Hosea 13:1-6
Hosea 13:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Waefraimu waliponena, watu walitetemeka; Waefraimu walikuwa na uwezo mkubwa huko Israeli, lakini walianza kumwabudu Baali, wakajiletea kifo. Waefraimu wameendelea kutenda dhambi, wakajitengenezea sanamu za kusubu, sanamu zilizotengenezwa kwa ustadi wao, zote zikiwa kazi ya mafundi. Wanasema, “Haya zitambikieni!” Wanaume wanabusu ndama! Basi, watatoweka kama ukungu wa asubuhi, kama umande utowekao upesi; kama makapi yanayopeperushwa mahali pa kupuria, kama moshi unaotoka katika bomba. Mwenyezi-Mungu asema: “Lakini mimi, Mwenyezi-Mungu, ni Mungu wenu, ambaye niliwatoa nchini Misri; hamna mungu mwingine ila mimi, wala hakuna awezaye kuwaokoeni. Ni mimi niliyewatunza mlipokuwa jangwani, katika nchi iliyokuwa ya ukame. Lakini mlipokwisha kula na kushiba, mlianza kuwa na kiburi, mpaka mkanisahau.
Hosea 13:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Efraimu aliponena, palikuwa na tetemeko; alijitukuza katika Israeli; Lakini alipokosa katika Baali, alikufa. Na sasa wanazidi kufanya dhambi, nao wamejifanyia sanamu kwa fedha yao, naam, sanamu kwa kadiri ya akili zao; zote pia ni kazi ya mafundi; nao huzitaja hivi, Wanaume watoao dhabihu na wazibusu ndama. Kwa sababu hiyo watakuwa kama wingu la asubuhi, na kama umande utowekao upesi, kama makapi yaliyopeperushwa na tufani sakafuni, na kama moshi utokao katika bomba. Lakini mimi ni BWANA, Mungu wako tangu nchi ya Misri; wala hutamjua mungu mwingine ila mimi; wala zaidi ya mimi hakuna mwokozi. Mimi nilikujua katika jangwa, katika nchi yenye ukame. Kwa kadiri ya malisho yao, kwa kadiri iyo hiyo walishiba; walishiba na moyo wao ukatukuka; ndiyo sababu wamenisahau mimi.
Hosea 13:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Efraimu aliponena, palikuwa na tetemeko; alijitukuza katika Israeli; Lakini alipokosa katika Baali, alikufa. Na sasa wanazidi kufanya dhambi, nao wamejifanyizia sanamu kwa fedha yao, naam, sanamu kwa kadiri ya akili zao; zote pia ni kazi ya mafundi; nao huzitaja hivi, Wanaume watoao dhabihu na wazibusu ndama. Kwa sababu hiyo watakuwa kama wingu la asubuhi, na kama umande utowekao upesi, kama makapi yaliyopeperushwa na tufani sakafuni, na kama moshi utokao katika bomba. Lakini mimi ni BWANA, Mungu wako tangu nchi ya Misri; wala hutamjua mungu mwingine ila mimi; wala zaidi ya mimi hakuna Mwokozi. Mimi nalikujua katika jangwa, katika nchi yenye kiu nyingi. Kwa kadiri ya malisho yao, kwa kadiri iyo hiyo walishiba; walishiba na moyo wao ukatukuka; ndiyo sababu wamenisahau mimi.
Hosea 13:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Efraimu alipozungumza, watu walitetemeka; alitukuzwa katika Israeli. Lakini alikuwa na hatia ya kumwabudu Baali, naye akafa. Sasa wanatenda dhambi zaidi na zaidi; wanajitengenezea sanamu kutokana na fedha yao, vinyago vilivyotengenezwa kwa uhodari, vyote kazi ya fundi stadi. Inasemekana kuhusu hawa watu, “Hutoa dhabihu za binadamu na kubusu sanamu za ndama.” Kwa hiyo watakuwa kama ukungu wa asubuhi, kama umande wa alfajiri utowekao, kama makapi yapeperushwayo kutoka sakafu ya kupuria nafaka, kama moshi utorokao kupitia dirishani. “Bali mimi ndimi BWANA Mungu wenu, niliyewaleta ninyi toka Misri. Msimkubali Mungu mwingine ila mimi, hakuna Mwokozi isipokuwa mimi. Niliwatunza huko jangwani, katika nchi yenye joto liunguzalo. Nilipowalisha, walishiba, waliposhiba, wakajivuna, kisha wakanisahau mimi.