Isaya 33:13-24
Isaya 33:13-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikilizeni mambo mliyofanya enyi mlio mbali, nanyi mlio karibu kirini uwezo wangu.” Wenye dhambi katika Siyoni wanaogopa, wasiomcha Mungu wanatetemeka na kusema: “Nani awezaye kuukaribia moto huu mkali? Nani awezaye kustahimili miali ya moto wa milele?” Ni mtu aishiye kwa uadilifu na asemaye ukweli; mtu anayedharau kabisa utajiri wa dhuluma, anayekataa hongo kata kata, asiyekubali kamwe kusikia mipango ya mauaji, wala hakubali macho yake yaone maovu. Mtu wa namna hiyo anaishi juu, mahali salama penye ngome na miamba; chakula chake atapewa daima, na maji yake ya kunywa hayatakosekana. Mtaweza kumwona mfalme katika fahari yake, mtaiona nchi anayotawala, kubwa na pana. Mtafikiria tisho lililopita na kujiuliza, “Wako wapi wale waliokadiria na kukisia kodi? Wako wapi wale waliopeleleza ulinzi wetu?” Hamtawaona tena watu wale wenye kiburi, wanaozungumza lugha isiyoeleweka. Tazameni Siyoni tunamofanya sikukuu zetu; tazameni mji Yerusalemu, makao matulivu, hema imara; vigingi vyake havitangolewa kamwe, kamba zake hazitakatwa hata moja. Humo Mwenyezi-Mungu atatuonesha ukuu wake. Kutakuwa na mito mikubwa na vijito, ambamo meli za vita hazitapita, wala meli kubwa kuingia. Maana Mwenyezi-Mungu ni hakimu wetu, yeye ni mtawala wetu; Mwenyezi-Mungu ni mfalme wetu, yeye ndiye anayetuokoa. Ewe Siyoni, kamba zako zimelegea, haziwezi kushikilia matanga yake, wala kuyatandaza. Lakini nyara nyingi zitagawanywa; hata vilema wataweza kuchukua sehemu yao. Hakuna atakayesema tena ni mgonjwa; watu watasamehewa uovu wao wote.
Isaya 33:13-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uwezo wangu. Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uangamizao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele? Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung'utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za umwagaji wa damu; afumbaye macho yake asitazame uovu. Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma. Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana. Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? Yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? Yuko wapi yeye aliyeihesabu minara? Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuielewa. Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa makao ya raha; hema isiyotikisika; vigingi vyake havitang'olewa, wala kamba zake hazitakatika. Bali huko BWANA atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo. Kwa maana BWANA ndiye mwamuzi wetu; BWANA ndiye mfanya sheria wetu; BWANA ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa. Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka. Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.
Isaya 33:13-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uweza wangu. Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele? Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung’utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu. Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma. Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana. Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? Yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? Yuko wapi yeye aliyeihesabu minara? Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuelewa nayo. Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa kao la raha; hema isiyotanga-tanga; vigingi vyake havitang’olewa, wala kamba zake hazitakatika. Bali huko BWANA atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo. Kwa maana BWANA ndiye mwamuzi wetu; BWANA ndiye mfanya sheria wetu; BWANA ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa. Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka. Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.
Isaya 33:13-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ninyi mlio mbali sana, sikieni lile nililofanya; ninyi mlio karibu, tambueni uweza wangu! Wenye dhambi katika Sayuni wametiwa hofu, kutetemeka kumewakumba wasiomcha Mungu: “Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto ulao? Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto unaowaka milele?” Yeye aendaye kwa uadilifu na kusema lililo haki, yeye anayekataa faida ipatikanayo kwa dhuluma na kuizuia mikono yake isipokee rushwa, yeye azuiaye masikio yake dhidi ya mashauri ya mauaji, na yeye afumbaye macho yake yasitazame uovu: huyu ndiye mtu atakayeishi mahali pa juu, ambaye kimbilio lake litakuwa ngome ya mlimani. Atapewa mkate wake, na maji yake hayatakoma. Macho yenu yatamwona mfalme katika uzuri wake na kuiona nchi inayoenea mbali. Katika mawazo yenu mtaifikiria hofu iliyopita: “Yuko wapi yule afisa mkuu? Yuko wapi yule aliyechukua ushuru? Yuko wapi afisa msimamizi wa minara?” Hutawaona tena wale watu wenye kiburi, wale watu wenye usemi wa mafumbo, wenye lugha ngeni, isiyoeleweka. Mtazame Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yenu yatauona Yerusalemu, mahali pa amani pa kuishi, hema ambalo halitaondolewa, nguzo zake hazitangʼolewa kamwe, wala hakuna kamba yake yoyote itakayokatika. Huko BWANA atakuwa Mwenye Nguvu wetu. Patakuwa kama mahali pa mito mipana na vijito. Hakuna jahazi lenye makasia litakalopita huko, wala hakuna meli yenye nguvu itakayopita huko. Kwa kuwa BWANA ni mwamuzi wetu, BWANA ndiye mtoa sheria wetu, BWANA ni mfalme wetu, yeye ndiye atakayetuokoa. Kamba zenu za merikebu zimelegea: Mlingoti haukusimama imara, nalo tanga halikukunjuliwa. Wingi wa mateka yatagawanywa, hata yeye aliye mlemavu atachukua nyara. Hakuna yeyote aishiye Sayuni atakayesema, “Mimi ni mgonjwa”; nazo dhambi za wale wanaoishi humo zitasamehewa.