Isaya 26:1-21
Isaya 26:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ile watu wataimba wimbo huu katika nchi ya Yuda: Sisi tuna mji imara: Mungu anatulinda kwa kuta na ngome. Fungueni malango ya mji, taifa aminifu liingie; taifa litendalo mambo ya haki. Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti, wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea. Mtumaini Mwenyezi-Mungu siku zote kwa maana yeye ni mwamba wa usalama milele. Amewaporomosha waliokaa pande za juu, mji maarufu ameuangusha mpaka chini, ameutupa mpaka mavumbini. Sasa mji huo unakanyagwakanyagwa kwa miguu ya watu maskini na fukara. Njia ya watu wanyofu ni rahisi; ewe Mungu mwadilifu, wasawazisha njia yao. Katika njia ya maamuzi yako tunakungojea ee Mwenyezi-Mungu; kulikumbuka jina lako ndiyo tamaa yetu. Moyo wangu wakutamani usiku kucha, nafsi yangu yakutafuta kwa moyo. Utakapoihukumu dunia, watu wote ulimwenguni watajifunza haki. Lakini waovu hata wakipewa fadhili, hawawezi kujifunza kutenda haki. Hata katika nchi ya wanyofu, wao bado wanatenda maovu, wala hawajali ukuu wako wewe Mwenyezi-Mungu. Ee Mwenyezi-Mungu umeinua mkono kuwaadhibu, lakini maadui zako hawauoni. Waoneshe uwapendavyo watu wako nao wataaibika. Moto wa hasira yako uwateketeze maadui zako! Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umetupatia amani; umefanikisha shughuli zetu zote. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, tulipata kutawaliwa na watu wengine na miungu yao, lakini twakiri wewe pekee kuwa Mungu wetu. Watu hao wamekufa, wala hawataishi tena; wamekuwa mizimu, wala hawatafufuka. Maana wewe umewaadhibu na kuwaangamiza, hakuna atakayeweza kuwakumbuka tena. Umelikuza taifa letu, ee Mwenyezi-Mungu, naam, umelizidisha taifa letu. Umeipanua mipaka yote ya nchi, kwa hiyo wewe watukuka. Ee Mwenyezi-Mungu, walipotaabika walikutafuta, walikuomba msaada ulipowaadhibu. Kama vile mama mjamzito anayejifungua hulia na kugaagaa kwa uchungu, ndivyo tulivyokuwa kwa sababu yako, ee Mwenyezi-Mungu. Sisi tulipata maumivu ya kujifungua lakini tukajifungua tu upepo! Hatukupata ushindi wowote kwa ajili ya nchi yetu, hatukuweza kuongeza idadi ya watu katika nchi. Wafu wako wataishi tena, miili yao itafufuka. Wanaolala mavumbini wataamka na kuimba kwa furaha! Mungu atapeleka umande wake wa uhai, nao walio kwa wafu watatoka hai. Njoni watu wangu, ingieni majumbani mwenu, mkajifungie humo ndani. Jificheni kwa muda mfupi, mpaka ifike ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Maana Mwenyezi-Mungu aja kutoka kwake juu, kutoka makao yake huko mbinguni; kuwaadhibu wakazi wa dunia kwa uovu wao. Nayo dunia haitaficha tena wale waliouawa, ila itaufichua umwagaji damu wote.
Isaya 26:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma. Fungueni malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie. Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana BWANA YEHOVA ni mwamba wa milele. Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hadi chini, auleta hadi mavumbini. Mguu utaukanyaga chini, Naam, miguu yao walio maskini, Na hatua zao walio wahitaji. Njia yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. Naam, katika njia ya hukumu zako Sisi tumekungoja, Ee BWANA; Shauku ya nafsi zetu inaelekea Jina lako na ukumbusho wako. Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; Maana hukumu zako zikiwapo duniani, Watu wakaao duniani hujifunza haki. Mtu mbaya ajapofadhiliwa, Hata hivyo hatajifunza haki; Katika nchi ya unyofu atatenda udhalimu, Wala hatauona utukufu wa BWANA. BWANA, mkono wako umeinuliwa, lakini hawaoni; lakini watauona wivu wako kwa ajili ya watu wako, nao watatahayari; naam, moto utawala adui zako. BWANA, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote. Ee BWANA, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametumiliki; lakini kwa msaada wako peke yako tutalitaja jina lako. Wao wamekufa, hawataishi; wamekwisha kufariki, hawatafufuka; kwa sababu hiyo umewajia, na kuwaangamiza, na kuupoteza ukumbusho wao. Umeliongeza hilo taifa, BWANA, umeliongeza taifa; wewe umetukuzwa, umeipanua mipaka yote ya nchi hii. BWANA, katika taabu zao walikwenda kwako; waliomba maombi mengi wakati adhabu yako ilipokuwa juu yao. Kama vile mwanamke mwenye mimba anayekaribia wakati wake wa kuzaa, alivyo na uchungu na kulia kwa sababu ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa sisi mbele zako, Ee BWANA. Tumekuwa na mimba, tumekuwa na uchungu, tumekuwa kana kwamba tumezaa upepo; hatukufanya wokovu wowote duniani, wala hawakuanguka wakaao duniani. Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa. Njooni, watu wangu, ingia wewe ndani ya vyumba vyako, ukafunge mlango nyuma yako ujifiche kitambo kidogo, mpaka ghadhabu hii itakapopita. Kwa maana, tazama, BWANA anakuja kutoka mahali pake, ili kuwaadhibu wakaao duniani, kwa sababu ya uovu wao; ardhi nayo itafunua damu yake, wala haitawafunika tena watu wake waliouawa.
Isaya 26:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma. Wekeni wazi malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie. Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana BWANA YEHOVA ni mwamba wa milele. Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini. Mguu utaukanyaga chini, Naam, miguu yao walio maskini, Na hatua zao walio wahitaji. Njia yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. Naam, katika njia ya hukumu zako Sisi tumekungoja, Ee BWANA; Shauku ya nafsi zetu inaelekea Jina lako na ukumbusho wako. Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; Maana hukumu zako zikiwapo duniani, Watu wakaao duniani hujifunza haki. Mtu mbaya ajapofadhiliwa, Hata hivyo hatajifunza haki; Katika nchi ya unyofu atatenda udhalimu, Wala hatauona utukufu wa BWANA. BWANA, mkono wako umeinuliwa, lakini hawaoni; lakini watauona wivu wako kwa ajili ya watu wako, nao watatahayari; naam, moto utawala adui zako. BWANA, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote. Ee BWANA, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametumiliki; lakini kwa msaada wako peke yako tutalitaja jina lako. Wao wamekufa, hawataishi; wamekwisha kufariki, hawatafufuka; kwa sababu hiyo umewajilia, na kuwaangamiza, na kuupoteza ukumbusho wao. Umeliongeza hilo taifa, BWANA, umeliongeza taifa; wewe umetukuzwa, umeipanua mipaka yote ya nchi hii. BWANA, katika taabu zao walikwenda kwako; waliomba maombi mengi wakati adhabu yako ilipokuwa juu yao. Kama vile mwanamke mwenye mimba anayekaribia wakati wake wa kuzaa, alivyo na utungu na kulia kwa sababu ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa sisi mbele zako, Ee BWANA. Tumekuwa na mimba, tumekuwa na utungu, tumekuwa kana kwamba tumezaa upepo; hatukufanya wokovu wo wote duniani, wala hawakuanguka wakaao duniani. Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa. Njoni, watu wangu, ingia wewe ndani ya vyumba vyako, ukafunge mlango nyuma yako ujifiche kitambo kidogo, mpaka ghadhabu hii itakapopita. Kwa maana, tazama, BWANA anakuja kutoka mahali pake, ili kuwaadhibu wakaao duniani, kwa sababu ya uovu wao; ardhi nayo itafunua damu yake, wala haitawafunika tena watu wake waliouawa.
Isaya 26:1-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda: Tuna mji ulio na nguvu, Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake. Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia, taifa lidumishalo imani. Utamlinda katika amani kamilifu yeye ambaye moyo wake ni thabiti kwa sababu anakutumaini wewe. Mtumaini BWANA milele, kwa kuwa BWANA, BWANA, ni Mwamba wa milele. Huwashusha wale wajikwezao, huushusha chini mji wenye kiburi, huushusha hadi ardhini na kuutupa chini mavumbini. Miguu huukanyagia chini: miguu ya hao waliodhulumiwa, hatua za hao maskini. Mapito ya wenye haki ni nyoofu. Ewe uliye Mwenye Haki, waisawazisha njia ya mtu mnyofu. Naam, BWANA, tukienenda katika sheria zako, twakungojea wewe, jina lako na sifa zako ndizo shauku za mioyo yetu. Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku, wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku. Hukumu zako zinapokuja juu ya dunia, watu wa ulimwengu hujifunza haki. Ingawa neema yaoneshwa kwa waovu, hawajifunzi haki; hata katika nchi ya unyofu huendelea kutenda mabaya wala hawazingatii utukufu wa BWANA. Ee BWANA, mkono wako umeinuliwa juu, lakini hawauoni. Wao na waone wivu wako kwa ajili ya watu wako tena waaibishwe, moto uliowekwa akiba kwa ajili ya adui zako na uwateketeze. BWANA, unaamuru amani kwa ajili yetu, yale yote tuliyoweza kuyakamilisha ni wewe uliyetenda kwa ajili yetu. Ee BWANA, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametutawala, lakini jina lako pekee ndilo tunaloliheshimu. Wao sasa wamekufa, wala hawako tena hai, roho za waliokufa hazitarudi tena. Uliwaadhibu na kuwaangamiza, umefuta kumbukumbu lao lote. Umeliongeza hilo taifa, Ee BWANA, umeliongeza hilo taifa. Umejipatia utukufu kwa ajili yako mwenyewe, umepanua mipaka yote ya nchi. BWANA, walikujia katika taabu yao, wewe ulipowarudi, waliweza kuomba kwa kunongʼona tu. Kama mwanamke mwenye mimba aliyekaribia kuzaa anavyogaagaa na kulia kwa ajili ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa mbele zako, Ee BWANA. Tulikuwa na mimba, tuligaagaa kwa maumivu, lakini tulizaa upepo. Hatukuleta wokovu duniani, hatujazaa watu katika ulimwengu huu. Lakini wafu wenu wataishi, nayo miili yao itafufuka. Ninyi mnaokaa katika mavumbi, amkeni mkashangilie kwa furaha. Umande wenu ni kama umande wa asubuhi, dunia itawazaa wafu wake. Nendeni, watu wangu, ingieni vyumbani mwenu na mfunge milango nyuma yenu, jificheni kwa kitambo kidogo hadi ghadhabu yake ipite. Tazama, BWANA anakuja kutoka makao yake ili kuwaadhibu watu wa dunia kwa ajili ya dhambi zao. Dunia itadhihirisha umwagaji damu juu yake, wala haitaendelea kuwaficha watu wake waliouawa.