Isaya 10:1-19
Isaya 10:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole wao wanaotunga sheria zisizo za haki, watu wanaopitisha sheria za kukandamiza. Huwanyima maskini haki zao, na kuwaibia maskini wa watu wangu maslahi yao. Wajane wamekuwa nyara kwao; yatima wamekuwa mawindo yao. Je, mtafanya nini siku ya adhabu, siku dhoruba itakapowajieni kutoka mbali? Mtamkimbilia nani kuomba msaada? Mtakwenda wapi kuweka mali yenu? Litakalowabakia ni kujikunyata kati ya wafungwa na kuangamia pamoja na wanaouawa vitani. Hata hivyo, hasira ya Mwenyezi-Mungu haijatulia, bado ameunyosha mkono wake. Ole wake Ashuru, fimbo ya hasira yangu, yeye ashikaye kiboko cha hasira yangu! Nilimtuma kuliadhibu taifa ovu, nilimwamuru kuwaadhibu watu niliowakasirikia, kuwapora na kuteka nyara, na kuwakanyaga chini kama tope njiani. Lakini Ashuru hakudhamiria hivyo, yeye alikuwa na nia nyingine; alikusudia kuharibu kabisa, kuangamiza mataifa mengi iwezekanavyo. Maana alisema: “Je, si kweli majemadari wangu ni wafalme? Je, si kweli kwamba Kalno nitautenda kama Karkemishi, mji wa Hamathi kama mji wa Arpadi, Samaria kama Damasko? Kama nimefaulu kuunyosha mkono wangu dhidi ya falme zenye sanamu za miungu kubwa kuliko sanamu za Yerusalemu na Samaria; je, nitashindwa kuutenda Yerusalemu na sanamu zake, kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake?” Wakati Mwenyezi-Mungu atakapomaliza kazi zake zote mlimani Siyoni na mjini Yerusalemu, atamwadhibu mfalme wa Ashuru, kwa sababu ya majivuno na kiburi chake. Maana mfalme wa Ashuru alisema: “Kwa nguvu zangu mwenyewe nimetenda hayo, na kwa hekima yangu, maana mimi ni mwerevu! Nimeondoa mipaka kati ya mataifa, nikazipora hazina zao; kama fahali nimewaporomosha walioketia viti vya enzi. Kama mtu anyoshaye mkono kwenye kiota, ndivyo nilivyochukua mali yao; kama mtu aokotavyo mayai yaliyoachwa kiotani, ndivyo nilivyowaokota duniani kote, wala hakuna mtu aliyeweza kupiga bawa, au aliyefungua kinywa kunipigia kelele.” Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Je, shoka litajigamba dhidi ya anayelitumia? Msumeno waweza kujivuna dhidi ya mwenye kukata nao? Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua anayeishika, au mkongojo kumwinua mwenye kuutumia!” Kwa hiyo, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, atawaletea askari wao ugonjwa wa kuwakondesha, na fahari yao itateketezwa kama kwa moto. Mungu aliye mwanga wa Israeli atakuwa kama moto, Mtakatifu wa Israeli atakuwa mwali wa moto ambao kwa siku moja utateketeza kila kitu: Miiba yake na mbigili zake pamoja. Misitu yake ya fahari na mashamba yake mazuri, Mwenyezi-Mungu atayaangamiza yote; itakuwa kama mtu aliyemalizwa na ugonjwa. Miti itakayobaki msituni mwake itakuwa michache sana hata mtoto mdogo ataweza kuihesabu.
Isaya 10:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao sheria za kudhulumu; ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang'anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao! Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi? Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa. Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache. Maana asema, Je! Wakuu wangu si wote wafalme? Je! Kalno si kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi? Samaria si kama Dameski? Kama vile mkono wangu ulivyofikia falme za sanamu, ambazo sanamu zao za kuchongwa zilikuwa bora kuliko sanamu za Yerusalemu na za Samaria; je! Sitautenda Yerusalemu na sanamu zake vile vile kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake? Basi, itakuwa, Bwana atakapokuwa ameitimiza kazi yake yote juu ya mlima Sayuni na juu ya Yerusalemu, nitamwadhibu matunda ya kiburi cha moyo wake mfalme wa Ashuru, na majivuno ya macho yake. Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kiota cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia. Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti. Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, atatuma maradhi ya kukondesha kwa wapiganaji walionenepa; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto. Na mwanga wa Israeli utakuwa ni moto, na Mtakatifu wake atakuwa muali wa moto; nao utateketeza na kula mbigili zake na miiba yake kwa siku moja. Naye atauteketeza utukufu wa msitu wake, na wa shamba lake linalositawi, tangu nafsi hata nyama ya mwili, itakuwa kama vile afapo mtu aliye mgonjwa. Na miti ya msitu wake itakayosalia itakuwa michache, hata mtoto ataweza kuihesabu.
Isaya 10:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu; ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang’anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao! Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi? Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa. Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache. Maana asema, Je! Wakuu wangu si wote wafalme? Je! Kalno si kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi? Samaria si kama Dameski? Kama vile mkono wangu ulivyofikilia falme za sanamu, ambazo sanamu zao za kuchongwa zilikuwa bora kuliko sanamu za Yerusalemu na za Samaria; je! Sitautenda Yerusalemu na sanamu zake vile vile kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake? Basi, itakuwa, Bwana atakapokuwa ameitimiza kazi yake yote juu ya mlima Sayuni na juu ya Yerusalemu, nitayaadhibu matunda ya kiburi cha moyo wake mfalme wa Ashuru, na majivuno ya macho yake. Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia. Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti. Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto. Na mwanga wa Israeli utakuwa ni moto, na Mtakatifu wake atakuwa mwali wa moto; nao utateketeza na kula mbigili zake na miiba yake katika siku moja. Naye atauteketeza utukufu wa msitu wake, na wa shamba lake linalositawi, tangu nafsi hata nyama ya mwili, itakuwa kama vile afapo mtu aliye mgonjwa. Na miti ya msitu wake itakayosalia itakuwa michache, hata mtoto ataweza kuihesabu.
Isaya 10:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ole wao wawekao sheria zisizo za haki, kwa wale watoao amri za kuonea, kuwanyima maskini haki zao na kuzuilia haki za watu wangu waliodhulumiwa, kuwafanya wajane mawindo yao na kuwanyangʼanya yatima. Mtafanya nini siku ya hukumu, wakati maafa yatakapokuja kutoka mbali? Mtamkimbilia nani awape msaada? Mtaacha wapi mali yenu? Hakutasalia kitu chochote, isipokuwa kujikunyata miongoni mwa mateka, au kuanguka miongoni mwa waliouawa. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu. “Ole kwa Ashuru, fimbo ya hasira yangu, ambaye mkononi mwake ana rungu ya ghadhabu yangu! Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu, ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha, kukamata mateka na kunyakua nyara, pia kuwakanyaga chini kama matope ya barabarani. Lakini hili silo analokusudia, hili silo alilo nalo akilini; kusudi lake ni kuangamiza, kuyakomesha mataifa mengi. Maana asema, ‘Je, wafalme wote si majemadari wangu? Je, Kalno hakutendwa kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi, nayo Samaria si kama Dameski? Kama vile mkono wangu ulivyotwaa falme za sanamu, falme ambazo vinyago vyao vilizidi vile vya Yerusalemu na Samaria: je, nisiutendee Yerusalemu na sanamu zake kama nilivyoutendea Samaria na vinyago vyake?’ ” Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.” Kwa kuwa anasema: “ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili, kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu. Niliondoa mipaka ya mataifa, niliteka nyara hazina zao, kama yeye aliye shujaa niliwatiisha wafalme wao. Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota, ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa; kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya nchi zote; wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ” Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu kuliko yule anayelitumia, au msumeno kujisifu dhidi ya yule anayeutumia? Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye, au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia! Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, atatuma ugonjwa wa kudhoofisha kwa mashujaa wake wanene, katika fahari yake moto utawaka kama mwali wa moto. Nuru ya Israeli itakuwa moto, Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto; katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba na michongoma yake. Fahari ya misitu yake na mashamba yenye rutuba utateketeza kabisa, kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo. Nayo miti inayobaki katika misitu yake itakuwa michache sana hata mtoto mdogo angeweza kuihesabu.