Hosea 7:1-7
Hosea 7:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Kila nikitaka kuwarekebisha watu wangu, ninapotaka kuwaponya Waisraeli, uovu wa watu wa Efraimu hufunuliwa, matendo mabaya ya Samaria hujitokeza. Wao huongozwa na udanganyifu, kwenye nyumba wezi huvunja nje barabarani wanyang'anyi huvamia. Hawafikiri hata kidogo kwamba mimi nayakumbuka maovu yao yote. Sasa maovu yao yamewabana. Yote waliyotenda yako mbele yangu. “Wanamfurahisha mfalme kwa maovu yao wanawafurahisha wakuu kwa uhaini wao. Wote ni wazinzi; wao ni kama tanuri iliyowashwa moto ambao mwokaji hauchochei tangu akande unga mpaka mkate utakapoumuka. Kwenye sikukuu ya mfalme, waliwalewesha sana maofisa wake; naye mfalme akashirikiana na wahuni. Kama tanuri iwakavyo, mioyo yao huwaka kwa hila; usiku kucha hasira yao hufuka moshi, ifikapo asubuhi, hulipuka kama miali ya moto. Wote wamewaka hasira kama tanuri, na wanawaangamiza watawala wao. Wafalme wao wote wameanguka, wala hakuna anayeniomba msaada.
Hosea 7:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakati nitakapo kumponya Israeli, ndipo yafunuliwapo maovu ya Efraimu, na ubaya wa Samaria; maana wanatenda uongo, na mwizi huvunja nyumba za watu, na kundi la magaidi hushambulia nje. Wala hawafikiri mioyoni mwao ya kwamba naukumbuka uovu wao wote; sasa matendo yao wenyewe yamewazunguka pande zote; yako mbele za uso wangu. Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao. Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuri iliyotiwa moto na mwokaji; asiyehitajika kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hadi utakapokwisha kutiwa chachu. Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu waliugua kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha. Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuri, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali. Wote wamepata moto kama tanuri, nao hula watawala wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi.
Hosea 7:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakati nitakapo kumponya Israeli, ndipo yafunuliwapo maovu ya Efraimu, na ubaya wa Samaria; maana wanatenda uongo, na mwivi huvunja nyumba za watu, na kundi la wanyang’anyi hushambulia nje. Wala hawafikiri mioyoni mwao ya kwamba naukumbuka uovu wao wote; sasa matendo yao wenyewe yamewazunguka pande zote; yako mbele za uso wangu. Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao. Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuu iliyotiwa moto na mwokaji; huacha kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hata umekwisha kutiwa chachu. Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu walijitapisha kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha. Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuu, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali. Wote wamepata moto kama tanuu, nao hula makadhi wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi.
Hosea 7:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
kila mara nilipotaka kumponya Israeli, dhambi za Efraimu zinafichuliwa na maovu ya Samaria yanafunuliwa. Wanafanya udanganyifu, wezi huvunja nyumba, maharamia hunyangʼanya barabarani, lakini hawafahamu kwamba ninakumbuka matendo yao yote mabaya. Dhambi zao zimewameza, ziko mbele zangu siku zote. “Wanamfurahisha sana mfalme kwa maovu yao, wakuu wao kwa uongo wao. Wote ni wazinzi, wanawaka kama tanuru ambalo moto wake mwokaji hana haja ya kuuchochea kuanzia kukanda unga hadi umekwisha kuumuka. Katika sikukuu ya mfalme wetu wakuu wanawaka kwa mvinyo, naye anawaunga mkono wenye mizaha. Mioyo yao ni kama tanuru, wanamwendea kwa hila. Hasira yao inafoka moshi usiku kucha, wakati wa asubuhi inalipuka kama miali ya moto. Wote ni moto kama tanuru; wanawaangamiza watawala wao. Wafalme wake wote wanaanguka, wala hakuna yeyote kati yao aniitaye mimi.