANA asema hivi, Hata mateka wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka wake aliye katili wataokoka; kwa maana nitapambana na yeye abishanaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu. Na hao wanaokuonea nitawalisha nyama yao wenyewe, nao watalewa kwa kuinywa damu yao wenyewe, kama kwa mvinyo mpya; na watu wote watajua ya kuwa mimi, BWANA, ni mwokozi wako, na Mkombozi wako ni Mwenye enzi wa Yakobo.
Isaya 49:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; BWANA ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha; akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina BWANA, na thawabu yangu ina Mungu wangu. Na sasa BWANA asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya BWANA, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia. BWANA, mkombozi wa Israeli, Mtakatifu wake, amwambia hivi yeye anayedharauliwa na wanadamu; yeye anayechukiwa na taifa hili; yeye aliye mtumishi wao watawalao; Wafalme wataona, watasimama; wakuu nao watasujudu; kwa sababu ya BWANA aliye mwaminifu, Mtakatifu wa Israeli aliyekuchagua BWANA asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza. Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia kuu zangu zitatukuzwa zote. Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya Sinimu. Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; Pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake, Naye atawahurumia watu wake walioteswa. Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima. Watoto wako wafanya haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako. Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema BWANA, hakika utajivika na hao wote, kama kwa uzuri, nawe utajifungia hao, kama bibi arusi. Maana katika habari za mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao waliokumeza watakuwa mbali. Watoto ulionyang’anywa watasema masikioni mwako, Mahali hapa ni pembamba, hapanitoshi; nipe nafasi nipate kukaa. Ndipo utasema moyoni mwako, Ni nani aliyenizalia watoto hawa, na mimi nimefiwa na watoto wangu, nami ni peke yangu, nimehamishwa, ninatanga-tanga huko na huku? Tena ni nani aliyewalea hawa? Tazama, naliachwa peke yangu; hawa je! Walikuwa wapi? Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainulia mataifa mkono wangu, na kuwatwekea kabila za watu bendera yangu; nao wataleta wana wako vifuani mwao, na binti zako watachukuliwa mabegani mwao. Na wafalme watakuwa baba zako za kulea, na malkia zao mama zako za kulea; watainama mbele yako kifudifudi, na kuramba mavumbi ya miguu yako; nawe utajua ya kuwa mimi ni BWANA, tena waningojeao hawatatahayarika. Je! Aliye hodari aweza kunyang’anywa mateka yake, au jeshi lao waliofungwa halali wataokoka? Naam, BWANA asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka; kwa maana nitateta na yeye atetaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu. Na hao wanaokuonea nitawalisha nyama yao wenyewe, nao watalewa kwa kuinywa damu yao wenyewe, kama kwa mvinyo mpya; na wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, BWANA, ni mwokozi wako, na Mkombozi wako ni Mwenye enzi wa Yakobo.
Isaya 49:1-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nisikilizeni, enyi visiwa, sikieni hili, ninyi mataifa mlio mbali: Kabla sijazaliwa, BWANA aliniita, tangu kuzaliwa kwangu, amelitaja jina langu. Akafanya kinywa changu kuwa kama upanga ulionolewa, katika uvuli wa mkono wake akanificha; akanifanya kuwa mshale uliosuguliwa, na kunificha katika podo lake. Akaniambia, “Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye ndani yake nitaonesha utukufu wangu.” Lakini nilisema, “Nimetumika bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida. Hata hivyo linalonistahili liko mkononi mwa BWANA, nao ujira wangu uko kwa Mungu wangu.” Sasa BWANA asema: yeye aliyeniumba tumboni kuwa mtumishi wake, kumrudisha tena Yakobo kwake na kumkusanyia Israeli, kwa maana nimepata heshima machoni pa BWANA, naye Mungu wangu amekuwa nguvu yangu; yeye asema: “Je, ni jambo dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kurejesha makabila ya Yakobo, na kuwarudisha wale Waisraeli niliowahifadhi? Pia nitakufanya uwe nuru kwa ajili ya watu wa Mataifa, ili upate kuleta wokovu wangu hata miisho ya dunia.” Hili ndilo asemalo BWANA, yeye Mkombozi na Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwake yeye aliyedharauliwa na kuchukiwa na taifa, kwa mtumishi wa watawala: “Wafalme watakuona na kusimama, wakuu wataona na kuanguka kifudifudi, kwa sababu ya BWANA, aliye mwaminifu, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, aliyekuchagua wewe.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Wakati wangu uliokubalika nitakujibu, nami katika siku ya wokovu nitakusaidia; nitakuhifadhi, nami nitakufanya kuwa agano kwa ajili ya watu, ili kurudisha nchi na kugawanyia urithi tena wale waliokuwa ukiwa, kuwaambia mateka, ‘Tokeni nje,’ nao wale walio gizani, ‘Kuweni huru!’ “Watajilisha kando ya barabara na kupata malisho yao juu ya kila kilima kilicho kitupu. Hawataona njaa wala kuona kiu, wala hari ya jangwani au jua halitawapiga. Yeye mwenye huruma juu yao atawaonesha njia, na kuwaongoza kando ya chemchemi za maji. Nitaifanya milima yangu yote kuwa barabara, na njia kuu zangu zitainuliwa. Tazama, watakuja kutoka mbali: wengine kutoka kaskazini, wengine kutoka magharibi, wengine kutoka nchi ya Sinimu.” Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu; furahi, ee dunia; pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima! Kwa maana BWANA anawafariji watu wake, naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa. Lakini Sayuni alisema, “BWANA ameniacha, Bwana amenisahau.” “Je, mama aweza kumsahau mtoto aliye matitini mwake akinyonya, wala asiwe na huruma juu ya mtoto aliyemzaa? Ingawa anaweza kusahau, mimi sitakusahau wewe! Tazama, nimekuchora kama muhuri katika vitanga vya mikono yangu, kuta zako zi mbele yangu daima. Wana wako wanaharakisha kurudi, nao wale waliokuteka wanaondoka kwako. Inua macho yako ukatazame pande zote: wana wako wote wanakusanyika na kukujia. Kwa hakika kama vile niishivyo, utawavaa wote kama mapambo, na kujifunga nao kama bibi arusi,” asema BWANA. “Ingawa uliangamizwa na kufanywa ukiwa, na nchi yako ikaharibiwa, sasa nafasi itakuwa finyu kwa ajili ya watu wako, nao wale waliokuangamiza watakuwa mbali sana. Watoto waliozaliwa wakati wa msiba wako bado watakuambia, ‘Mahali hapa ni finyu sana kwetu, tupe eneo kubwa zaidi la kuishi.’ Ndipo utasema moyoni mwako, ‘Ni nani aliyenizalia hawa? Nilikuwa nimefiwa, tena tasa; nilikuwa nimehamishwa na kukataliwa. Ni nani aliyewalea hawa? Niliachwa peke yangu, lakini hawa wametoka wapi?’ ” Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: “Tazama, nitawaashiria watu wa Mataifa, nitainua bendera yangu kwa mataifa; watawaleta wana wako mikononi yao, na kuwabeba binti zenu juu ya mabega yao. Wafalme watakuwa baba zenu wa kuwalea, na malkia wao watakuwa mama zenu wa kuwalea. Watasujudu mbele yako nyuso zao zikigusa chini; wataramba mavumbi yaliyo miguuni mwako. Ndipo utajua ya kuwa Mimi ndimi BWANA; wale wanaonitumaini mimi hawataaibika.” Je, nyara zaweza kuchukuliwa kutoka kwa mashujaa wa vita, au mateka kuokolewa kutoka kwa watu wakali? Lakini hili ndilo asemalo BWANA: “Naam, mateka watachukuliwa kutoka kwa mashujaa, na nyara zitapokonywa kutoka kwa watu wakali. Nitashindana na wale wanaoshindana nawe, nami nitawaokoa watoto wako. Nitawafanya wanaokudhulumu wale nyama yao wenyewe; watalewa kwa damu yao wenyewe, kama vile kwa mvinyo. Ndipo wanadamu wote watajua ya kuwa Mimi, BWANA, ni Mwokozi wako, Mkombozi wako, niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo.”