Isaya 16:1-14
Isaya 16:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Pelekeni wanakondoo kwa mtawala wa nchi, pelekeni kutoka Sela jangwani mpaka mlimani Siyoni. Kama ndege wanavyohangaika na kurukaruka, wakiwa wamefukuzwa kutoka viota vyao, ndivyo walivyo mabinti wa Moabu kwenye vivuko vya Arnoni. Wamoabu wanawaambia watu wa Yuda, “Tupeni mwongozo, tuamulieni. Enezeni ulinzi wenu juu yetu, kama vile usiku uenezavyo kivuli chake. Tuficheni sisi wakimbizi; msitusaliti sisi tuliofukuzwa. Wakimbizi wa Moabu waishi kwenu, muwe kimbilio lao mbali na mwangamizi.” Mdhalimu atakapokuwa ametoweka, udhalimu utakapokuwa umekoma, na wavamizi kutoweka nchini, utawala adili utazinduliwa katika maskani ya Daudi, mtawala apendaye kutenda haki, na mwepesi wa kufanya yaliyo sawa; atatawala humo kwa uaminifu. Watu wa Yuda wanasema hivi: “Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu, tunajua jinsi alivyojivuna mno; tumesikia juu ya majivuno, kiburi na ufidhuli wake; lakini majivuno yake hayo ni bure.” Sasa Wamoabu wanalia; wote wanaomboleza juu ya nchi yao. Ombolezeni kwa pigo hilo kubwa, na juu ya maandazi ya zabibu za Kir-haresethi. Mashamba ya Heshboni yamefifia. Kadhalika na zabibu za Sibma ambazo ziliwalevya wakuu wa mataifa zikafika Yazeri na kusambaa hata jangwani, chipukizi zake zikafika hata ngambo ya bahari. Kwa hiyo ninalia pamoja na Yazeri kwa ajili ya mizabibu ya Sibma. Machozi yananitoka kwa ajili yenu, enyi miji ya Heshboni na Eleale; maana vigelegele vya mavuno ya matunda, vigelegele vya mavuno ya nafaka vimetoweka. Furaha na shangwe zimetoweka katika shamba la rutuba. Kwenye mizabibu hakuna kuimba tena, wala kupiga vigelegele. Hakuna tena kukamua zabibu shinikizoni, sauti za furaha za mavuno zimekomeshwa. Hivyo, nafsi yangu yalilia Moabu kama kinubi, na moyo wangu kwa ajili ya mji wa Kir-heresi. Watu wa Moabu wanapojitokeza kuabudu mungu wao, wanapojichosha huko juu mahali pa ibada, wanapokwenda mahali pao patakatifu kusali, hawatakubaliwa. Hili ndilo jambo alilosema Mwenyezi-Mungu wakati uliopita kuhusu Moabu. Lakini sasa Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Baada ya miaka mitatu kamili, ikihesabiwa kama mfanyakazi anavyohesabu siku zake, fahari ya Moabu itakwisha. Ingawa watu wake ni wengi, watakaobaki hai watakuwa wachache na wanyonge.”
Isaya 16:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Pelekeni wana-kondoo, kodi yake aitawalaye nchi toka Sela kuelekea jangwani, mpaka mlima wa binti Sayuni. Na binti za Moabu watakuwa kama ndege warukao huku na huko, kama kiota cha ndege waliotiwa hofu, kwenye vivuko vya Arnoni. Lete shauri; kata neno; fanya kivuli chako kuwa kama usiku kati ya mchana; wafiche waliofukuzwa; usiwachongee waliopotea. Watu wangu waliofukuzwa waache wakae pamoja nawe; katika habari za Moabu, uwe kimbilio kwake mbele ya uso wake anayeharibu; maana yeye atozaye kwa nguvu amekoma; afanyaye ukiwa ametoweka; waliokanyaga watu wametoka katika nchi. Na kiti cha enzi kitafanywa imara kwa rehema; na mmoja ataketi juu yake katika kweli, katika hema ya Daudi; akifanya hukumu, akitaka sana yaliyo haki, mwepesi wa kutenda haki. Tumesikia habari za kiburi cha Moabu, ya kwamba ni mwenye kiburi kingi; habari za majivuno yake, na kiburi chake, na ghadhabu yake; majivuno yake si kitu. Kwa sababu hiyo Moabu atalia kwa ajili ya Moabu, kila mmoja atalia, maana mtaiombolezea mikate ya zabibu ya Kir-Haresethi, mkipigwa sana. Maana mashamba ya Heshboni yamenyauka, na mzabibu wa Sibma; mabwana wa mataifa wameyavunja matawi yake mateule; yamefika hadi Yazeri, yalitangatanga hadi jangwani matawi yake yalitapakaa, yaliivuka bahari. Basi, naililia mizabibu ya Sibma kwa kilio cha Yazeri, nitawanyeshea machozi yangu, Ee Heshboni na Eleale, kwa kuwa kelele za vita zimeyaangukia mavuno ya matunda yako, na mavuno ya mizabibu yako. Na furaha imeondolewa, na shangwe toka mashamba yaliyozaa sana; hapana kuimba katika mashamba ya mizabibu, wala sauti za furaha; akanyagaye hakanyagi divai katika mashinikizo; nimeikomesha sauti ya furaha yake akanyagaye. Kwa sababu hiyo mtima wangu unamlilia Moabu kama kinubi, na nafsi yangu kwa ajili ya Kir-Heresi. Tena itakuwa, Moabu akionekana, na kujichosha kwa kulia juu ya mahali pa juu, na kuingia katika patakatifu pake aombe, hatapata kushinda. Hilo ndilo neno lile alilolisema BWANA juu ya Moabu zamani. Lakini sasa BWANA asema hivi, Katika muda wa miaka mitatu, kama miaka ya mtu wa mshahara, utukufu wa Moabu utadharauliwa, licha ya wingi wa watu wake; na watakaobaki watakuwa wachache sana na dhaifu.
Isaya 16:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Pelekeni wana-kondoo, kodi yake aitawalaye nchi toka Sela kuelekea jangwani, mpaka mlima wa binti Sayuni. Na binti za Moabu watakuwa kama ndege warukao huko na huko, kama kioto cha ndege waliotiwa hofu, kwenye vivuko vya Arnoni. Lete shauri; kata neno; fanya kivuli chako kuwa kama usiku kati ya mchana; wafiche waliofukuzwa; usiwachongee waliopotea. Watu wangu waliofukuzwa waache wakae pamoja nawe; katika habari za Moabu, uwe sitara kwake mbele ya uso wake anayeharibu; maana yeye atozaye kwa nguvu amekoma; afanyaye ukiwa ametoweka; waliokanyaga watu wametoka katika nchi. Na kiti cha enzi kitafanywa imara kwa rehema; na mmoja ataketi juu yake katika kweli, katika hema ya Daudi; akifanya hukumu, akitaka sana yaliyo haki, mwepesi wa kutenda haki. Tumesikia habari za kiburi cha Moabu, ya kwamba ni mwenye kiburi kingi; habari za majivuno yake, na kiburi chake, na ghadhabu yake; majivuno yake si kitu. Kwa sababu hiyo Moabu atalia kwa ajili ya Moabu, kila mmoja atalia, maana mtaiombolezea mikate ya zabibu ya Kir-Haresethi, mkipigwa sana. Maana makonde ya Heshboni yamenyauka, na mzabibu wa Sibma; mabwana wa mataifa wameyavunja matawi yake mateule; yamefika hata Yazeri, yalitanga-tanga hata nyikani; matawi yake yalitapakaa, yaliivuka bahari. Basi, naililia mizabibu ya Sibma kwa kilio cha Yazeri, nitawanyeshea machozi yangu, Ee Heshboni na Eleale, kwa kuwa kelele za vita zimeyaangukia mavuno ya matunda yako, na mavuno ya mizabibu yako. Na furaha imeondolewa, na shangwe toka mashamba yaliyozaa sana; hapana kuimba katika mashamba ya mizabibu, wala sauti za furaha; akanyagaye hakanyagi divai katika mashinikizo; nimeikomesha sauti ya furaha yake akanyagaye. Kwa sababu hiyo mtima wangu unamlilia Moabu kama kinubi, na matumbo yangu kwa ajili ya Kir-Heresi. Tena itakuwa, Moabu akionekana, na kujichosha kwa kulia juu ya mahali pa juu, na kuingia katika patakatifu pake aombe, hatapata kushinda. Hilo ndilo neno lile alilolisema BWANA juu ya Moabu zamani. Lakini sasa BWANA asema hivi, Katika muda wa miaka mitatu, kama miaka ya mtu wa mshahara, utukufu wa Moabu utadharauliwa, pamoja na wingi wake wote; mabaki yake yatakuwa machache sana, kama si kitu kabisa.
Isaya 16:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Pelekeni wana-kondoo kama ushuru kwa mtawala wa nchi, Kutoka Sela, kupitia jangwani, hadi mlima wa Binti Sayuni. Kama ndege wanaopapatika waliofukuzwa kutoka kiota, ndivyo walivyo wanawake wa Moabu kwenye vivuko vya Mto Arnoni. “Tupeni shauri, toeni uamuzi. Wakati wa adhuhuri, fanyeni kivuli chenu kama usiku. Waficheni watoro, msisaliti wakimbizi. Waacheni watoro wa Moabu wakae pamoja nanyi; kuweni mahali pao pa salama ili kuepuka mwangamizi.” Mtesi atafikia mwisho na maangamizi yatakoma, aletaye vita atatoweka kutoka nchi. Kwa upendo kiti cha utawala kitaimarishwa, kwa uaminifu mtu ataketi juu yake, yeye atokaye nyumba ya Daudi: yeye ambaye katika kuhukumu hutafuta haki, na huhimiza njia ya haki. Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu: kiburi chake cha kujivuna na udanganyifu, kiburi chake na ufidhuli wake, lakini majivuno yake si kitu. Kwa hiyo Wamoabu wanaomboleza, wanaiombolezea Moabu kwa pamoja. Wanaomboleza na kuhuzunika kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi. Mashamba ya Heshboni yananyauka, pia na mizabibu ya Sibma. Watawala wa mataifa wamekanyaga mizabibu iliyo mizuri sana, ambayo ilipata kufika Yazeri na kuenea kuelekea jangwani. Machipukizi yake yalienea yakafika hadi baharini. Hivyo ninalia kama Yazeri aliavyo, kwa ajili ya mizabibu ya Sibma. Ee Heshboni, ee Eleale, ninakulowesha kwa machozi! Shangwe za furaha kwa ajili ya tunda lako lililoiva na kwa ajili ya mavuno zimekomeshwa. Furaha na shangwe zimeondolewa kutoka mashamba ya matunda; hakuna yeyote aimbaye wala apazaye sauti katika mashamba ya mizabibu; hakuna yeyote akanyagaye zabibu shinikizoni, kwa kuwa nimekomesha makelele. Moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama kinubi, nafsi yangu yote kwa ajili ya Kir-Haresethi. Moabu anapojitokeza mahali pake pa juu pa kuabudia, anajichosha mwenyewe tu; anapoenda mahali pake pa ibada za sanamu ili kuomba, haitamfaidi lolote. Hili ndilo neno ambalo BWANA ameshasema kuhusu Moabu. Lakini sasa BWANA anasema: “Katika miaka mitatu, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, fahari ya Moabu na watu wake wengi watadharauliwa, nao walionusurika watakuwa wachache sana, tena wanyonge.”