Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 7:3-16

Hosea 7:3-16 Biblia Habari Njema (BHN)

“Wanamfurahisha mfalme kwa maovu yao wanawafurahisha wakuu kwa uhaini wao. Wote ni wazinzi; wao ni kama tanuri iliyowashwa moto ambao mwokaji hauchochei tangu akande unga mpaka mkate utakapoumuka. Kwenye sikukuu ya mfalme, waliwalewesha sana maofisa wake; naye mfalme akashirikiana na wahuni. Kama tanuri iwakavyo, mioyo yao huwaka kwa hila; usiku kucha hasira yao hufuka moshi, ifikapo asubuhi, hulipuka kama miali ya moto. Wote wamewaka hasira kama tanuri, na wanawaangamiza watawala wao. Wafalme wao wote wameanguka, wala hakuna anayeniomba msaada. “Efraimu amechanganyika na watu wa mataifa. Anaonekana kama mkate ambao haukugeuzwa. Wageni wamezinyonya nguvu zake, wala yeye mwenyewe hajui; mvi zimetapakaa kichwani mwake, lakini mwenyewe hana habari. Kiburi cha Waisraeli chashuhudia dhidi yao, hawanirudii mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao; wala hawanitafuti kwa matukio hayo yote. Efraimu ni kama njiwa, mjinga asiye na akili; mara yuko Misri, mara Ashuru kuomba. Watakapokwenda nitatandaza wavu wangu niwanase, nitawaangusha chini kama ndege wa angani; nitamwaadhibu kadiri ya ripoti ya maovu yao. Ole wao kwa kuwa wameniacha! Maangamizi na yawapate, maana wameniasi. Nilitaka kuwakomboa, lakini wanazua uongo dhidi yangu. “Wananililia, lakini si kwa moyo. Wanagaagaa na kujikatakata vitandani mwao, kusudi nisikilize dua zao za nafaka na divai; lakini wanabaki waasi dhidi yangu. Mimi ndimi niliyeiimarisha mikono yao, lakini wanafikiria maovu dhidi yangu. Wanaigeukia miungu batili, wako kama uta uliolegea. Viongozi wao watakufa kwa upanga, kwa sababu ya maneno yao ya kiburi. Kwa hiyo, watadharauliwa nchini Misri.

Shirikisha
Soma Hosea 7

Hosea 7:3-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao. Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuri iliyotiwa moto na mwokaji; asiyehitajika kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hadi utakapokwisha kutiwa chachu. Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu waliugua kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha. Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuri, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali. Wote wamepata moto kama tanuri, nao hula watawala wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi. Efraimu ajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate usiogeuzwa. Wageni wamekula nguvu zake, naye hana habari; naam, nywele za mvi zimeonekana huku na huko juu yake, naye hana habari. Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; ila hata hivyo hawakumrudia BWANA, Mungu wao, wala hawakumtafuta kwa ajili ya hayo yote. Naye Efraimu amekuwa kama njiwa mpumbavu, asiye na fahamu; humwita Misri, huenda Ashuru. Watakapokwenda nitatandika wavu wangu juu yao; nitawashusha kama ndege wa angani; nitawarudi, kama vile mkutano wao ulivyosikia. Ole wao! Kwa kuwa wamenikimbia; uharibifu na uwapate! Kwa kuwa wameniasi; ingawa ninataka kuwakomboa, hata hivyo wamenena uongo juu yangu. Wala hawakunililia kwa moyo, lakini wanalalamika vitandani mwao; hujikutanisha ili kupata nafaka na divai; huniasi mimi. Ingawa nimewafundisha na kuwatia nguvu mikono yao, hata hivyo hukusudia udhalimu juu yangu. Wao hurudi, lakini si kwake Aliye Juu; wamekuwa kama upinde usiotumainika; wakuu wao wataanguka kwa upanga, kwa sababu ya ujeuri wa ndimi zao; na kwa sababu hiyo watachekwa katika nchi ya Misri.

Shirikisha
Soma Hosea 7

Hosea 7:3-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao. Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuu iliyotiwa moto na mwokaji; huacha kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hata umekwisha kutiwa chachu. Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu walijitapisha kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha. Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuu, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali. Wote wamepata moto kama tanuu, nao hula makadhi wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi. Efraimu ajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate usiogeuzwa. Wageni wamekula nguvu zake, naye hana habari; naam, nywele za mvi zimeonekana huko na huko juu yake, naye hana habari. Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; ila hata hivyo hawakumrudia BWANA, Mungu wao, wala hawakumtafuta kwa ajili ya hayo yote. Naye Efraimu amekuwa kama njiwa mpumbavu, asiye na fahamu; humwita Misri, huenda Ashuru. Watakapokwenda nitatandika wavu wangu juu yao; nitawashusha kama ndege wa angani; nitawarudi, kama vile mkutano wao ulivyosikia. Ole wao! Kwa kuwa wamenikimbia; uharibifu na uwapate! Kwa kuwa wameniasi; ingawa ninataka kuwakomboa, hata hivyo wamenena uongo juu yangu. Wala hawakunililia kwa moyo, lakini wanalalamika vitandani mwao; hujikutanisha ili kupata nafaka na divai; huniasi mimi. Ingawa nimewafundisha na kuwatia nguvu mikono yao, hata hivyo hukusudia udhalimu juu yangu. Wao hurudi, lakini si kwake Aliye juu; wamekuwa kama upinde usiotumainika; wakuu wao wataanguka kwa upanga, kwa sababu ya jeuri ya ndimi zao; jambo hili litakuwa kwao sababu ya kuchekwa katika nchi ya Misri.

Shirikisha
Soma Hosea 7

Hosea 7:3-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

“Wanamfurahisha sana mfalme kwa maovu yao, wakuu wao kwa uongo wao. Wote ni wazinzi, wanawaka kama tanuru ambalo moto wake mwokaji hana haja ya kuuchochea kuanzia kukanda unga hadi umekwisha kuumuka. Katika sikukuu ya mfalme wetu wakuu wanawaka kwa mvinyo, naye anawaunga mkono wenye mizaha. Mioyo yao ni kama tanuru, wanamwendea kwa hila. Hasira yao inafoka moshi usiku kucha, wakati wa asubuhi inalipuka kama miali ya moto. Wote ni moto kama tanuru; wanawaangamiza watawala wao. Wafalme wake wote wanaanguka, wala hakuna yeyote kati yao aniitaye mimi. “Efraimu anajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate ambao haukuiva. Wageni wananyonya nguvu zake, lakini hafahamu hilo. Nywele zake zina mvi hapa na pale, lakini hana habari. Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yake, lakini pamoja na haya yote harudi kwa BWANA Mungu wake wala kumtafuta. “Efraimu ni kama hua, hudanganywa kwa urahisi na hana akili: mara anaita Misri, mara anageukia Ashuru. Watakapoenda, nitatupa wavu wangu juu yao; nitawavuta chini waanguke kama ndege wa angani. Nitakaposikia wakikusanyika pamoja, nitawanasa. Ole wao, kwa sababu wamepotoka kutoka kwangu! Maangamizi ni yao kwa sababu wameniasi! Ninatamani kuwakomboa, lakini wanasema uongo dhidi yangu. Hawanililii mimi kutoka mioyoni mwao, bali wanaomboleza vitandani mwao. Hukusanyika pamoja kwa ajili ya nafaka na divai mpya, lakini hugeukia mbali nami. Niliwafundisha na kuwatia nguvu, lakini wanapanga mabaya dhidi yangu. Hawamgeukii Yeye Aliye Juu Sana, wako kama upinde wenye kasoro. Viongozi wao wataanguka kwa upanga kwa sababu ya maneno yao ya jeuri. Kwa ajili ya hili watadhihakiwa katika nchi ya Misri.

Shirikisha
Soma Hosea 7