Isaya 13:1-22
Isaya 13:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Kauli ya Mungu dhidi ya Babuloni ambayo Isaya, mwana wa Amozi, alipewa katika maono: Mungu asema: “Twekeni bendera juu ya mlima usio na miti. Wapaazieni sauti askari wapungieni watu mkono waingie malango ya mji wa wakuu. Mimi nimewaamuru wateule wangu, nimewaita mashujaa wangu, hao wenye kunitukuza wakishangilia, waje kutekeleza lengo la hasira yangu.” Sikilizeni kelele milimani kama za kundi kubwa la watu! Sikilizeni kelele za falme, na mataifa yanayokusanyika! Mwenyezi-Mungu wa majeshi analikagua jeshi linalokwenda vitani. Wanakuja kutoka nchi za mbali, wanatoka hata miisho ya dunia: Mwenyezi-Mungu na silaha za hasira yake anakuja kuiangamiza dunia. Lieni maana siku ya Mwenyezi-Mungu imekaribia; inakuja kama maafa kutoka kwa Mungu Mwenye Nguvu. Kwa hiyo mikono ya kila mtu italegea, kila mtu atakufa moyo. Watu watafadhaika, watashikwa na hofu na maumivu, watakuwa na uchungu kama mama anayejifungua. Watatazamana kwa mashaka, nyuso zao zitawaiva kwa haya. Siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja, siku kali, ya ghadhabu na hasira kali. Itaifanya nchi kuwa uharibifu, itawaangamiza wenye dhambi wake. Nyota na vilimia vyake angani hazitaangaza; jua linapochomoza litakuwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nitauadhibu ulimwengu kwa uovu wake, waovu kwa sababu ya makosa yao. Nitakikomesha kiburi cha wenye majivuno, na kuporomosha ubaradhuli wa watu katili. Nitawafanya watu kuwa wachache kuliko dhahabu safi; binadamu watakuwa wachache kuliko dhahabu ya Ofiri. Nitazitetemesha mbingu nayo nchi itatikisika katika misingi yake kwa sababu ya ghadhabu yangu Mwenyezi-Mungu siku ile ya hasira yangu kali. “Kama swala anayewindwa, kama kondoo wasio na mchungaji, kila mmoja atajiunga na watu wake kila mtu atakimbilia nchini mwake. Yeyote atakayeonekana atatumbuliwa, atakayekamatwa atauawa kwa upanga. Watoto wao wachanga watapondwapondwa mbele yao, watanyanganywa nyumba zao, na wake zao watanajisiwa. “Ninawachochea Wamedi dhidi yao; watu ambao hawajali fedha wala hawavutiwi na dhahabu. Mishale yao itawaua vijana, hawatakuwa na huruma kwa watoto, wala kuwahurumia watoto wachanga. Babuloni johari ya falme zote na umaarufu wa kiburi cha Wakaldayo utakuwa kama Sodoma na Gomora, wakati Mungu alipoiangamiza. Kamwe hautakaliwa tena na watu, watu hawataishi humo katika vizazi vyote. Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake humo, wala mchungaji atakayechunga wanyama wake humo. Badala yake watakuwamo wanyama wakali wa porini, bundi watajaa katika nyumba zake. Mbuni wataishi humo, na majini yatachezea humo. Mbwamwitu watalia ndani ya ngome zake, mbweha wataonekana ndani ya nyumba zao za anasa. Wakati wa Babuloni umekaribia, wala siku zake hazitaongezwa.”
Isaya 13:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ufunuo juu ya Babeli; maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi. Haya! Juu ya mlima usio na miti inueni bendera, wapazieni sauti zenu, wapungieni mkono, kwamba waingie katika malango ya wakuu. Mimi mwenyewe nimewaamuru watu wangu waliowekwa wakfu kwangu, naam, nimewaita watu wangu walio hodari kwa ajili ya hasira yangu, watu wangu wenye kiburi. Kelele milimani kama kelele za watu wengi sana; kelele za falme za mataifa waliokutana pamoja; BWANA wa majeshi anapanga jeshi kwa vita; watu waliotoka katika nchi iliyo mbali, tokea upande wa mwisho wa mbingu; naam, BWANA na silaha za ghadhabu yake, ili aiangamize nchi yote. Pigeni kelele za hofu; maana siku ya BWANA i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka. Nao watafadhaika; watashikwa na uchungu na maumivu; watakuwa na uchungu kama mwanamke aliye karibu kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto. Tazama, siku ya BWANA inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake. Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze. Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayashusha chini majivuno yao walio wakali; nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri. Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya BWANA wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali. Basi, itakuwa kama vile paa aliyetishwa, na kama kondoo wasio na mtu wa kuwakusanya; kila mtu atageukia watu wake; nao watakimbia, kila mtu aende nchi yake mwenyewe. Kila mtu atakayeonekana atatumbuliwa, na kila mtu atakayepatikana ataanguka kwa upanga. Na watoto wao wachanga watavunjwavunjwa mbele ya macho yao, nyumba zao zitatekwa nyara, na wake zao watanajisiwa. Tazama, nitawaamsha Wamedi juu yao, ambao hawaoni fedha kuwa kitu, wala hawafurahii dhahabu. Na nyuta zao zitawaangusha vijana; wala hawatahurumia mazao ya tumbo; jicho lao halitawahurumia watoto. Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza. Hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi. Mwarabu hatapiga hema yake huko, wala wachungaji hawatalaza makundi yao huko. Lakini huko watalala wanyama wakali wa nyikani; na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini watacheza huko. Na mbwamwitu watalia ndani ya ngome zake; na mbweha ndani ya majumba ya anasa; na wakati wake u karibu kufika, na siku zake hazitaongezeka.
Isaya 13:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ufunuo juu ya Babeli; maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi. Haya! Juu ya mlima usio na miti inueni bendera, wapazieni sauti zenu, wapungieni mkono, kwamba waingie katika malango ya wakuu. Mimi mwenyewe nimewaamuru watu wangu waliowekwa wakfu kwangu, naam, nimewaita watu wangu walio hodari kwa ajili ya hasira yangu, watu wangu wenye kutakabari. Kelele milimani kama kelele za watu wengi sana; kelele za falme za mataifa waliokutana pamoja; BWANA wa majeshi anapanga jeshi kwa vita; watu waliotoka katika nchi iliyo mbali, tokea upande wa mwisho wa mbingu; naam, BWANA na silaha za ghadhabu yake, ili aiangamize nchi yote. Pigeni kelele za hofu; maana siku ya BWANA i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka. Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto. Tazama, siku ya BWANA inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake. Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze. Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali; nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri. Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya BWANA wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali. Basi, itakuwa kama vile paa aliyetishwa, na kama kondoo wasio na mtu wa kuwakusanya; kila mtu atageukia watu wake; nao watakimbia, kila mtu aende nchi yake mwenyewe. Kila mtu atakayeonekana atatumbuliwa, na kila mtu atakayepatikana ataanguka kwa upanga. Na watoto wao wachanga watavunjwa-vunjwa mbele ya macho yao, nyumba zao zitatekwa nyara, na wake zao watatendwa jeuri. Tazama, nitawaamsha Wamedi juu yao, ambao hawaoni fedha kuwa kitu, wala hawafurahii dhahabu. Na nyuta zao zitawaangusha vijana; wala hawatahurumia mazao ya tumbo; jicho lao halitawahurumia watoto. Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza. Hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi. Mwarabu hatapiga hema yake huko, wala wachungaji hawatalaza makundi yao huko. Lakini huko watalala hayawani wakali wa nyikani; na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini watacheza huko. Na mbwa-mwitu watalia ndani ya ngome zake; na mbweha ndani ya majumba ya anasa; na wakati wake u karibu kufika, na siku zake hazitaongezeka.
Isaya 13:1-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno la unabii kuhusu Babeli ambalo Isaya mwana wa Amozi aliliona: Twekeni bendera juu ya mlima usio na kitu, wapazieni sauti, wapungieni mkono waingie katika malango ya wenye heshima. Nimewaamuru watakatifu wangu; nimewaita mashujaa wangu waitimize hasira yangu: wale wanaoshangilia ushindi wangu. Sikilizeni kelele juu ya milima, kama ile ya umati mkubwa wa watu! Sikilizeni, makelele katika falme, kama mataifa yanayokusanyika pamoja! BWANA wa majeshi anakusanya jeshi kwa ajili ya vita. Wanakuja kutoka nchi za mbali sana, kutoka miisho ya mbingu, BWANA na silaha za ghadhabu yake, kuangamiza nchi yote. Ombolezeni, kwa maana siku ya BWANA i karibu, itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi. Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea, moyo wa kila mtu utayeyuka. Hofu itawakamata, uchungu na maumivu makali yatawashika, watagaagaa kama mwanamke aliye na uchungu wa kuzaa. Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake, nyuso zao zikiwaka kama moto. Tazameni, siku ya BWANA inakuja, siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali, kuifanya nchi kuwa ukiwa, na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo. Nyota za mbinguni na makundi ya nyota havitatoa mwanga wake. Jua linalochomoza litatiwa giza na mwezi hautatoa nuru yake. Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake, waovu kwa ajili ya dhambi zao. Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi, na nitakishusha kiburi cha watu wakatili. Nitawafanya wanadamu kuwa adimu kuliko dhahabu safi, watakuwa wachache sana kuliko dhahabu ya Ofiri. Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke, nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake katika ghadhabu ya BWANA wa majeshi, katika siku ya hasira yake iwakayo. Kama paa awindwaye, kama kondoo wasio na mchungaji, kila mmoja atarudi kwa watu wake mwenyewe, kila mmoja atakimbilia nchi yake ya kuzaliwa. Yeyote atakayetekwa atapasuliwa tumbo, wote watakaokamatwa watauawa kwa upanga. Watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande mbele ya macho yao; nyumba zao zitatekwa, na wake zao watanajisiwa. Tazama, nitawachochea Wamedi dhidi yao, ambao hawajali fedha wala hawafurahii dhahabu. Mishale yao itawaangusha vijana, hawatakuwa na huruma kwa watoto wachanga wala hawataangalia watoto kwa huruma. Babeli, johari ya falme, utukufu wa kiburi cha Wababeli, utaangushwa na Mungu kama Sodoma na Gomora. Hautakaliwa na watu kamwe, wala watu hawataishi humo kwa vizazi vyote. Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake huko, hakuna mchungaji atakayepumzisha makundi yake huko. Lakini viumbe wa jangwani watalala huko, mbweha watajaza nyumba zake, bundi wataishi humo nao mbuzi-mwitu watarukaruka humo. Fisi watalia ndani ya ngome zake, mbweha ndani ya majumba yake ya kifahari. Wakati wake umewadia, na siku zake hazitaongezwa.