Isaya 14:3-14
Isaya 14:3-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Ewe Israeli, wakati Mwenyezi-Mungu atakapokufariji baada ya mateso, misukosuko na utumwa uliofanyiwa, utaimba utenzi huu wa kumdhihaki mfalme wa Babuloni: “Jinsi gani mdhalimu alivyokomeshwa! Ujeuri wake umekomeshwa! Mwenyezi-Mungu amelivunja gongo la waovu, ameivunja fimbo ya kifalme ya watawala, ambao walipiga nayo watu kwa hasira bila kukoma, na kuwatawala kwa udhalimu bila huruma. Sasa dunia yote ina utulivu na amani, kila mtu anaimba kwa furaha. Misonobari inafurahia kuanguka kwako, nayo mierezi ya Lebanoni pamoja yasema: ‘Kwa vile sasa umeangushwa, hakuna mkata miti atakayekuja dhidi yetu!’ “Kuzimu nako kumechangamka, ili kukulaki wakati utakapokuja. Kunaiamsha mizimu ije kukusalimu na wote waliokuwa wakuu wa dunia; huwaamsha kutoka viti vyao vya enzi wote waliokuwa wafalme wa mataifa. Wote kwa pamoja watakuambia: ‘Nawe pia umedhoofika kama sisi! Umekuwa kama sisi wenyewe! Fahari yako imeteremshwa kuzimu pamoja na muziki wa vinubi vyako. Chini mabuu ndio kitanda chako, na wadudu ndio blanketi lako!’ “Jinsi gani ulivyoporomoshwa toka mbinguni, wewe uliyekuwa nyota angavu ya alfajiri. Jinsi gani ulivyoangushwa chini, wewe uliyeyashinda mataifa! Wewe ulijisemea moyoni mwako: ‘Nitapanda mpaka mbinguni; nitaweka kiti changu juu ya nyota za Mungu, nitaketi juu ya mlima wakutanapo miungu, huko mbali pande za kaskazini. Nitapanda vilele vya mawingu nitajifanya kuwa sawa na Mungu Mkuu.’
Isaya 14:3-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena itakuwa katika siku ile, ambayo BWANA atakupa raha baada ya huzuni yako, na baada ya taabu yako, na baada ya utumishi ule mgumu uliotumikishwa; utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema, Jinsi mdhalimu alivyokoma; Jinsi ulivyokoma mji ule wenye ujeuri! BWANA amelivunja gongo la wabaya, Fimbo ya enzi yao wenye kutawala. Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu, Kwa mapigo yasiyokoma; Aliyewatawala mataifa kwa hasira, Ameadhibiwa asizuie mtu. Dunia yote inastarehe na kutulia; Nao wanashangilia kwa kuimba. Naam, misonobari inakufurahia, Na mierezi ya Lebanoni, ikisema, Tokea wakati ulipolazwa chini wewe, Hapana mkata miti aliyetujia. Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako, Ili kukulaki utakapokuja; Huwaamsha waliokufa kwa ajili yako, Naam, walio wakuu wote wa dunia; Huwainua wafalme wote wa mataifa, Watoke katika viti vyao vya enzi. Hao wote watajibu na kukuambia, Je! Wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi! Fahari yako imeshushwa hadi kuzimu, Na sauti ya vinanda vyako; Funza wametandazwa chini yako, Na vidudu vinakufunika. Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye Juu.
Isaya 14:3-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena itakuwa katika siku ile, ambayo BWANA atakupa raha baada ya huzuni yako, na baada ya taabu yako, na baada ya utumishi ule mgumu uliotumikishwa; utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema, Jinsi alivyokoma mwenye kuonea; Jinsi ulivyokoma mji ule wenye jeuri! BWANA amelivunja gongo la wabaya, Fimbo ya enzi yao wenye kutawala. Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu, Kwa mapigo yasiyokoma; Aliyewatawala mataifa kwa hasira, Ameadhibiwa asizuie mtu. Dunia yote inastarehe na kutulia; Hata huanzilisha kuimba. Naam, misunobari inakufurahia, Na mierezi ya Lebanoni, ikisema, Tokea wakati ulipolazwa chini wewe, Hapana mkata miti aliyetujia. Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako, Ili kukulaki utakapokuja; Huwaamsha waliokufa kwa ajili yako, Naam, walio wakuu wote wa dunia; Huwainua wafalme wote wa mataifa, Watoke katika viti vyao vya enzi. Hao wote watajibu na kukuambia, Je! Wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi! Fahari yako imeshushwa hata kuzimu, Na sauti ya vinanda vyako; Funza wametandazwa chini yako, Na vidudu vinakufunika. Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu.
Isaya 14:3-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika siku BWANA atakapokuondolea mateso, udhia na utumwa wa kikatili, utaichukua dhihaka hii dhidi ya mfalme wa Babeli: Tazama jinsi mtesi alivyofikia mwisho! Tazama jinsi ghadhabu yake kali ilivyokoma! BWANA amevunja fimbo ya mwovu, fimbo ya utawala ya watawala, ambayo kwa hasira waliyapiga mataifa kwa mapigo yasiyo na kikomo, nao kwa ghadhabu kali waliwatiisha mataifa kwa jeuri pasipo huruma. Nchi zote ziko kwenye mapumziko na kwenye amani, wanabubujika kwa kuimba. Hata misunobari na mierezi ya Lebanoni inashangilia mbele yako na kusema, “Basi kwa kuwa umeangushwa chini, hakuna mkata miti atakayekuja kutukata.” Kuzimu kumetaharuki kukulaki unapokuja, kunaamsha roho za waliokufa ili kukupokea, wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu, kunawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme: wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa. Wote wataitikia, watakuambia, “Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo; wewe umekuwa kama sisi.” Majivuno yako yote yameshushwa hadi Kuzimu, pamoja na kelele ya vinubi vyako, mafunza yametanda chini yako, na minyoo imekufunika. Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko! Umetupwa chini duniani, wewe uliyepata kuangusha mataifa! Ulisema moyoni mwako, “Nitapanda juu hadi mbinguni, nitakiinua kiti changu cha utawala juu ya nyota za Mungu; nitaketi nimetawazwa juu ya mlima wa kusanyiko, kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu. Nitapaa juu kupita mawingu, nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”