Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 45:1-25

Isaya 45:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Koreshi: “Wewe ni mfalme wangu niliyekuteua; mimi naitegemeza nguvu yako ili uyashinde mataifa mbele yako, na kuzivunja nguvu za wafalme. Mimi nayafungua malango ya mji mbele yako, na hakuna lango litakalofungwa. Mimi nitakutangulia, na kuisawazisha milima mbele yako. Nitaivunjavunja milango ya shaba, na kuvikatakata vizuizi vyake vya chuma. Nitakupa hazina zilizofichwa gizani, na mali iliyo mahali pa siri, upate kutambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninayekuita kwa jina lako. Kwa ajili ya mtumishi wangu Yakobo, naam, kwa ajili ya mteule wangu Israeli, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la heshima ingawa wewe hunijui. “Mimi ni Mwenyezi-Mungu, wala hakuna mwingine; hakuna Mungu mwingine ila mimi. Ninakuimarisha ingawa wewe hunijui, ili watu wote, toka mashariki hadi magharibi, wajue kwamba hakuna Mungu mwingine ila mimi; mimi ni Mwenyezi-Mungu na hakuna mwingine. Mimi hufanya mwanga na kuumba giza; huleta fanaka na kusababisha balaa. Mimi Mwenyezi-Mungu hutenda vitu hivi vyote. Enyi mbingu, nyesheni kutoka huko juu, mawingu na yadondoshe uadilifu; dunia na ifunuke, ichipushe wokovu, na kuchanusha uadilifu pia! Mimi, Mwenyezi-Mungu nimefanya hayo.” Ole wake mtu ashindanaye na Muumba wake, mtu aliye chombo cha udongo kushindana na mfinyanzi wake! Je, udongo humwuliza anayeufinyanga: “Unatengeneza nini hapa?” Au kumwambia, “Kazi yako si kamili!” Ole wake mtoto amwambiaye baba yake, “Kwa nini umenizaa?” Au amwambiaye mama yake, “Ya nini umenileta duniani?” Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli, Mungu, Muumba wa Israeli asema: “Je, mwathubutu kuniuliza juu ya watoto wangu, au kuniamuru juu ya kazi zangu mwenyewe? Ni mimi niliyeifanya dunia, na kuumba binadamu aishiye humo. Mikono yangu ndiyo iliyozitandaza mbingu, na jeshi lote la nyota liko kwa amri yangu. Ni mimi niliyemwamuru Koreshi kuchukua hatua, atekeleze matakwa yangu. Nitazifanikisha njia zake zote; ataujenga upya mji wangu Yerusalemu, na kuwapa uhuru watu wangu walio uhamishoni, bila kutaka malipo wala zawadi.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amesema. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Utajiri wa Misri na bidhaa za Kushi, pamoja na za watu wa Seba, majitu marefu, zitakuja kwako mwenyewe wewe taifa la Israeli, zote zitakuwa mali yako. Watu hao watakutumikia wamefungwa minyororo; watakusujudia na kukiri wakisema: ‘Kwako kuna Mungu wa kweli, wala hakuna Mungu mwingine ila yeye.’” Kweli wewe ni Mungu uliyefichika, Mungu wa Israeli, Mungu Mwokozi. Watengenezaji sanamu wataaibika na kufadhaika, wote kwa pamoja watavurugika. Lakini taifa la Israeli litaokolewa na Mwenyezi-Mungu, litapata wokovu wa milele. Halitaaibishwa wala kufadhaishwa milele. Mwenyezi-Mungu, Mungu pekee, ndiye aliyeiumba dunia, ndiye aliyeiumba na kuitegemeza. Hakuiumba iwe ghasia na tupu, ila aliiumba ikaliwe na viumbe vyake. Yeye asema sasa: “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, wala hakuna mwingine. Mimi sikunena kwa siri, wala katika nchi yenye giza. Mimi sikuwaambia wazawa wa Yakobo wanitafute katika ghasia. Mimi Mwenyezi-Mungu husema ukweli, maneno yangu ni ya kuaminika.” Enyi watu wa mataifa mliosalia, kusanyikeni pamoja mje! Nyinyi mmekosa akili: Nyinyi mwabeba sanamu za miti na kumwomba mungu asiyeweza kuokoa watu. Semeni wazi na kutoa hoja zenu; shaurianeni pamoja! Ni nani aliyetangaza zamani matukio ya sasa? Ni nani aliyetamka mambo haya zamani? Je, haikuwa mimi Mwenyezi-Mungu? Hakuna Mungu mwingine ila mimi! Mimi ni Mungu wa haki na mwokozi; hakuna mwingine ila mimi. Nigeukieni mimi mpate kuokolewa, popote mlipo duniani. Maana mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine. Mimi nimeapa kwa nafsi yangu, ninachotamka ni ukweli, neno langu halitarudi nyuma: Kila binadamu atanipigia magoti, kila mtu ataapa uaminifu. “Watasema juu yangu, ‘Haki na nguvu viko kwa Mwenyezi-Mungu peke yake.’” Wote waliomwakia hasira Mwenyezi-Mungu watamjia yeye na kuaibishwa. Lakini wazawa wa Israeli watapata ushindi kwake Mwenyezi-Mungu na kufurahi.

Shirikisha
Soma Isaya 45

Isaya 45:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Haya ndiyo BWANA amwambiayo Koreshi, masihi wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kulia, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza nguvu za wafalme; ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa. Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukatakata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli. Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua. Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakuimarisha ijapokuwa hukunijua; ili wapate kujua toka maawio ya jua, na toka magharibi, ya kuwa hapana mwingine zaidi ya mimi; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine. Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni BWANA, niyatendaye hayo yote. Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki; Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu, Nayo itoe haki ikamee pamoja; Mimi, BWANA, nimeiumba. Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unatengeneza nini? Au chombo ulichotengeneza hakina mikono? Ole wake amwambiaye baba yake, Wazaa nini? Au mwanamke, Una uchungu wa kujifungua nini? BWANA, Mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni. Mimi nimeiumba dunia, nimemhuluku mwanadamu juu yake; Mimi, naam, mikono yangu mimi, imezitanda mbingu, na jeshi lake lote nimeliamuru. Mimi nimemwinua katika haki, nami nitazinyosha njia zake zote; ataujenga mji wangu, naye atawaacha huru watu wangu waliohamishwa, si kwa kulipwa fedha, wala kwa kupewa zawadi, asema BWANA wa majeshi. BWANA asema hivi, Kazi ya Misri, na bidhaa ya Kushi, na Waseba, watu walio warefu, watakujia, nao watakuwa wako; watakufuata; watakuja katika minyororo; wataanguka chini mbele yako, watakuomba, wakisema, Hakika Mungu yu ndani yako; wala hapana mwingine, hapana Mungu tena. Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako, Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi. Watatahayarika, naam, watafadhaika, wote pia; wale watengenezao sanamu wataingia fadhaa pamoja. Bali Israeli wataokolewa na BWANA kwa wokovu wa milele; ninyi hamtatahayarika, wala kufadhaika, milele na milele. Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba iwe ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine. Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, BWANA, nasema ukweli; nanena mambo ya haki. Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka; hawana maarifa wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga; wamwombao mungu asiyeweza kuokoa. Hubirini, toeni habari; naam, na wafanye mashauri pamoja; ni nani aliyeonesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, BWANA? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine. Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa. Mmoja ataniambia, Kwa BWANA, peke yake, iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye, na wote waliomkasirikia watatahayarika. Katika BWANA wazao wote wa Israeli watapewa haki, na kutukuka.

Shirikisha
Soma Isaya 45

Isaya 45:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Haya ndiyo BWANA amwambiayo Koreshi, masihi wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya wafalme; ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa. Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli. Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua. Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua; ili wapate kujua toka maawio ya jua, na toka magharibi, ya kuwa hapana mwingine zaidi ya mimi; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine. Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni BWANA, niyatendaye hayo yote. Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki; Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu, Nayo itoe haki ikamee pamoja; Mimi, BWANA, nimeiumba. Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono? Ole wake amwambiaye baba yake, Wazaa nini? Au mwanamke, Una utungu wa nini? BWANA, Mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni. Mimi nimeiumba dunia, nimemhuluku mwanadamu juu yake; Mimi, naam, mikono yangu mimi, imezitanda mbingu, na jeshi lake lote nimeliamuru. Mimi nimemwinua katika haki, nami nitazinyosha njia zake zote; ataujenga mji wangu, naye atawaacha huru watu wangu waliohamishwa, si kwa kulipwa fedha, wala kwa kupewa zawadi, asema BWANA wa majeshi. BWANA asema hivi, Kazi ya Misri, na bidhaa ya Kushi, na Waseba, watu walio warefu, watakujilia, nao watakuwa wako; watakufuata; watakuja katika minyororo; wataanguka chini mbele yako, watakuomba, wakisema, Hakika Mungu yu ndani yako; wala hapana mwingine, hapana Mungu tena. Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako, Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi. Watatahayarika, naam, watafadhaika, wote pia; wale wafanyao sanamu wataingia fadhaa pamoja. Bali Israeli wataokolewa na BWANA kwa wokovu wa milele; ninyi hamtatahayarika, wala kufadhaika, milele na milele. Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine. Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, BWANA, nasema haki; nanena mambo ya adili. Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka; hawana maarifa wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga; wamwombao mungu asiyeweza kuokoa. Hubirini, toeni habari; naam, na wafanye mashauri pamoja; ni nani aliyeonyesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, BWANA? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine. Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa. Mmoja ataniambia, Kwa BWANA, peke yake, iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye, na wote waliomkasirikia watatahayarika. Katika BWANA wazao wote wa Israeli watapewa haki, na kutukuka.

Shirikisha
Soma Isaya 45

Isaya 45:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

“Hili ndilo asemalo BWANA kwa mpakwa mafuta wake, Koreshi, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume kutiisha mataifa mbele yake na kuwavua wafalme silaha zao, kufungua milango mbele yake ili malango yasije yakafungwa: Nitaenda mbele yako na kusawazisha milima; nitavunjavunja malango ya shaba na kukatakata mapingo ya chuma. Nitakupa hazina za gizani, mali iliyofichwa mahali pa siri, ili upate kujua kwamba Mimi ndimi BWANA, Mungu wa Israeli, akuitaye kwa jina lako. Kwa ajili ya Yakobo mtumishi wangu, Israeli niliyemchagua, nimekuita wewe kwa jina lako, na kukupa jina la heshima, ingawa wewe hunitambui. Mimi ndimi BWANA, wala hakuna mwingine, zaidi yangu hakuna Mungu. Nitakutia nguvu, ingawa wewe hujanitambua, ili kutoka mawio ya jua hadi machweo yake, watu wapate kujua kwamba hakuna Mungu mwingine ila Mimi. Mimi ndimi BWANA wala hakuna mwingine. Mimi ninaumba nuru na kuhuluku giza, ninaleta mafanikio na kusababisha maafa. Mimi, BWANA, huyatenda haya yote. “Enyi mbingu juu, nyesheni haki, mawingu na yaidondoshe. Dunia na ifunguke sana, wokovu na uchipuke, haki na ikue pamoja nao. Mimi, BWANA, ndiye niliyeiumba. “Ole wake yeye ashindanaye na Muumba wake, yeye ambaye ni kigae tu kati ya vigae juu ya ardhi. Je, udongo wa kufinyangia humwambia mfinyanzi, ‘Unatengeneza nini wewe?’ Je, kazi yako husema, ‘Hana mikono’? Ole wake amwambiaye baba yake, ‘Umezaa nini?’ Au kumwambia mama yake, ‘Umezaa kitu gani?’ “Hili ndilo asemalo BWANA, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake: Kuhusu mambo yatakayokuja, je, unaniuliza habari za watoto wangu, au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu? Mimi ndiye niliyeumba dunia na kumuumba mwanadamu juu yake. Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu, nikayapanga majeshi yake yote ya angani. Mimi nitamwinua Koreshi katika haki yangu: nitazinyoosha njia zake zote. Yeye atajenga mji wangu upya, na kuwaweka huru watu wangu walio uhamishoni, lakini si kwa kulipiwa fedha wala kupewa zawadi, asema BWANA wa majeshi.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Mazao ya Misri na bidhaa za Kushi, nao wale Waseba warefu, watakujia na kuwa wako, watakujia wakijikokota nyuma yako, watakujia wamefungwa minyororo. Watasujudu mbele yako, wakikusihi na kusema, ‘Hakika Mungu yu pamoja nawe, wala hakuna mwingine; hakuna Mungu mwingine.’ ” Hakika wewe u Mungu unayejificha, Ee Mungu na Mwokozi wa Israeli. Wote watengenezao sanamu wataaibika na kutahayarika; wataenda kutahayarika pamoja. Lakini Israeli ataokolewa na BWANA kwa wokovu wa milele; kamwe hutaaibika wala kutatahayarika, milele yote. Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA, yeye aliyeumba mbingu, ndiye Mungu; yeye aliyeifanya dunia na kuiumba, yeye ndiye aliiwekea misingi imara, hakuiumba ili iwe tupu, bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake. Anasema: “Mimi ndimi BWANA, wala hakuna mwingine. Sijasema sirini, kutoka mahali fulani katika nchi ya giza; sijawaambia wazao wa Yakobo, ‘Nitafuteni bure.’ Mimi, BWANA, nasema kweli; ninatangaza lililo sahihi. “Kusanyikeni pamoja mje, enyi wakimbizi kutoka mataifa. Wale wabebao sanamu za mti ni watu wasio na akili, wale waombao miungu isiyoweza kuokoa. Tangazeni litakalokuwepo, lisemeni hilo; wao na wafanye shauri pamoja. Ni nani aliyetangulia kusema hili tangu zamani, aliyelitangaza tangu zamani za kale? Je, haikuwa Mimi, BWANA? Wala hapana Mungu mwingine zaidi yangu mimi, Mungu mwenye haki na Mwokozi; hapana mwingine ila mimi. “Nigeukieni mimi, nanyi mkaokolewe, enyi miisho yote ya dunia; kwa maana mimi ndimi Mungu, wala hapana mwingine. Nimeapa kwa nafsi yangu, kinywa changu kimenena katika uadilifu wote neno ambalo halitatanguka: Kila goti litapigwa mbele zangu, kwangu mimi kila ulimi utaapa. Watasema kunihusu, ‘Katika BWANA peke yake ndiko kuna haki na nguvu.’ ” Wote ambao wamemkasirikia Mungu watamjia yeye, nao watatahayarika. Lakini katika BWANA wazao wote wa Israeli wataonekana wenye haki na watashangilia.

Shirikisha
Soma Isaya 45