Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 40:1-11

Isaya 40:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Wafarijini, wafarijini watu wangu, asema Mungu wenu. Sema na Yerusalemu kwa upole, umtangazie kwamba kazi yake ngumu imekamilika, kwamba dhambi yake imelipiwa fidia, kwamba amepokea kutoka mkononi mwa BWANA maradufu kwa ajili ya dhambi zake zote. Sauti ya mtu aliaye nyikani: “Itengenezeni njia ya BWANA jangwani, yanyoosheni mapito nyikani kwa ajili ya Mungu wetu. Kila bonde litainuliwa, kila mlima na kilima kitashushwa; penye mabonde patanyooshwa, napo palipoparuza patasawazishwa. Utukufu wa BWANA utafunuliwa, nao wanadamu wote watauona pamoja. Kwa maana kinywa cha BWANA kimenena.” Sauti husema, “Piga kelele.” Nami nikasema, “Nipige kelele gani?” “Wanadamu wote ni kama majani, nao utukufu wao wote ni kama maua ya kondeni. Majani hunyauka na maua huanguka, kwa sababu pumzi ya BWANA huyapuliza. Hakika wanadamu ni majani. Majani hunyauka na maua huanguka, lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.” Wewe uletaye habari njema Sayuni, panda juu ya mlima mrefu. Wewe uletaye habari njema Yerusalemu, paza sauti yako, piga kelele kwa nguvu, paza sauti, usiogope; iambie miji ya Yuda, “Yuko hapa Mungu wenu!” Tazameni, BWANA Mwenyezi anakuja na nguvu, nao mkono wake ndio utawalao kwa ajili yake. Tazameni, ujira wake u pamoja naye, nayo malipo yake yanafuatana naye. Huchunga kundi lake kama mchungaji wa mifugo: Hukusanya wana-kondoo katika mikono yake na kuwachukua karibu na moyo wake, huwaongoza taratibu wale wanaonyonyesha.

Shirikisha
Soma Isaya 40