Hosea 9:1-16
Hosea 9:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Msifurahi enyi Waisraeli! Msifanye sherehe kama mataifa mengine; maana, mmekuwa wazinzi kwa kumwacha Mungu wenu. Mmefurahia malipo ya uzinzi, kila mahali pa kupuria nafaka. Lakini ngano na mapipa ya divai haitawalisha, hamtapata divai mpya. Hawatakaa katika nchi ya Mwenyezi-Mungu; naam, watu wa Efraimu watarudi utumwani Misri; watakula vyakula najisi huko Ashuru. Hawatamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya divai, wala hawatamfurahisha kwa tambiko zao. Chakula chao kitakuwa kama cha matanga, wote watakaokila watatiwa unajisi. Kitakuwa chakula cha kuwashibisha tu, hakitafaa kuletwa nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu. Mtafanya nini katika sikukuu ile iliyopangwa, au katika karamu ya Mwenyezi-Mungu? Mtakapoyakimbia maangamizi ya nchi yenu, Misri itawakaribisheni kwake, lakini makaburi yenu yawangoja huko Memfisi. Magugu yatamiliki hazina zenu za fedha, miiba itajaa katika mahema yenu. Siku za adhabu zimewadia, naam, siku za kulipiza kisasi zimefika; Waisraeli lazima wautambue wakati huo! Nyinyi mnasema, “Nabii ni mpumbavu; anayeongozwa na roho ni mwendawazimu.” Mnasema hivyo kwa sababu ya uovu wenu mkubwa, kwa sababu ya chuki yenu kali dhidi yake. Nabii ni mlinzi wa Waefraimu kwa niaba ya Mungu; lakini, kokote aendako anategewa mtego kama ndege. Hata nyumbani mwa Mungu wake anachukiwa. Nyinyi mmezama katika uovu, kama ilivyokuwa kule Gibea. Mungu atayakumbuka makosa yao, na kuwaadhibu kwa dhambi zao. Mwenyezi-Mungu asema: “Nilipowakuta Waisraeli walikuwa kama zabibu jangwani. Nilipowaona wazee wenu walikuwa bora kama tini za kwanza. Lakini mara walipofika huko Baal-peori, walijiweka wakfu kuabudu chukizo Baali, wakawa chukizo kama hicho walichokipenda. Fahari ya Efraimu itatoweka kama ndege; watoto hawatazaliwa tena, hakutakuwa na watoto wa kuzaliwa, wala hakutakuwa na kuchukuliwa mimba! Hata kama wakilea watoto, sitamwacha hai hata mmoja wao. Ole wao, nitakapowaacha peke yao!” Kama nilivyokwisha ona hapo kwanza, Efraimu alikuwa kama mtende mchanga penye konde zuri; lakini sasa Efraimu itamlazimu kuwapeleka watoto wake wauawe. Uwaadhibu watu hawa ee Mwenyezi-Mungu! Lakini utawaadhibu namna gani? Uwafanye wanawake wao kuwa tasa; uwafanye wakose maziwa ya kunyonyesha watoto wao! Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Uovu wao wote ulianzia Gilgali; huko ndiko nilipoanza kuwachukia. Kwa sababu ya uovu wa matendo yao, nitawafukuza nyumbani kwangu. Sitawapenda tena. Viongozi wao wote ni waasi. Watu wa Efraimu wamepigwa, wamekuwa kama mti wenye mzizi mkavu, hawatazaa watoto wowote. Hata kama wakizaa watoto, nitawaua watoto wao wawapendao.”
Hosea 9:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Usifurahi, Israeli, kwa sababu ya furaha, kama hao mataifa; kwa kuwa umezini juu ya Mungu wako, umependa ujira katika kila sakafu ya nafaka. Sakafu na shinikizo hazitawalisha, na divai mpya itampungukia. Hawatakaa katika nchi ya BWANA; lakini Efraimu atarudi Misri, nao watakula chakula najisi katika Ashuru. Hawatammiminia BWANA divai, wala hazitampendeza sadaka zao; mkate wao utakuwa kama chakula cha matanga kwao; wote watakaokila watatiwa unajisi; kwa maana mkate wao utakuwa kwa shauku zao; hautaingia katika nyumba ya BWANA. Mtafanya nini katika siku ya mkutano wa sikukuu teule, na katika siku ya karamu ya BWANA? Kwa maana, tazama, wamekwenda zao ili kukimbia uharibifu, lakini Misri itawakusanya, Nofu itawazika; vitu vyao vya fedha viwapendezavyo, magugu yatavimiliki; miiba itakuwa katika hema zao. Siku za kupatilizwa zimekuja, siku za kulipa zimefika; Israeli atayajua hayo; huyo nabii ni mpumbavu, huyo mtu mwenye roho ana wazimu; kwa sababu ya wingi wa uovu wako, na kwa sababu uadui umekuwa mkubwa. Efraimu alikuwa mlinzi pamoja na Mungu wangu; na huyo nabii, mtego wa mwindaji ndege u katika njia zake zote; katika nyumba ya Mungu wake umo uadui. Wamejiharibu mno, kama katika siku za Gibea; ataukumbuka uovu wao, atazilipiza dhambi zao. Mimi nilimkuta Israeli kama zabibu nyikani; nami niliwaona baba zenu kama matunda ya mtini yaliyoiva kwanza, msimu wake wa kwanza; lakini walikwenda Baal-Peori, wakajiweka wakfu kwa kitu cha aibu, wakawa chukizo kama kitu kile walichokipenda. Naye Efraimu, utukufu wake utarukia mbali kama ndege, uzazi hautakuwako, wala aliye na mimba, wala achukuaye mimba. Wajapolea watoto wao, mimi nitawanyang'anya watoto wao, asisalie hata mtu mmoja; naam, ole wao! Nitakapoondoka na kuwaacha. Efraimu amepandwa mahali pazuri, kama nilivyoona Tiro; lakini Efraimu atamtolea mwuaji watoto wake. Wape, Ee BWANA; utawapa kitu gani? Wape tumbo lenye kuharibu mimba na maziwa makavu. Uovu wao wote u katika Gilgali; maana huko niliwachukia; kwa sababu ya uovu wa matendo yao nitawafukuza watoke katika nyumba yangu; sitawapenda tena; wakuu wao wote ni waasi. Efraimu amepigwa; mzizi wao umekauka; hawatazaa matunda; naam, wajapozaa, nitaliua tunda la tumbo lipendwalo sana.
Hosea 9:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Usifurahi, Israeli, kwa sababu ya furaha, kama hao mataifa; kwa kuwa umezini juu ya Mungu wako, umependa ujira katika kila sakafu ya nafaka. Sakafu na shinikizo hazitawalisha, na divai mpya itampungukia. Hawatakaa katika nchi ya BWANA; lakini Efraimu atarudi Misri, nao watakula chakula kinajisi katika Ashuru. Hawatammiminia BWANA divai, wala hazitampendeza sadaka zao; mkate wao utakuwa kama chakula cha matanga kwao; wote watakaokila watatiwa unajisi; kwa maana mkate wao utakuwa kwa shauku zao; hautaingia katika nyumba ya BWANA. Mtafanya nini katika siku ya mkutano wa idi, na katika siku ya karamu ya BWANA? Kwa maana, tazama, wamekwenda zao ili kukimbia uharibifu, lakini Misri itawakusanya, Nofu itawazika; vitu vyao vya fedha viwapendezavyo, magugu yatavimiliki; miiba itakuwa katika hema zao. Siku za kupatilizwa zimekuja, siku za kulipa zimefika; Israeli atayajua hayo; huyo nabii ni mpumbavu, huyo mtu mwenye roho ana wazimu; kwa sababu ya wingi wa uovu wako, na kwa sababu uadui umekuwa mkubwa. Efraimu alikuwa mlinzi pamoja na Mungu wangu; na huyo nabii, mtego wa mwinda ndege u katika njia zake zote; katika nyumba ya Mungu wake umo uadui. Wamejiharibu mno, kama katika siku za Gibea; ataukumbuka uovu wao, atazilipiza dhambi zao. Mimi nalimkuta Israeli kama zabibu nyikani; nami naliwaona baba zenu kama matunda ya mtini yaliyoiva kwanza, wakati wake wa kwanza; lakini walikwenda Baal-Peori, wakajiweka wakfu kwa kitu cha aibu, wakawa chukizo kama kitu kile walichokipenda. Naye Efraimu, utukufu wake utarukia mbali kama ndege, uzazi hautakuwako, wala aliye na mimba, wala achukuaye mimba. Wajapolea watoto wao, mimi nitawanyang’anya watoto wao, asisalie hata mtu mmoja; naam, ole wao! Nitakapoondoka na kuwaacha. Efraimu amepandwa mahali pazuri, kama nilivyoona Tiro; lakini Efraimu atamtolea mwuaji watoto wake. Wape, Ee BWANA; utawapa kitu gani? Wape tumbo lenye kuharibu mimba na maziwa makavu. Uovu wao wote u katika Gilgali; maana huko naliwachukia; kwa sababu ya uovu wa matendo yao nitawafukuza watoke katika nyumba yangu; sitawapenda tena; wakuu wao wote ni waasi. Efraimu amepigwa; mzizi wao umekauka; hawatazaa matunda; naam, wajapozaa, nitaliua tunda la tumbo lipendwalo sana.
Hosea 9:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Usifurahie, ee Israeli; usishangilie kama mataifa mengine. Kwa kuwa hukuwa mwaminifu kwa Mungu wako; umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu ya kupuria nafaka. Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai havitalisha watu, divai mpya itawapungukia. Hawataishi katika nchi ya BWANA, Efraimu atarudi Misri na atakula chakula kilicho najisi huko Ashuru. Hawatammiminia BWANA sadaka ya divai wala dhabihu zao hazitampendeza. Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao kama mkate wa waombolezaji; nao wote wazilao watakuwa najisi. Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe; kisije katika Hekalu la BWANA. Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamriwa, katika siku za sikukuu za BWANA? Hata ikiwa wataokoka maangamizi, Misri atawakusanya, nayo Memfisi itawazika. Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma, nayo miiba itafunika mahema yao. Siku za adhabu zinakuja, siku za malipo zimewadia. Israeli na afahamu hili. Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana na uadui wenu ni mkubwa sana, nabii anadhaniwa ni mpumbavu, mtu aliyeongozwa na Mungu anaonekana mwendawazimu. Nabii, pamoja na Mungu wangu, ndiye mlinzi juu ya Efraimu, hata hivyo mitego inamngojea katika mapito yake yote, na uadui katika nyumba ya Mungu wake. Wamezama sana katika rushwa, kama katika siku za Gibea. Mungu atakumbuka uovu wao na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao. “Nilipompata Israeli, ilikuwa kama kupata zabibu jangwani; nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona matunda ya kwanza katika mtini. Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu kwa ile sanamu ya aibu, nao wakawa najisi kama kitu kile walichokipenda. Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege: hakuna kuzaa, hakuna kubeba mimba, hakuna kuchukua mimba. Hata wakilea watoto, nitamuua kila mmoja. Ole wao nitakapowapiga kisogo! Nimemwona Efraimu, kama Tiro, aliyeoteshwa mahali pazuri. Lakini Efraimu wataleta watoto wao kwa mchinjaji.” Wape, Ee BWANA, je, utawapa nini? Wape tumbo zinazoharibu mimba na matiti yaliyokauka. “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali, niliwachukia huko. Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi, nitawafukuza katika nyumba yangu. Sitawapenda tena, viongozi wao wote ni waasi. Efraimu ameharibiwa, mzizi wao umenyauka, hawazai tunda. Hata kama watazaa watoto, nitawachinja wazao wao waliotunzwa vizuri.”