Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 36:1-22 - Compare All Versions

Isaya 36:1-22 BHN (Biblia Habari Njema)

Mnamo mwaka wa kumi na nne wa utawala wa mfalme Hezekia, mfalme Senakeribu wa Ashuru aliishambulia miji yote yenye ngome ya Yuda na kuiteka. Kisha mfalme wa Ashuru alimtuma jemadari mkuu kutoka Lakishi na jeshi kubwa kumwendea mfalme Hezekia. Jemadari alisimama karibu na mfereji wa bwawa lililoko upande wa juu katika barabara kuu inayoelekea uwanda wa Dobi. Nao walilakiwa na Eliakimu mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa ikulu, Shebna aliyekuwa katibu, pamoja na mwandishi Yoa mwana wa Asafu. Ndipo mkuu wa matowashi wa Ashuru alipowaambia, “Mwambieni Hezekia kuwa mfalme mkuu wa Ashuru anamwuliza, ‘Je, unategemea nini kwa ukaidi wako huo? Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi? Angalia! Sasa unategemea Misri, utete uliovunjika ambao utamchoma mkono yeyote atakayeuegemea. Hivyo ndivyo Farao, mfalme wa Misri alivyo, kwa wote wale wanaomtegemea.’ Lakini hata kama mkiniambia, ‘Tunamtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,’ je, si huyohuyo ambaye Hezekia aliziharibu madhabahu zake na kuwaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, ‘Mnapaswa kuabudu mbele ya madhabahu hii?’ Basi, fanyeni mkataba na bwana wangu mfalme wa Ashuru; mimi nitawapatieni farasi 2,000, kama mtaweza kupata wapandafarasi. Mwawezaje kumrudisha nyuma ofisa mmoja kati ya watumishi wa bwana wangu aliye na cheo cha chini sana wakati mnategemea Misri kupata magari ya vita na wapandafarasi! Zaidi ya hayo, je, mnafikiri nimekuja bila amri ya Mwenyezi-Mungu ili kuishambulia na kuiangamiza nchi hii? Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeniambia ‘Ishambulie nchi hii na kuiangamiza!’” Kisha Eliakimu, Shebna na Yoa wakamjibu mkuu wa matowashi, “Tafadhali sema nasi kwa lugha ya Kiaramu maana tunaielewa. Usiseme nasi kwa lugha ya Kiebrania kwa kuwa watu walioko ukutani wanasikia.” Yule mkuu wa matowashi akawaambia, “Je unadhani bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu wenyewe tu? Maneno yangu ni pia kwa watu wanaokaa ukutani! Muda si muda wao kama vile nyinyi itawabidi kula mavi yao wenyewe na kunywa mikojo yao wenyewe!” Kisha huyo mkuu wa matowashi akasimama, akapaza sauti na kusema kwa Kiebrania, “Sikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! Hiki ndicho anachosema mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye, kwa sababu hataweza kuwaokoa. Msikubali awashawishi ili mumtegemee Mwenyezi-Mungu akisema, ‘Mwenyezi-Mungu hakika atatuokoa na mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’ Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru anasema: ‘Muwe na amani nami, na kujisalimisha kwangu. Hapo kila mmoja wenu ataweza kula matunda ya mzabibu wake mwenyewe na ya matunda ya mtini wake mwenyewe na kunywa maji ya kisima chake mwenyewe. Mpaka baadaye nitakapokuja na kuwapelekeni katika nchi kama hii yenu; nchi yenye nafaka na divai, nchi yenye mkate na mashamba ya mizabibu.’ Angalieni basi Hezekia asiwahadae akisema kwamba Mwenyezi-Mungu atawaokoeni. Je, kuna yoyote kati ya miungu ya mataifa aliyewahi kuokoa nchi yake mkononi mwa mfalme wa Ashuru? Je, iko wapi miungu ya Hamathi na Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu? Je, imeokoa Samaria mkononi mwangu? Ni nani miongoni mwa miungu ya nchi hizi aliyeokoa nchi zao katika mkono wangu, hata iwe kwamba Mwenyezi-Mungu ataweza kuuokoa mji wa Yerusalemu mkononi mwangu?” Lakini watu walinyamaza, wala hawakumjibu neno kama vile walivyoamriwa na mfalme akisema, “Msimjibu.” Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa mkuu wa ikulu, katibu Shebna, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi, wakamwendea mfalme Hezekia huku mavazi yao yakiwa yameraruliwa, wakamweleza maneno ya mkuu wa matowashi.

Shirikisha
Isaya 36 BHN

Isaya 36:1-22 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)

Ikawa, katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa. Mfalme wa Ashuru akamtuma amiri toka Lakishi hata Yerusalemu, kwa mfalme Hezekia, pamoja na jeshi kubwa. Naye akasimama karibu na mfereji wa birika ya juu, iliyo katika njia kuu ya kuuendea uwanda wa dobi. Wakamtokea Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe. Yule amiri akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kwamba mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia? Nasema, mashauri yako, na nguvu zako kwa vita, ni maneno yasiyo na maana; basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi? Tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliopondeka, yaani, Misri, ambayo, mtu akitegemea juu yake, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio. Lakini ukiniambia, Tunamtumaini BWANA, Mungu wetu, je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake mlimoinuka, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii? Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao. Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa akida mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi? Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la BWANA? BWANA ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule amiri, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa watu wote walio ukutani. Lakini yule amiri akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma kwa bwana wako, na kwako wewe, niseme maneno haya? Hakunituma kwa watu hawa walio ukutani, ili wale mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi? Kisha yule amiri akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akisema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru. Mfalme asema hivi; Hezekia asiwadanganye, kwa maana hataweza kuwaokoa; wala msimwache Hezekia kuwatia moyo wa kumtumaini BWANA; akisema, BWANA bila shaka atatuokoa, mji huu hautatiwa katika mkono wa mfalme wa Ashuru. Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie, mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika yake mwenyewe; hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu. Jihadharini, asije Hezekia akawadanganya, akisema, BWANA atatuokoa. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake na mkono wa mfalme wa Ashuru? Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je! Wameiokoa Samaria na mkono wangu? Katika miungu yote ya nchi hizi ni nani waliookoa nchi yao na mkono wangu, hata BWANA auokoe Yerusalemu na mkono wangu? Lakini watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana ilikuwa amri ya mfalme, kwamba, Msimjibu neno. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu mwenye kuandika tarehe, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zimeraruliwa, wakamwambia Hezekia maneno ya yule amiri.

Shirikisha
Isaya 36 SUV

Isaya 36:1-22 SRUV (Swahili Revised Union Version)

Ikawa, katika mwaka wa kumi na nne wa kutawala kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa. Mfalme wa Ashuru akamtuma amiri toka Lakishi pamoja na jeshi kubwa kwenda hadi Yerusalemu kwa mfalme Hezekia. Naye akasimama karibu na mfereji wa bwawa la juu, lililo katika njia kuu ya kuuendea Uwanda wa Dobi. Wakamtokea Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika kumbukumbu. Yule kamanda akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kwamba mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia? Nasema, mashauri yako, na nguvu zako kwa vita, ni maneno yasiyo na maana; basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi? Tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliovunjika, yaani, Misri, ambayo, mtu akitegemea juu yake, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio. Lakini ukiniambia, Tunamtumaini BWANA, Mungu wetu, je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake mlimoinuka, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii? Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao. Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa afisa mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi? Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la BWANA? BWANA ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule kamanda, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa watu wote walio ukutani. Lakini yule kamanda akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma niseme, maneno haya kwa bwana wako na kwako wewe? Hakunituma pia kwa watu hawa wanaokaa ukutani, wanaokabiliwa na tisho la kula mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi? Kisha yule kamanda akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akisema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru. Mfalme asema hivi; Hezekia asiwadanganye, kwa maana hataweza kuwaokoa; wala msimwache Hezekia kuwatia moyo wa kumtumaini BWANA; akisema, BWANA bila shaka atatuokoa, mji huu hautatiwa katika mkono wa mfalme wa Ashuru. Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie, mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya kisima chake mwenyewe; hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu. Jihadharini, Hezekia asije akawadanganya, akisema, BWANA atatuokoa. Je! Kati ya miungu ya mataifa, kuna yeyote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka kwa mkono wa mfalme wa Ashuru? Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je! Wameiokoa Samaria kutoka kwa mkono wangu? Katika miungu yote ya nchi hizi ni nani waliookoa nchi yao kutoka kwa mkono wangu, hata BWANA auokoe Yerusalemu kutoka kwa mkono wangu? Lakini watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana ilikuwa amri ya mfalme, kwamba, Msimjibu neno. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu mwenye kuandika kumbukumbu, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zikiwa zimeraruliwa, wakamwambia Hezekia maneno ya yule kamanda.

Shirikisha
Isaya 36 SRUV

Isaya 36:1-22 NEN (Neno)

Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka. Kisha mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wa jeshi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Jemadari wa jeshi akasimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi. Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakamwendea. Jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia, “ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako? Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi? Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea. Nawe ukiniambia, “Tunamtumainia BWANA Mungu wetu”: Je, si yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya”? “ ‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao! Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi? Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza nchi hii bila BWANA? BWANA mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ” Ndipo Eliakimu, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania watu walio juu ya ukuta wakiwa wanasikia.” Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioketi ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mkojo wao wenyewe?” Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, akasema: “Sikieni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! Hili ndilo asemalo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa! Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini BWANA kwa kuwaambia, ‘Hakika BWANA atatuokoa. Mji huu hautaangukia mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’ “Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwa mzabibu wake na mtini wake mwenyewe, na kunywa maji kutoka kisima chake mwenyewe, hadi nije nikawapeleke katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na ya mashamba ya mizabibu. “Msikubali Hezekia awapotoshe asemapo, ‘BWANA atatuokoa.’ Je, yuko mungu wa taifa lolote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru? Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu? Je, imeokoa Samaria kutoka mkononi mwangu? Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi BWANA aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?” Lakini wale watu wakakaa kimya, wala hawakujibu lolote, kwa kuwa mfalme alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lolote.” Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu, na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa, na kumwambia vile jemadari wa jeshi alivyosema.

Shirikisha
Isaya 36 NEN