Isaya 30:1-9
Isaya 30:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ole wao watoto wanaoniasi, wanaotekeleza mipango yao na si mipango yangu, wanaofanya mikataba kinyume cha matakwa yangu! Naam, wanarundika dhambi juu ya dhambi. Bila kunitaka shauri, wanafunga safari kwenda Misri, kukimbilia usalama katika ulinzi wa Farao, kupata mahali pa usalama nchini Misri. Lakini ulinzi wa Farao utakuwa aibu yenu, na usalama nchini Misri utakuwa fedheha yenu. Maana ingawa maofisa wao wamefika Soani, na wajumbe wao mpaka Hanesi, wote wataaibishwa na hao wasioweza kuwasaidia, watu ambao hawawezi kuwapa msaada au faida, ila tu kuwapa aibu na fedheha.” Kauli ya Mungu juu ya wanyama wa pande za Negebu: “Wajumbe wanapita katika nchi ya taabu na shida, yenye simba, nyoka wa sumu na majoka. Wamewabebesha wanyama wao mali zao, kuwapelekea watu wasioweza kuwafaa kitu. Maana msaada wa Misri ni bure, haufai kitu; kwa hiyo nimeipanga Misri jina: ‘Joka lisilo na nguvu!’” Mungu aliniambia: “Sasa chukua kibao cha kuandikia, uandike jambo hili mbele yao, liwe ushahidi wa milele: Watu hawa ni waasi, watoto wasioaminika; watu wasiopenda kusikia mafunzo ya Mwenyezi-Mungu.
Isaya 30:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wa watoto waasi; asema BWANA; watakao mashauri lakini hawayataki kwangu mimi; wajifunikao kifuniko lakini si cha roho yangu; wapate kuongeza dhambi juu ya dhambi; waendao kuteremkia Misri wala hawakuuliza kinywani mwangu; ili wajitie nguvu kwa nguvu za Farao, na kutumainia kivuli cha Misri. Basi, nguvu za Farao zitakuwa aibu yenu, na kutumainia kivuli cha Misri kutakuwa aibu yenu. Kwa maana wakuu wake wako Soani, na wajumbe wake wamefika Hanesi. Wote watawaonea haya watu wasioweza kuwafaidia, wasio na msaada wala faida, bali ni aibu na sababu ya kushutumiwa. Ufunuo juu ya wanyama wa Negebu. Katikati ya nchi ya taabu na dhiki, Ambayo hutoka huko simba jike na simba angurumaye, Nyoka na joka la moto arukaye, Huchukua mali zao mabegani mwa punda wachanga, Na hazina zao juu ya nundu za ngamia Waende kwa watu ambao hawatawafaa kitu. Kwa maana msaada wa Misri haufai kitu na ni bure; Kwa hiyo nimemwita, “Rahabu aketiye kimya”. Haya, nenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele. Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA
Isaya 30:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wa watoto waasi; asema BWANA; watakao mashauri lakini hawayataki kwangu mimi; wajifunikao kifuniko lakini si cha roho yangu; wapate kuongeza dhambi juu ya dhambi; waendao kutelemkia Misri wala hawakuuliza kinywani mwangu; ili wajitie nguvu kwa nguvu za Farao, na kutumainia kivuli cha Misri. Basi, nguvu za Farao zitakuwa aibu yenu, na kutumainia kivuli cha Misri kutakuwa kufadhaika kwenu. Kwa maana wakuu wake wako Soani, na wajumbe wake wamefika Hanesi. Wote watawaonea haya watu wasioweza kuwafaidia, wasio na msaada wala faida, bali ni aibu na sababu ya kushutumiwa. Ufunuo juu ya hayawani wa Negebu. Katikati ya nchi ya taabu na dhiki, Ambayo hutoka huko simba jike na simba, Nyoka na joka la moto arukaye, Huchukua mali zao mabegani mwa punda wachanga, Na hazina zao juu ya nundu za ngamia Waende kwa watu ambao hawatawafaa kitu. Kwa maana Misri huwasaidia bure, bila faida; Kwa hiyo nimemwita, Rahabu aketiye kimya. Haya, enenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele. Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA
Isaya 30:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA asema, “Ole kwa watoto wakaidi, kwa wale wanaotimiza mipango ambayo si yangu, wakifanya makubaliano, lakini si kwa Roho wangu, wakilundika dhambi juu ya dhambi, wale wanaoshuka kwenda Misri bila kutaka ushauri wangu, wanaotafuta msaada wa ulinzi wa Farao, wanaotafuta kivuli cha Misri kiwe kimbilio. Lakini ulinzi wa Farao utakuwa kwa aibu yenu, kivuli cha Misri kitawaletea fedheha. Ingawa wana maafisa katika Soani na wajumbe wamewasili katika Hanesi, kila mmoja ataaibishwa kwa sababu ya taifa lisilowafaa kitu, ambalo haliwaletei msaada wala faida, bali aibu tu na fedheha.” Neno la unabii kuhusu wanyama wa Negebu: Katika nchi ya taabu na shida, ya simba za dume na jike, ya nyoka mwenye sumu kali na nyoka warukao, wajumbe huchukua utajiri wao juu ya migongo ya punda, hazina zao juu ya nundu za ngamia, kwa lile taifa lisilokuwa na faida, kuvipeleka Misri, ambaye msaada wake haufai kabisa. Kwa hiyo nimemwita “Rahabu Asiyefanya Chochote.” Nenda sasa, liandike neno hili juu ya kibao kwa ajili yao, liandike kwenye kitabu, ili liweze kuwa shahidi milele kwa ajili ya siku zijazo. Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu, watoto ambao hawataki kusikiliza mafundisho ya BWANA.