Isaya 26:1-9
Isaya 26:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ile watu wataimba wimbo huu katika nchi ya Yuda: Sisi tuna mji imara: Mungu anatulinda kwa kuta na ngome. Fungueni malango ya mji, taifa aminifu liingie; taifa litendalo mambo ya haki. Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti, wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea. Mtumaini Mwenyezi-Mungu siku zote kwa maana yeye ni mwamba wa usalama milele. Amewaporomosha waliokaa pande za juu, mji maarufu ameuangusha mpaka chini, ameutupa mpaka mavumbini. Sasa mji huo unakanyagwakanyagwa kwa miguu ya watu maskini na fukara. Njia ya watu wanyofu ni rahisi; ewe Mungu mwadilifu, wasawazisha njia yao. Katika njia ya maamuzi yako tunakungojea ee Mwenyezi-Mungu; kulikumbuka jina lako ndiyo tamaa yetu. Moyo wangu wakutamani usiku kucha, nafsi yangu yakutafuta kwa moyo. Utakapoihukumu dunia, watu wote ulimwenguni watajifunza haki.
Isaya 26:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma. Fungueni malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie. Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana BWANA YEHOVA ni mwamba wa milele. Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hadi chini, auleta hadi mavumbini. Mguu utaukanyaga chini, Naam, miguu yao walio maskini, Na hatua zao walio wahitaji. Njia yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. Naam, katika njia ya hukumu zako Sisi tumekungoja, Ee BWANA; Shauku ya nafsi zetu inaelekea Jina lako na ukumbusho wako. Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; Maana hukumu zako zikiwapo duniani, Watu wakaao duniani hujifunza haki.
Isaya 26:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma. Wekeni wazi malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie. Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana BWANA YEHOVA ni mwamba wa milele. Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini. Mguu utaukanyaga chini, Naam, miguu yao walio maskini, Na hatua zao walio wahitaji. Njia yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. Naam, katika njia ya hukumu zako Sisi tumekungoja, Ee BWANA; Shauku ya nafsi zetu inaelekea Jina lako na ukumbusho wako. Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; Maana hukumu zako zikiwapo duniani, Watu wakaao duniani hujifunza haki.
Isaya 26:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda: Tuna mji ulio na nguvu, Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake. Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia, taifa lidumishalo imani. Utamlinda katika amani kamilifu yeye ambaye moyo wake ni thabiti kwa sababu anakutumaini wewe. Mtumaini BWANA milele, kwa kuwa BWANA, BWANA, ni Mwamba wa milele. Huwashusha wale wajikwezao, huushusha chini mji wenye kiburi, huushusha hadi ardhini na kuutupa chini mavumbini. Miguu huukanyagia chini: miguu ya hao waliodhulumiwa, hatua za hao maskini. Mapito ya wenye haki ni nyoofu. Ewe uliye Mwenye Haki, waisawazisha njia ya mtu mnyofu. Naam, BWANA, tukienenda katika sheria zako, twakungojea wewe, jina lako na sifa zako ndizo shauku za mioyo yetu. Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku, wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku. Hukumu zako zinapokuja juu ya dunia, watu wa ulimwengu hujifunza haki.