Isaya 1:1-20
Isaya 1:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi, kuhusu Yuda na mji wa Yerusalemu, nyakati za utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Sikilizeni enyi mbingu, tega sikio ee dunia. Mimi nimewalea wanangu wakakua, lakini sasa wameniasi! Ngombe humfahamu mwenyewe, punda hujua kibanda cha bwana wake; lakini Waisraeli hawajui, watu wangu, hawaelewi!” Ole wako wewe taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, wazawa wa wenye kutenda maovu, watu waishio kwa udanganyifu! Nyinyi mmemwacha Mwenyezi-Mungu, mmemdharau Mtakatifu wa Israeli, mmefarakana naye na kurudi nyuma. Kwa nini huachi uasi wako? Mbona wataka kuadhibiwa bado? Kichwa chote ni majeraha matupu, na moyo wote unaugua! Toka wayo hadi kichwa hamna penye nafuu, umejaa majeraha na vidonda vitoavyo damu, navyo havikuoshwa, kufungwa wala kutiwa mafuta. Nchi yenu imeharibiwa kabisa; miji yenu imeteketezwa kwa moto. Wageni wananyakua nchi yenu mkiona kwa macho, imeharibiwa kama uharibifu wa Sodoma. Mji Siyoni umeachwa kama kibanda shambani, kama kitalu katika shamba la matango, kama mji uliozingirwa. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asingalituachia wachache, tungalikwisha kuwa kama watu wa Sodoma, tungalikuwa hali ileile ya Gomora. Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu enyi watawala waovu kama wa Sodoma! Sikilizeni mafunzo ya Mungu wetu enyi watu waovu kama wa Gomora! Mwenyezi-Mungu asema hivi; “Wingi wa tambiko zenu ni kitu gani kwangu? Nimezichoka sadaka zenu za kondoo wa kuteketezwa na mafuta ya wanyama wenu wanono. Sipendezwi na damu ya fahali, wala ya wanakondoo, wala ya beberu. Mnapokuja mbele yangu kuniabudu nani aliyewataka mkanyagekanyage nyua zangu? Msiniletee tena matoleo yenu yasiyo na maana; ubani ni chukizo kwangu. Acheni kufanya sikukuu za mwezi mpya, Sabato na mikutano mikubwa ya ibada; sikubali ibada zilizochanganyika na dhambi. Sikukuu zenu za mwezi mpya na nyinginezo moyo wangu wazichukia. Zimekuwa mzigo mzito kwangu, nami nimechoka kuzivumilia. “Mnapoinua mikono yenu kuomba nitauficha uso wangu nisiwaone. Hata mkiomba kwa wingi sitawasikia, maana mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu mbele yangu. Acheni kutenda maovu, jifunzeni kutenda mema. Tendeni haki, ondoeni udhalimu, walindeni yatima, teteeni haki za wajane.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Njoni, basi, tuhojiane. Ingawa mna madoa mekundu ya dhambi, mtatakaswa na kuwa weupe kama theluji; madoa yenu yajapokuwa mekundu kama damu, mtakuwa weupe kama sufu. Mkiwa tayari kunitii, mtakula mazao mema ya nchi. Lakini mkikaidi na kuniasi, mtaangamizwa kwa upanga. Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema.”
Isaya 1:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haya ni maono ya Isaya, mwana wa Amozi aliyoyaona kuhusu Yuda na Yerusalemu, siku za Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana BWANA amenena; Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi. Ng'ombe amjua bwana wake, Na punda ajua kibanda cha bwana wake; Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri. Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha BWANA, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma. Mbona mnataka kupigwa, hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia. Toka wayo wa mguu hadi kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwazongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta. Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni. Na binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa. Kama BWANA wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora. Lisikieni neno la BWANA, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema BWANA. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo dume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi dume. Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu? Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mwandamo na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua. Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama damu, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya.
Isaya 1:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haya ni maono ya Isaya, mwana wa Amozi, aliyoyaona katika habari za Yuda na Yerusalemu, siku za Uzia na Yothamu na Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana BWANA amenena; Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi. Ng’ombe amjua bwana wake, Na punda ajua kibanda cha bwana wake; Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri. Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha BWANA, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma. Mbona mnataka kupigwa hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia. Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwa-zongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta. Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni. Na binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa. Kama BWANA wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora. Lisikieni neno la BWANA, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema BWANA. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng’ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume. Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu? Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua. Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya.
Isaya 1:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia! Kwa maana BWANA amesema: “Nimewalisha watoto na kuwalea, lakini wameniasi mimi. Ngʼombe anamjua bwana wake, naye punda anajua hori la mmiliki wake, lakini Israeli hajui, watu wangu hawaelewi.” Ole wa taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, uzao wa watenda mabaya, watoto waliozoelea upotovu! Wamemwacha BWANA, Wamemkataa kwa dharau yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na kumgeuzia kisogo. Kwa nini mzidi kupigwa? Kwa nini kudumu katika uasi? Kichwa chako chote kimejeruhiwa, moyo wako wote ni mgonjwa. Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako hakuna uzima: ni majeraha matupu na makovu na vidonda vinavyotoa damu, havikusafishwa au kufungwa wala kulainishwa kwa mafuta. Nchi yenu imekuwa ukiwa, miji yenu imeteketezwa kwa moto; mashamba yenu yameachwa tupu na wageni mbele ya macho yenu, yameharibiwa kama yaliyopinduliwa na wageni. Binti Sayuni ameachwa kama kipenu katika shamba la mizabibu, kama kibanda katika shamba la matango, kama mji uliozingirwa. Kama BWANA wa majeshi hakutuachia walionusurika, tungekuwa kama Sodoma, tungefanana na Gomora. Sikieni neno la BWANA, ninyi watawala wa Sodoma; sikilizeni sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora! BWANA anasema, “Wingi wa sadaka zenu, ni kitu gani kwangu? Nina sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi, za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona. Sipendezwi na damu za mafahali wala za wana-kondoo na mbuzi. Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu, ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo, huku kuzikanyaga nyua zangu? Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana! Uvumba wenu ni chukizo kwangu. Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada: siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu. Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa: moyo wangu unazichukia kabisa. Zimekuwa mzigo kwangu, nimechoka kuzivumilia. Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi, nitaficha macho yangu nisiwaone; hata mkiomba maombi mengi sitasikiliza. “Mikono yenu imejaa damu! “Jiosheni na mkajitakase. Yaondoeni matendo yenu maovu mbele zangu; acheni kutenda mabaya. Jifunzeni kutenda mema, tafuteni haki. Wateteeni waliodhulumiwa. Teteeni shauri la yatima, wateteeni wajane. “Njooni basi tujadiliane,” asema BWANA. “Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu, zitakuwa nyeupe kama theluji; ingawa ni nyekundu sana kama damu, zitakuwa nyeupe kama sufu. Mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi, lakini mkikataa na kuasi, mtaangamizwa kwa upanga.” Kwa kuwa kinywa cha BWANA kimenena.