Hosea 8:1-14
Hosea 8:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
“Pigeni baragumu! Adui anakuja kama tai kuivamia nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa wamelivunja agano langu na kuiasi sheria yangu. Waisraeli hunililia wakisema: ‘Mungu wetu, sisi tunakujua.’ Lakini Israeli amepuuza mambo mema, kwa hiyo, sasa adui watamfuatia. “Walijiwekea wafalme bila kibali changu, walijiteulia viongozi ambao sikuwatambua. Wamejitengenezea miungu ya fedha na dhahabu, jambo ambalo litawaangamiza. Watu wa Samaria, naichukia sanamu yenu ya ndama. Hasira yangu inawaka dhidi yenu. Mtaendelea mpaka lini kuwa na hatia? Nanyi Waisraeli ni hivyohivyo! Na sanamu yenu hiyo fundi ndiye aliyeitengeneza. Yenyewe si Mungu hata kidogo. Naam! Sanamu ya ndama ya Samaria itavunjwavunjwa! “Wanapanda upepo, watavuna kimbunga! Mimea yao ya nafaka iliyo mashambani haitatoa nafaka yoyote. Na hata kama ikizaa, mazao yake yataliwa na wageni. Waisraeli wamemezwa; sasa wamo kati ya mataifa mengine, kama chombo kisicho na faida yoyote; kwa kuwa wamekwenda kuomba msaada Ashuru. Efraimu ni punda anayetangatanga peke yake; Efraimu amekodisha wapenzi wake. Wametafuta wapenzi kati ya watu wa mataifa, lakini mimi nitawakusanya mara. Na hapo watasikia uzito wa mzigo, ambao mfalme wa wakuu aliwatwika. “Watu wa Efraimu wamejijengea madhabahu nyingi, na madhabahu hizo zimewazidishia dhambi. Hata kama ningewaandikia sheria zangu mara nyingi, wao wangeziona kuwa kitu cha kigeni tu. Wanapenda kutoa tambiko, na kula nyama yake; lakini mimi Mwenyezi-Mungu sipendezwi hata kidogo. Mimi nayakumbuka makosa yao; nitawaadhibu kwa dhambi zao; nitawarudisha utumwani Misri. Waisraeli wamemsahau Muumba wao, wakajijengea majumba ya fahari; watu wa Yuda wamejiongezea miji ya ngome, lakini mimi nitaipelekea moto miji hiyo, na kuziteketeza ngome zao.”
Hosea 8:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tia baragumu kinywani mwako. Kama tai, anakuja juu ya nyumba ya BWANA; kwa sababu wamelivunja agano langu, wameiasi sheria yangu. Watanililia, Mungu wangu, sisi Israeli tunakujua. Israeli ameyatupa yaliyo mema; adui watamfuatia. Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nilikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali. Ndama wako amemtupa, Ee Samaria; ghadhabu yangu imewaka juu yao; Wataendelea kuwa na hatia hadi lini? Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjika vipande vipande. Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza. Israeli amemezwa; sasa wamo miongoni mwa mataifa kama chombo kisichopendeza. Kwa maana wamekwea kwenda Ashuru, mfano wa punda wa porini aliye peke yake; Efraimu ameajiri wapenzi. Naam, ijapokuwa waajiri kati ya mataifa, sasa nitawakusanya; nao wanaanza kupunguka kwa sababu ya mzigo wa mfalme wa wakuu. Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake. Nijapomwandikia sheria yangu katika amri makumi elfu, zimehesabiwa kuwa ni kitu kigeni. Kwa habari za dhabihu za matoleo yangu, hutoa dhabihu ya nyama na kuila; lakini BWANA hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao; watarudi kwenda Misri. Maana Israeli amemsahau Muumba wake, naye amejenga nyumba za enzi; na Yuda ameongeza miji yenye maboma; lakini nitatuma moto juu ya miji yake, nao utaziteketeza ngome zake.
Hosea 8:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tia baragumu kinywani mwako. Kama tai, anakuja juu ya nyumba ya BWANA; kwa sababu wamelihalifu agano langu, wameiasi sheria yangu. Watanililia, Mungu wangu, sisi Israeli tunakujua. Israeli ameyatupa yaliyo mema; adui watamfuatia. Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyizia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali. Amemtupa ndama yako, Ee Samaria; hasira yangu imewaka juu yao; siku ngapi zitapita kabla ya hao kupata hali isiyo na hatia? Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjika vipande vipande. Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza. Israeli amemezwa; sasa wamo miongoni mwa mataifa kama chombo kisichopendeza. Kwa maana wamekwea kwenda Ashuru, mfano wa punda wa mwituni aliye peke yake; Efraimu ameajiri wapenzi. Naam, ijapokuwa waajiri kati ya mataifa, sasa nitawakusanya; nao wanaanza kupunguka kwa sababu ya mzigo wa mfalme wa wakuu. Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake. Nijapomwandikia sheria yangu katika amri elfu kumi, zimehesabiwa kuwa ni kitu kigeni. Kwa habari za dhabihu za matoleo yangu, hutoa dhabihu ya nyama na kuila; lakini BWANA hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao; watarudi kwenda Misri. Maana Israeli amemsahau Muumba wake, naye amejenga nyumba za enzi; na Yuda ameongeza miji yenye maboma; lakini nitapeleka moto juu ya miji yake, nao utaziteketeza ngome zake.
Hosea 8:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Wekeni tarumbeta midomoni mwenu! Tai yuko juu ya nyumba ya BWANA kwa sababu watu wamevunja agano langu, wameasi dhidi ya sheria yangu. Israeli ananililia, ‘Ee Mungu wetu, tunakukubali!’ Lakini Israeli amekataa lile lililo jema, adui atamfuatia. Wanaweka wafalme bila idhini yangu, wamechagua wakuu bila kibali changu. Kwa fedha zao na dhahabu wamejitengenezea sanamu kwa ajili ya maangamizi yao wenyewe. Ee Samaria, tupilieni mbali sanamu yenu ya ndama! Hasira yangu inawaka dhidi yao. Watakuwa najisi hadi lini? Zimetoka katika Israeli! Ndama huyu: ametengenezwa na fundi, si Mungu. Atavunjwa vipande vipande, yule ndama wa Samaria. “Wanapanda upepo na kuvuna kisulisuli. Bua halina suke, halitatoa unga. Kama lingetoa nafaka, wageni wangeila yote. Israeli amemezwa; sasa yupo miongoni mwa mataifa kama kitu kisicho na thamani. Kwa kuwa wamepanda kwenda Ashuru kama punda-mwitu anayetangatanga peke yake. Efraimu amejiuza mwenyewe kwa wapenzi. Ingawa wamejiuza wenyewe miongoni mwa mataifa, sasa nitawakusanya pamoja. Wataanza kudhoofika chini ya uonevu wa mfalme mwenye nguvu. “Ingawa Efraimu alijenga madhabahu nyingi kwa ajili ya sadaka za dhambi, hizi zimekuwa madhabahu za kufanyia dhambi. Niliwaandikia mambo mengi yaliyohusu sheria yangu, lakini waliziangalia kama kitu kigeni. Wanatoa dhabihu nilizopewa mimi nao wanakula hiyo nyama, lakini BWANA hapendezwi nao. Sasa ataukumbuka uovu wao na kuadhibu dhambi zao: Watarudi Misri. Israeli amemsahau Muumba wake na kujenga majumba ya kifalme, Yuda amejengea miji mingi ngome. Lakini nitatuma moto kwenye miji yao utakaoteketeza ngome zao.”