Hosea 2:2-23
Hosea 2:2-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mlaumuni mama yenu mlaumuni, maana sasa yeye si mke wangu wala mimi si mume wake. Mlaumuni aondokane na uasherati wake, ajiepushe na uzinzi wake. La sivyo, nitamvua nguo abaki uchi, nitamfanya awe kama alivyozaliwa. Nitamfanya awe kama jangwa, nitamweka akauke kama nchi kavu. Nitamuua kwa kiu. Na watoto wake sitawahurumia, maana ni watoto wa uzinzi. Mama yao amefanya uzinzi, aliyewachukua mimba amefanya mambo ya aibu. Alisema; “Nitaambatana na wapenzi wangu, ambao hunipa chakula na maji, sufu na kitani, mafuta na divai.” Basi, nitaiziba njia yake kwa miiba, nitamzungushia ukuta, asipate njia ya kutokea nje. Atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; naam, atawatafuta, lakini hatawaona. Hapo ndipo atakaposema, “Nitarudi kwa mume wangu wa kwanza; maana hapo kwanza nilikuwa nafuu kuliko sasa.” Hakujua kwamba ni mimi niliyempa nafaka, divai na mafuta, niliyemjalia fedha na dhahabu kwa wingi, ambazo alimpelekea Baali. Kwa hiyo wakati wa mavuno nitaichukua nafaka yangu, nitaiondoa divai yangu wakati wake. Nitamnyang'anya nguo zangu za sufu na kitani, ambazo zilitumika kuufunika uchi wake. Nitamvua abaki uchi mbele ya wapenzi wake, wala hakuna mtu atakayeweza kunizuia. Nitazikomesha starehe zake zote, sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato, na sikukuu zote zilizoamriwa. Nitaiharibu mizabibu yake na mitini, anayosema ni malipo kutoka kwa wapenzi wake. Nitaifanya iwe misitu, nao wanyama wa porini wataila. Nitamlipiza sikukuu za Baali alizoadhimisha, muda alioutumia kuwafukizia ubani, akajipamba kwa pete zake na johari, na kuwaendea wapenzi wake, akanisahau mimi. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema. Kwa hiyo, nitamshawishi, nitampeleka jangwani na kusema naye kwa upole. Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu, bonde la Akori nitalifanya lango la tumaini. Atanifuata kwa hiari kama alipokuwa kijana, kama wakati alipotoka katika nchi ya Misri. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku hiyo, wewe utaniita ‘Mume wangu,’ na sio tena ‘Baali wangu.’ Maana, nitalifanya jina la Baali lisitamkike tena kinywani mwako. Nitafanya agano na wanyama wa porini, ndege wa angani pamoja na vyote vitambaavyo, wasikuumize. Nitatokomeza upinde, upanga na silaha za vita katika nchi, na kukufanya uishi kwa usalama. Nitakufanya mke wangu milele; uwe wangu kwa uaminifu na haki, kwa fadhili na huruma. Naam, nitakuposa kwa uaminifu, nawe utanijua mimi Mwenyezi-Mungu. “Siku hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema, nitaikubali haja ya mbingu ya kunyesha mvua, mbingu nazo zitaikubali haja ya ardhi. Ardhi itaikubali haja ya nafaka, divai na mafuta, navyo vitatosheleza mahitaji ya Yezreeli. Nitamwotesha Yezreeli katika nchi; nitamhurumia ‘Asiyehurumiwa’, na wale walioitwa ‘Siwangu’, nitawaambia, ‘Nyinyi ni watu wangu.’ Nao watasema, ‘Wewe ni Mungu wetu.’”
Hosea 2:2-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Msihini mama yenu, msihini; kwa maana yeye si mke wangu, wala mimi si mume wake; na aondokane na usherati wake usiwe mbele ya uso wake, na uzinzi wake usiwe kati ya matiti yake; nisije nikamvua nguo zake akawa uchi, nikamweka katika hali aliyokuwa nayo siku ya kuzaliwa kwake, na kumfanya kama jangwa, na kumweka kama nchi kame, na kumwua kwa kiu; naam, sitawaonea rehema watoto wake; kwa maana ni watoto wa uzinzi. Maana mama yao amezini; yeye aliyewachukua mimba ametenda mambo ya aibu; maana alisema, Nitafuatana na wapenzi wangu, wanipao chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na vileo vyangu. Basi kwa ajili ya hayo, angalia, nitaiziba njia yako kwa miiba, nami nitafanya kitalu juu yake, asipate kuyaona mapito yake. Naye atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; atawatafuta, lakini hatawaona; ndipo atakaposema, Nitakwenda nikamrudie mume wangu wa kwanza; kwa maana hali yangu ya zamani ilikuwa njema kuliko hali yangu ya sasa. Maana hakujua ya kuwa mimi ndiye niliyempa ngano, na divai, na mafuta, na kumwongezea fedha na dhahabu, walivyovitumia kwa ajili ya Baali. Basi kwa ajili ya hayo, nitaitwaa tena ngano yangu kwa wakati wake, na divai yangu kwa wakati wake, nami nitamnyang'anya sufu yangu na kitani yangu, vya kumfunika uchi wake. Na sasa nitaifunua aibu yake mbele ya macho ya wapenzi wake, wala hapana mtu atakayemwokoa katika mkono wangu. Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa. Nami nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema, Hii ndiyo ujira wangu niliopewa na wapenzi wangu; nami nitaifanya kuwa msitu, na wanyama wa mashamba wataila. Nami nitamwadhibu kwa sababu ya siku za Mabaali, aliowafukizia uvumba; hapo alipojipamba kwa pete masikioni mwake, na kwa vito asema BWANA. Kwa hiyo angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo. Nami nitampa mashamba yake ya mizabibu toka huko, na bonde la Akori kuwa mlango wa tumaini; naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri. Tena siku hiyo itakuwa, asema BWANA, utaniita Ishi, wala hutaniita tena Baali. Kwa maana nitayaondoa majina ya Mabaali kinywani mwake, wala hawatatajwa tena kwa majina yao. Nami siku hiyo nitafanya agano na wanyama wa mashamba kwa ajili yao, tena na ndege wa angani, tena na wadudu wa nchi; nami nitavivunja upinde na upanga na silaha vitoke katika nchi, nami nitawalalisha salama salimini. Nami nitakuposa uwe wangu wa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema. Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua BWANA. Tena itakuwa siku hiyo, mimi nitaitika, asema BWANA; nitaziitikia mbingu, nazo zitaiitikia nchi; nayo nchi itaiitikia nafaka na divai na mafuta; nayo yataiitikia Yezreeli. Nami nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe; nami nitamrehemu yeye asiyepewa rehema; nami nitawaambia wale wasiokuwa watu wangu, Ninyi ndinyi watu wangu; nao watasema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Hosea 2:2-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Msihini mama yenu, msihini; kwa maana yeye si mke wangu, wala mimi si mume wake; na ayawekee mbali mambo ya uasherati wake yasiwe mbele ya uso wake, na mambo ya uzinzi wake yasiwe kati ya maziwa yake; nisije nikamvua nguo zake akawa uchi, nikamweka katika hali aliyokuwa nayo siku ya kuzaliwa kwake, na kumfanya kama jangwa, na kumweka kama nchi kame, na kumfisha kwa kiu; naam, sitawaonea rehema watoto wake; kwa maana ni watoto wa uzinzi. Maana mama yao amezini; yeye aliyewachukua mimba ametenda mambo ya aibu; maana alisema, Nitafuatana na wapenzi wangu, wanipao chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na vileo vyangu. Basi kwa ajili ya hayo, angalia, nitaiziba njia yako kwa miiba, nami nitafanya kitalu juu yake, asipate kuyaona mapito yake. Naye atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; atawatafuta, lakini hatawaona; ndipo atakaposema, Nitakwenda nikamrudie mume wangu wa kwanza; kwa maana hali yangu ya zamani ilikuwa njema kuliko hali yangu ya sasa. Maana hakujua ya kuwa mimi ndiye aliyempa ngano, na divai, na mafuta, na kumwongezea fedha na dhahabu, walivyovitumia kwa ajili ya Baali. Basi kwa ajili ya hayo, nitaitwaa tena ngano yangu kwa wakati wake, na divai yangu kwa wakati wake, nami nitamnyang’anya sufu yangu na kitani yangu, vya kumfunika uchi wake. Na sasa nitaifunua aibu yake mbele ya macho ya wapenzi wake, wala hapana mtu atakayemwokoa katika mkono wangu. Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa. Nami nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema, Hii ndiyo ujira wangu niliopewa na wapenzi wangu; nami nitaifanya kuwa msitu, na wanyama wa mashamba wataila. Nami nitamwadhibu kwa sababu ya siku za Mabaali, aliowafukizia uvumba; hapo alipojipamba kwa pete masikioni mwake, na kwa vito asema BWANA. Kwa hiyo angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo. Nami nitampa mashamba yake ya mizabibu toka huko, na bonde la Akori kuwa mlango wa tumaini; naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri. Tena siku hiyo itakuwa, asema BWANA, utaniita Ishi, wala hutaniita tena Baali. Kwa maana nitayaondoa majina ya Mabaali kinywani mwake, wala hawatatajwa tena kwa majina yao. Nami siku hiyo nitafanya agano na wanyama wa mashamba kwa ajili yao, tena na ndege wa angani, tena na wadudu wa nchi; nami nitavivunja upinde na upanga na silaha vitoke katika nchi, nami nitawalalisha salama salimini. Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema. Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua BWANA. Tena itakuwa siku hiyo, mimi nitaitika, asema BWANA; nitaziitikia mbingu, nazo zitaiitikia nchi; nayo nchi itaiitikia nafaka na divai na mafuta; nayo yataiitikia Yezreeli. Nami nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe; nami nitamrehemu yeye asiyepewa rehema; nami nitawaambia wale wasiokuwa watu wangu, Ninyi ndinyi watu wangu; nao watasema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Hosea 2:2-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Mkemeeni mama yenu, mkemeeni, kwa maana yeye si mke wangu, nami si mume wake. Aondoe sura ya uzinzi katika uso wake na uzinzi kati ya matiti yake. Kama sivyo nitamvua nguo zake awe uchi na kumwacha uchi kama siku ile aliyozaliwa. Nitamfanya kama jangwa, nitamgeuza awe nchi ya kiu, nami nitamuua kwa kiu. Sitaonesha upendo wangu kwa watoto wake, kwa sababu ni watoto wa uzinzi. Mama yao amekosa uaminifu na amewachukua mimba katika aibu. Gomeri alisema, ‘Nitawaendea wapenzi wangu, ambao hunipa chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na kinywaji changu.’ Kwa hiyo mimi Mungu nitaizuia njia yake kwa vichaka vya miiba, nitamjengea ukuta ili asiweze kutoka. Gomeri atawafuatia wapenzi wake lakini hatawapata; atawatafuta lakini hatawapata. Kisha atasema, ‘Nitarudi kwa mume wangu kama kwanza, kwa maana nilikuwa na hali njema kuliko sasa.’ Gomeri hajakubali kuwa mimi ndiye niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta, niliyemwongezea fedha na dhahabu waliyoitumia kwa kumtumikia Baali. “Kwa hiyo nitachukua nafaka yangu wakati itakapokomaa na divai yangu mpya wakati itakapokuwa tayari. Nitamnyangʼanya sufu yangu na kitani yangu iliyokusudiwa kufunika uchi wake. Basi sasa nitaufunua ufisadi wake mbele ya wapenzi wake; hakuna yeyote atakayemtoa mikononi mwangu. Nitakomesha furaha na macheko yake yote: sikukuu zake za mwaka, sikukuu za Miandamo ya Mwezi, siku zake za Sabato, sikukuu zake zote zilizoamriwa. Nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema yalikuwa malipo yake kutoka kwa wapenzi wake; nitaifanya kuwa kichaka, nao wanyama pori wataila. Nitamwadhibu kwa ajili ya siku alizowafukizia uvumba Mabaali; alipojipamba kwa pete na kwa vito vya thamani, na kuwaendea wapenzi wake, lakini mimi alinisahau,” asema BWANA. “Kwa hiyo sasa nitamshawishi; nitamwongoza hadi jangwani na kuzungumza naye kwa upole. Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu, nami nitalifanya Bonde la Akori mlango wa matumaini. Huko ataimba kama alivyofanya katika siku za ujana wake, kama siku zile alizotoka Misri. “Katika siku ile,” asema BWANA, “utaniita mimi ‘Mume wangu’; hutaniita tena mimi ‘Bwana wangu.’ Nitaondoa majina ya Mabaali kutoka mdomoni mwake, wala hataomba tena kwa majina yao. Katika siku ile nitafanya agano kwa ajili yao na wanyama wa kondeni, na ndege wa angani, na viumbe vinavyotambaa ardhini. Upinde, upanga na vita, nitaondolea mbali katika nchi, ili wote waweze kukaa salama. Nitakuposa uwe wangu milele; nitakuposa kwa uadilifu na haki, kwa upendo na huruma. Nitakuposa kwa uaminifu, nawe utamkubali BWANA. “Katika siku ile nitajibu,” asema BWANA, “nitajibu kwa anga, nazo anga zitajibu kwa nchi; nayo nchi itajibu kwa nafaka, divai mpya na mafuta, navyo vitajibu kwa Yezreeli. Nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe; nami nitaonesha pendo langu kwake yule ambaye nilimwita, ‘Si Mpendwa Wangu.’ Nitawaambia wale walioitwa, ‘Sio Watu Wangu,’ ‘Ninyi ni Watu Wangu’; nao watasema, ‘Wewe ndiwe Mungu wangu’.”