Isaya 35:1-8
Isaya 35:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Nyika na nchi kavu vitachangamka, jangwa litafurahi na kuchanua maua. Litachanua maua kwa wingi kama waridi, litashangilia na kuimba kwa furaha. Mungu atalijalia fahari ya milima ya Lebanoni, uzuri wa mlima Karmeli na wa bonde la Sharoni. Watu watauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu, watauona ukuu wa Mungu wetu. Imarisheni mikono yenu dhaifu, kazeni magoti yenu manyonge. Waambieni waliokufa moyo: “Jipeni moyo, msiogope! Tazameni Mungu wenu atakuja kulipiza kisasi, atakuja kuwaadhibu maadui zenu; atakuja yeye mwenyewe kuwaokoeni.” Hapo vipofu wataona tena, na viziwi watasikia tena. Walemavu watarukaruka kama paa, na bubu wataimba kwa furaha. Maji yatabubujika nyikani na vijito vya maji jangwani. Mchanga wa moto jangwani utakuwa bwawa la maji, ardhi kavu itabubujika vijito vya maji. Makao ya mbwamwitu yatajaa maji; nyasi zitamea na kukua kama mianzi. Humo kutakuwa na barabara kuu, nayo itaitwa “Njia Takatifu.” Watu najisi hawatapitia humo, ila tu watu wake Mungu; wapumbavu hawatadiriki kuikanyaga
Isaya 35:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa BWANA, ukuu wa Mungu wetu. Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yaimarisheni magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema atarukaruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung'aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi. Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.
Isaya 35:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa BWANA, ukuu wa Mungu wetu. Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi. Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.
Isaya 35:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Jangwa na nchi kame vitafurahi; nyika itashangilia na kuchanua maua. Kama waridi, litachanua maua, litashangilia sana na kupaza sauti kwa furaha. Litapewa utukufu wa Lebanoni, fahari ya Karmeli na Sharoni; wataona utukufu wa BWANA, fahari ya Mungu wetu. Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea, waambieni wale wenye mioyo ya hofu, “Kuweni hodari, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja kulipa kisasi, pamoja na ujira wake, atakuja na kuwaokoa.” Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo kilema atarukaruka kama kulungu, nao ulimi wa aliye bubu utapaza sauti kwa shangwe. Maji yatatiririka kwa kasi katika nyika, na vijito katika jangwa. Mchanga wa moto utakuwa bwawa la maji, ardhi yenye kiu itabubujika chemchemi. Maskani ya mbweha walikolala hapo awali patamea nyasi, matete na mafunjo. Nako kutakuwa na njia kuu, nayo itaitwa Njia ya Utakatifu. Wasio safi hawatapita juu yake; itakuwa ya wale wanaotembea katika Njia Ile; yeye asafiriye juu yake, ajapokuwa mjinga, hatapotea.