Isaya 26:1-13
Isaya 26:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ile watu wataimba wimbo huu katika nchi ya Yuda: Sisi tuna mji imara: Mungu anatulinda kwa kuta na ngome. Fungueni malango ya mji, taifa aminifu liingie; taifa litendalo mambo ya haki. Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti, wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea. Mtumaini Mwenyezi-Mungu siku zote kwa maana yeye ni mwamba wa usalama milele. Amewaporomosha waliokaa pande za juu, mji maarufu ameuangusha mpaka chini, ameutupa mpaka mavumbini. Sasa mji huo unakanyagwakanyagwa kwa miguu ya watu maskini na fukara. Njia ya watu wanyofu ni rahisi; ewe Mungu mwadilifu, wasawazisha njia yao. Katika njia ya maamuzi yako tunakungojea ee Mwenyezi-Mungu; kulikumbuka jina lako ndiyo tamaa yetu. Moyo wangu wakutamani usiku kucha, nafsi yangu yakutafuta kwa moyo. Utakapoihukumu dunia, watu wote ulimwenguni watajifunza haki. Lakini waovu hata wakipewa fadhili, hawawezi kujifunza kutenda haki. Hata katika nchi ya wanyofu, wao bado wanatenda maovu, wala hawajali ukuu wako wewe Mwenyezi-Mungu. Ee Mwenyezi-Mungu umeinua mkono kuwaadhibu, lakini maadui zako hawauoni. Waoneshe uwapendavyo watu wako nao wataaibika. Moto wa hasira yako uwateketeze maadui zako! Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umetupatia amani; umefanikisha shughuli zetu zote. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, tulipata kutawaliwa na watu wengine na miungu yao, lakini twakiri wewe pekee kuwa Mungu wetu.
Isaya 26:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma. Fungueni malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie. Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana BWANA YEHOVA ni mwamba wa milele. Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hadi chini, auleta hadi mavumbini. Mguu utaukanyaga chini, Naam, miguu yao walio maskini, Na hatua zao walio wahitaji. Njia yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. Naam, katika njia ya hukumu zako Sisi tumekungoja, Ee BWANA; Shauku ya nafsi zetu inaelekea Jina lako na ukumbusho wako. Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; Maana hukumu zako zikiwapo duniani, Watu wakaao duniani hujifunza haki. Mtu mbaya ajapofadhiliwa, Hata hivyo hatajifunza haki; Katika nchi ya unyofu atatenda udhalimu, Wala hatauona utukufu wa BWANA. BWANA, mkono wako umeinuliwa, lakini hawaoni; lakini watauona wivu wako kwa ajili ya watu wako, nao watatahayari; naam, moto utawala adui zako. BWANA, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote. Ee BWANA, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametumiliki; lakini kwa msaada wako peke yako tutalitaja jina lako.
Isaya 26:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma. Wekeni wazi malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie. Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana BWANA YEHOVA ni mwamba wa milele. Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini. Mguu utaukanyaga chini, Naam, miguu yao walio maskini, Na hatua zao walio wahitaji. Njia yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. Naam, katika njia ya hukumu zako Sisi tumekungoja, Ee BWANA; Shauku ya nafsi zetu inaelekea Jina lako na ukumbusho wako. Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; Maana hukumu zako zikiwapo duniani, Watu wakaao duniani hujifunza haki. Mtu mbaya ajapofadhiliwa, Hata hivyo hatajifunza haki; Katika nchi ya unyofu atatenda udhalimu, Wala hatauona utukufu wa BWANA. BWANA, mkono wako umeinuliwa, lakini hawaoni; lakini watauona wivu wako kwa ajili ya watu wako, nao watatahayari; naam, moto utawala adui zako. BWANA, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote. Ee BWANA, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametumiliki; lakini kwa msaada wako peke yako tutalitaja jina lako.
Isaya 26:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda: Tuna mji ulio na nguvu, Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake. Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia, taifa lidumishalo imani. Utamlinda katika amani kamilifu yeye ambaye moyo wake ni thabiti kwa sababu anakutumaini wewe. Mtumaini BWANA milele, kwa kuwa BWANA, BWANA, ni Mwamba wa milele. Huwashusha wale wajikwezao, huushusha chini mji wenye kiburi, huushusha hadi ardhini na kuutupa chini mavumbini. Miguu huukanyagia chini: miguu ya hao waliodhulumiwa, hatua za hao maskini. Mapito ya wenye haki ni nyoofu. Ewe uliye Mwenye Haki, waisawazisha njia ya mtu mnyofu. Naam, BWANA, tukienenda katika sheria zako, twakungojea wewe, jina lako na sifa zako ndizo shauku za mioyo yetu. Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku, wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku. Hukumu zako zinapokuja juu ya dunia, watu wa ulimwengu hujifunza haki. Ingawa neema yaoneshwa kwa waovu, hawajifunzi haki; hata katika nchi ya unyofu huendelea kutenda mabaya wala hawazingatii utukufu wa BWANA. Ee BWANA, mkono wako umeinuliwa juu, lakini hawauoni. Wao na waone wivu wako kwa ajili ya watu wako tena waaibishwe, moto uliowekwa akiba kwa ajili ya adui zako na uwateketeze. BWANA, unaamuru amani kwa ajili yetu, yale yote tuliyoweza kuyakamilisha ni wewe uliyetenda kwa ajili yetu. Ee BWANA, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametutawala, lakini jina lako pekee ndilo tunaloliheshimu.