Hosea 4:1-19
Hosea 4:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Msikilizeni Mwenyezi-Mungu, enyi Waisraeli. Mwenyezi-Mungu anawashutumu wakazi wa nchi hii. “Hamna tena uaminifu wala wema nchini; hamna anayemjua Mungu katika nchi hii. Kuapa, uongo, mauaji, wizi na uzinzi huzuka humo. Umwagaji damu hufuatana mfululizo. Kwa hiyo, nchi yote ni kame, wakazi wake wote wanaangamia pamoja na wanyama wa porini na ndege; hata samaki wa baharini wanaangamizwa. “Lakini watu wasilaumiwe, wasishutumiwe; maana mimi nakushutumu wewe kuhani. Wewe utajikwaa mchana, naye nabii atajikwaa pamoja nawe usiku. Nitamwangamiza mama yako Israeli. Watu wangu wameangamia kwa kutonijua, maana wewe kuhani umekataa mafundisho. Nimekukataa kuwa kuhani wangu. Kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, nami pia nitawasahau watoto wako. “Kadiri makuhani walivyoongezeka, ndivyo wote walivyozidi kuniasi. Basi, nitaigeuza fahari yao kuwa aibu. Wanajishibisha kwa sadaka za watu wangu wenye dhambi. Wana hamu sana ya kuwaona wametenda dhambi. Lakini yatakayowapata watu yatawapata makuhani; nitawaadhibu kwa sababu ya mwenendo wao, nitawalipiza matendo yao wenyewe. Watakula, lakini hawatashiba; watazini, lakini hawatapata watoto, kwa sababu wameniacha mimi Mwenyezi-Mungu, na kufuata miungu mingine. “Divai mpya na ya zamani huondoa maarifa. Watu wangu huomba shauri kutoka kwa mti; kijiti chao cha ramli ndicho kinachowapa kauli. Nia ya kufanya uzinzi imewapotosha; wamefanya uzinzi kwa kufuata miungu mingine, wakaniacha mimi Mungu wao. Wanatambikia kwenye vilele vya milima; naam, wanatoa tambiko vilimani, chini ya mialoni, migude na mikwaju, maana kivuli chao ni kizuri. “Kwa hiyo binti zenu hufanya uzinzi, na bibiarusi wenu hufanya uasherati. Lakini sitawaadhibu binti zenu wanapofanya uzinzi, wala bibi arusi wenu wanapofanya uasherati, maana, wanaume wenyewe ndio wanaofuatana na wazinzi, na kutambikia pamoja nao katika ibada za uzinzi. Watu hawa watovu wa akili hakika wataangamia! “Ama kweli nyinyi Waisraeli ni wazinzi! Lakini, msiwafanye watu wa Yuda wawe na hatia! Msiende mahali patakatifu huko Gilgali, wala msiende kule Beth-aveni. Wala msiape mkisema, ‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo!’” Waisraeli ni wakaidi kama punda. Kwa nini basi Mungu ashughulike kuwachunga, kama kondoo kwenye malisho mapana? “Watu wa Efraimu wamejifunga na sanamu. Haya! Waache waendelee tu! Kama vile genge la walevi, wanajitosa wenyewe katika uzinzi; wanapendelea aibu kuliko heshima yao. Basi, kimbunga kitawapeperusha, na watayaonea aibu matambiko yao kwa miungu ya uongo.
Hosea 4:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lisikieni neno la BWANA, enyi wana wa Israeli; kwa maana BWANA ana shutuma nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi. Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na kumwaga damu mfululizo. Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na kila mtu akaaye ndani yake atadhoofika, pamoja na wanyama wa porini na ndege wa angani; naam, samaki wa baharini pia wataangamizwa. Lakini asishindane mtu, wala mtu asikemee; maana watu wako ni kama wao washindanao na kuhani. Na wewe utajikwaa wakati wa mchana, na nabii naye atajikwaa pamoja nawe wakati wa usiku; nami nitamwangamiza mama yako. Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako. Kadiri walivyozidishwa, kwa kadiri iyo hiyo walinitenda dhambi; nami nitageuza utukufu wao kuwa aibu. Hujilisha dhambi ya watu wangu, hujifurahisha moyo kwa uovu wao. Hata itakuwa, kama walivyo watu, ndivyo atakavyokuwa kuhani; nami nitawaadhibu kwa ajili ya njia zao, na kuwalipa kwa matendo yao. Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa, lakini hawataongezeka; kwa sababu wameacha kumwangalia BWANA. Uzinzi na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu. Watu wangu hutaka shauri kwa kipande cha mti, na fimbo yao huwatolea uaguzi; maana roho ya uzinzi imewapotosha, wakawacha Mungu wao. Hutoa dhabihu juu ya vilele vya milima, na kufukiza uvumba juu ya vilima, chini ya mialoni na milibua na miela, kwa kuwa uvuli wake ni mwema; kwa sababu hiyo binti zenu huzini, na bibi arusi zenu hufanya uasherati. Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia. Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo BWANA. Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! BWANA atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye malisho mazuri. Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache. Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu. Upepo umemfunika kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao.
Hosea 4:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lisikieni neno la BWANA, enyi wana wa Israeli; kwa maana BWANA ana mateto nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi. Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na damu hugusana na damu. Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na kila mtu akaaye ndani yake atadhoofika, pamoja na wanyama wa kondeni na ndege wa angani; naam, samaki wa baharini pia wataondolewa. Walakini asishindane mtu, wala mtu asikemee; maana watu wako ni kama wao washindanao na kuhani. Na wewe utajikwaa wakati wa mchana, na nabii naye atajikwaa pamoja nawe wakati wa usiku; nami nitamwangamiza mama yako. Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako. Kadiri walivyozidishwa, kwa kadiri iyo hiyo walinitenda dhambi; nami nitageuza utukufu wao kuwa aibu. Hujilisha dhambi ya watu wangu, hujifurahisha moyo kwa uovu wao. Hata itakuwa, kama walivyo watu, ndivyo atakavyokuwa kuhani; nami nitawaadhibu kwa ajili ya njia zao, na kuwalipa kwa matendo yao. Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa, lakini hawataongezeka; kwa sababu wameacha kumwangalia BWANA. Uzinzi na divai na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu. Watu wangu hutaka shauri kwa gongo lao, na fimbo yao huwahubiri mambo; maana roho ya uzinzi imewakosesha, nao wamekwenda kuzini mbali na Mungu wao. Hutoa dhabihu juu ya vilele vya milima, na kufukiza uvumba juu ya vilima, chini ya mialoni na milibua na miela, kwa kuwa uvuli wake ni mwema; kwa sababu hiyo binti zenu huzini, na bibi arusi zenu hufanya uasherati. Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wao wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia. Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-Aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo BWANA. Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! BWANA atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye nafasi! Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache. Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu. Upepo umemfunikiza kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao.
Hosea 4:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sikieni neno la BWANA, enyi Waisraeli, kwa sababu BWANA analo shtaka dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi: “Hakuna uaminifu, hakuna upendo, hakuna kumjua Mungu katika nchi. Kuna kulaani tu, uongo na uuaji, wizi na uzinzi, bila kuwa na mipaka, nao umwagaji damu mmoja baada ya mwingine. Kwa sababu hii nchi huomboleza, wote wanaoishi ndani yake wanadhoofika; wanyama wa kondeni, ndege wa angani na samaki wa baharini wanakufa. “Lakini mtu yeyote na asilete shtaka, mtu yeyote na asimlaumu mwenzake, kwa maana watu wako ni kama wale waletao mashtaka dhidi ya kuhani. Unajikwaa usiku na mchana, nao manabii hujikwaa pamoja nawe. Kwa hiyo nitamwangamiza mama yako: watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. “Kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeacha kuijali sheria ya Mungu wako mimi nami sitawajali watoto wako. Kadiri makuhani walivyoongezeka, ndivyo walivyozidi kutenda dhambi dhidi yangu, walibadilisha utukufu wao kwa kitu cha aibu. Wanajilisha dhambi za watu wangu na kupendezwa na uovu wao. Hata itakuwa: Kama walivyo watu, ndivyo walivyo makuhani. Nitawaadhibu wote wawili kwa ajili ya njia zao na kuwalipa kwa matendo yao. “Watakula lakini hawatashiba; watajiingiza katika ukahaba lakini hawataongezeka, kwa sababu wamemwacha BWANA na kujiingiza wenyewe katika ukahaba; kunywa divai ya zamani na divai mpya huondoa ufahamu wa watu wangu. Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti nao hujibiwa na fimbo ya mti. Roho ya ukahaba imewapotosha, hawana uaminifu kwa Mungu wao. Wanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima, chini ya mialoni, milibua na miela, ambako kuna vivuli vizuri. Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba na wake za wana wenu uzinzi. “Sitawaadhibu binti zenu wakati wanapogeukia ukahaba, wala wake za wana wenu wanapofanya uzinzi, kwa sababu wanaume wenyewe huandamana na malaya na kutambikia pamoja na makahaba wa mahali pa ibada za sanamu: watu wasiokuwa na ufahamu wataangamia! “Ingawa umefanya uzinzi, ee Israeli, Yuda naye asije akawa na hatia. “Usiende Gilgali, usipande kwenda Beth-Aveni. Wala usiape, ‘Hakika kama BWANA aishivyo!’ Waisraeli ni wakaidi, kama ndama jike mkaidi. Ni jinsi gani basi BWANA anaweza kuwachunga kama wana-kondoo katika shamba la majani? Efraimu amejiunga na sanamu, achana naye! Hata wakati wamemaliza vileo vyao wanaendelea na ukahaba wao, watawala wao hupenda sana njia za aibu. Kisulisuli kitawafagilia mbali na dhabihu zao zitawaletea aibu.