Isaya 35:3-7
Isaya 35:3-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Imarisheni mikono yenu dhaifu, kazeni magoti yenu manyonge. Waambieni waliokufa moyo: “Jipeni moyo, msiogope! Tazameni Mungu wenu atakuja kulipiza kisasi, atakuja kuwaadhibu maadui zenu; atakuja yeye mwenyewe kuwaokoeni.” Hapo vipofu wataona tena, na viziwi watasikia tena. Walemavu watarukaruka kama paa, na bubu wataimba kwa furaha. Maji yatabubujika nyikani na vijito vya maji jangwani. Mchanga wa moto jangwani utakuwa bwawa la maji, ardhi kavu itabubujika vijito vya maji. Makao ya mbwamwitu yatajaa maji; nyasi zitamea na kukua kama mianzi.
Isaya 35:3-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yaimarisheni magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema atarukaruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung'aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi.
Isaya 35:3-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi.
Isaya 35:3-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea, waambieni wale wenye mioyo ya hofu, “Kuweni hodari, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja kulipa kisasi, pamoja na ujira wake, atakuja na kuwaokoa.” Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo kilema atarukaruka kama kulungu, nao ulimi wa aliye bubu utapaza sauti kwa shangwe. Maji yatatiririka kwa kasi katika nyika, na vijito katika jangwa. Mchanga wa moto utakuwa bwawa la maji, ardhi yenye kiu itabubujika chemchemi. Maskani ya mbweha walikolala hapo awali patamea nyasi, matete na mafunjo.