Hosea 13:1-16
Hosea 13:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Waefraimu waliponena, watu walitetemeka; Waefraimu walikuwa na uwezo mkubwa huko Israeli, lakini walianza kumwabudu Baali, wakajiletea kifo. Waefraimu wameendelea kutenda dhambi, wakajitengenezea sanamu za kusubu, sanamu zilizotengenezwa kwa ustadi wao, zote zikiwa kazi ya mafundi. Wanasema, “Haya zitambikieni!” Wanaume wanabusu ndama! Basi, watatoweka kama ukungu wa asubuhi, kama umande utowekao upesi; kama makapi yanayopeperushwa mahali pa kupuria, kama moshi unaotoka katika bomba. Mwenyezi-Mungu asema: “Lakini mimi, Mwenyezi-Mungu, ni Mungu wenu, ambaye niliwatoa nchini Misri; hamna mungu mwingine ila mimi, wala hakuna awezaye kuwaokoeni. Ni mimi niliyewatunza mlipokuwa jangwani, katika nchi iliyokuwa ya ukame. Lakini mlipokwisha kula na kushiba, mlianza kuwa na kiburi, mpaka mkanisahau. Basi, nitakuwa kama simba kwenu nyote; nitawavizieni kama chui njiani. Nitawarukieni kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake. Nitawararua vifua vyenu na kuwala papo hapo kama simba; nitawararua vipandevipande kama mnyama wa porini. “Nitawaangamiza, enyi Waisraeli. Nani ataweza kuwasaidia? Yuko wapi sasa mfalme wenu awaokoe? Wako wapi wale wakuu wenu wawalinde? Nyinyi ndio mlioomba: ‘Tupatie mfalme na wakuu watutawale.’ Kwa hasira yangu mimi nikawapa mfalme, kisha nikamwondoa kwa ghadhabu yangu. “Uovu wa Efraimu uko umeandikwa, dhambi yake imehifadhiwa ghalani. Maumivu kama ya kujifungua mtoto yanamfikia. Lakini yeye ni mtoto mpumbavu; wakati ufikapo wa kuzaliwa yeye hukataa kutoka tumboni kwa mama! Yanibidi kuwakomboa hawa watu kutoka kuzimu; sharti niwaokoe kutoka kifoni! Ewe Kifo, yako wapi maafa yako? Ewe Kuzimu, yako wapi maangamizi yako? Mimi sitawaonea tena huruma! “Hata kama Efraimu atastawi kama nyasi, mimi Mwenyezi-Mungu nitavumisha upepo wa mashariki, upepo utakaozuka huko jangwani, navyo visima vyake vitakwisha maji, chemchemi zake zitakauka. Hazina zake zote za thamani zitanyakuliwa.” Watu wa Samaria wataadhibiwa kwa kosa lao. Kwa sababu wamemwasi Mungu wao. Watauawa kwa upanga, vitoto vyao vitapondwapondwa, na kina mama wajawazito watatumbuliwa.
Hosea 13:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Efraimu aliponena, palikuwa na tetemeko; alijitukuza katika Israeli; Lakini alipokosa katika Baali, alikufa. Na sasa wanazidi kufanya dhambi, nao wamejifanyia sanamu kwa fedha yao, naam, sanamu kwa kadiri ya akili zao; zote pia ni kazi ya mafundi; nao huzitaja hivi, Wanaume watoao dhabihu na wazibusu ndama. Kwa sababu hiyo watakuwa kama wingu la asubuhi, na kama umande utowekao upesi, kama makapi yaliyopeperushwa na tufani sakafuni, na kama moshi utokao katika bomba. Lakini mimi ni BWANA, Mungu wako tangu nchi ya Misri; wala hutamjua mungu mwingine ila mimi; wala zaidi ya mimi hakuna mwokozi. Mimi nilikujua katika jangwa, katika nchi yenye ukame. Kwa kadiri ya malisho yao, kwa kadiri iyo hiyo walishiba; walishiba na moyo wao ukatukuka; ndiyo sababu wamenisahau mimi. Basi nimekuwa kama simba kwao; kama chui nitavizia njiani; nitawajia kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake; nami nitararua nyama ya mioyo yao; na huko nitawala kama simba; huyo mnyama mkali atawararua. Haya ndiyo maangamizo yako, Ee Israeli, kwa kuwa wewe u kinyume changu mimi, kinyume cha msaada wako. Yuko wapi sasa mfalme wako, apate kukuokoa katika miji yako yote? Na hao waamuzi wako, uliowanena hivi, Nipe mfalme na wakuu? Nimekupa mfalme katika hasira yangu, nikamwondoa katika ghadhabu yangu. Uovu wa Efraimu umefungwa kwa kukazwa; dhambi yake imewekwa akiba. Uchungu wa mwanamke mwenye mimba utampata; yeye ni mwana asiye na akili; maana wakati umewadia, ambao haimpasi kukawia mahali wapenyapo watoto. Nitawakomboa kwa nguvu za kaburi; nitawaokoa kutoka kwa mauti; ewe mauti, ya wapi mapigo yako? Ewe kaburi, ku wapi kuharibu kwako? Huruma itafichika machoni mwangu. Ajapokuwa yeye ni mwenye kuzaa sana kati ya ndugu zake, upepo wa mashariki utakuja, hiyo pumzi ya BWANA itokayo upande wa nyikani, na kijito chake cha maji kitakauka, na chemchemi yake itakaushwa; yeye atateka nyara hazina ya vyombo vyote vipendezavyo. Samaria atachukua hatia yake; kwa maana amemwasi Mungu wake; wataanguka kwa upanga; watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande, na wanawake wao wenye mimba watatumbuliwa.
Hosea 13:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Efraimu aliponena, palikuwa na tetemeko; alijitukuza katika Israeli; Lakini alipokosa katika Baali, alikufa. Na sasa wanazidi kufanya dhambi, nao wamejifanyizia sanamu kwa fedha yao, naam, sanamu kwa kadiri ya akili zao; zote pia ni kazi ya mafundi; nao huzitaja hivi, Wanaume watoao dhabihu na wazibusu ndama. Kwa sababu hiyo watakuwa kama wingu la asubuhi, na kama umande utowekao upesi, kama makapi yaliyopeperushwa na tufani sakafuni, na kama moshi utokao katika bomba. Lakini mimi ni BWANA, Mungu wako tangu nchi ya Misri; wala hutamjua mungu mwingine ila mimi; wala zaidi ya mimi hakuna Mwokozi. Mimi nalikujua katika jangwa, katika nchi yenye kiu nyingi. Kwa kadiri ya malisho yao, kwa kadiri iyo hiyo walishiba; walishiba na moyo wao ukatukuka; ndiyo sababu wamenisahau mimi. Basi nimekuwa kama simba kwao; kama chui nitavizia njiani; nitakutana nao kama dubu aliyenyang’anywa watoto wake; nami nitararua nyama ya mioyo yao; na huko nitawala kama simba; huyo mnyama mkali atawararua. Haya ndiyo maangamizo yako, Ee Israeli, ya kuwa wewe u kinyume changu mimi, kinyume cha msaada wako. Yuko wapi sasa mfalme wako, apate kukuokoa katika miji yako yote? Na hao waamuzi wako, uliowanena hivi, Nipe mfalme na wakuu? Nimekupa mfalme katika hasira yangu, nikamwondoa katika ghadhabu yangu. Uovu wa Efraimu umefungwa kwa kukazwa; dhambi yake imewekwa akiba. Utungu wa mwanamke mwenye mimba utampata; yeye ni mwana asiye na akili; maana wakati umewadia, ambao haimpasi kukawia mahali wapenyapo watoto. Nitawakomboa na nguvu za kaburi; nitawaokoa na mauti; ewe mauti, ya wapi mapigo yako? Ewe kaburi, ku wapi kuharibu kwako? Kujuta kutafichwa na macho yangu. Ajapokuwa yeye ni mwenye kuzaa sana kati ya ndugu zake, upepo wa mashariki utakuja, hiyo pumzi ya BWANA itokayo upande wa nyikani, na kijito chake cha maji kitakauka, na chemchemi yake itakaushwa; yeye atateka nyara hazina ya vyombo vyote vipendezavyo. Samaria atachukua hatia yake; kwa maana amemwasi Mungu wake; wataanguka kwa upanga; watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande, na wanawake wao wenye mimba watatambuliwa.
Hosea 13:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Efraimu alipozungumza, watu walitetemeka; alitukuzwa katika Israeli. Lakini alikuwa na hatia ya kumwabudu Baali, naye akafa. Sasa wanatenda dhambi zaidi na zaidi; wanajitengenezea sanamu kutokana na fedha yao, vinyago vilivyotengenezwa kwa uhodari, vyote kazi ya fundi stadi. Inasemekana kuhusu hawa watu, “Hutoa dhabihu za binadamu na kubusu sanamu za ndama.” Kwa hiyo watakuwa kama ukungu wa asubuhi, kama umande wa alfajiri utowekao, kama makapi yapeperushwayo kutoka sakafu ya kupuria nafaka, kama moshi utorokao kupitia dirishani. “Bali mimi ndimi BWANA Mungu wenu, niliyewaleta ninyi toka Misri. Msimkubali Mungu mwingine ila mimi, hakuna Mwokozi isipokuwa mimi. Niliwatunza huko jangwani, katika nchi yenye joto liunguzalo. Nilipowalisha, walishiba, waliposhiba, wakajivuna, kisha wakanisahau mimi. Kwa hiyo nitakuja juu yao kama simba, kama chui nitawavizia kando ya njia. Kama dubu aliyenyangʼanywa watoto wake, nitawashambulia na kurarua vifua vyenu. Kama simba nitawala; mnyama pori atawararua vipande vipande. “Ee Israeli, umeangamizwa, kwa sababu wewe u kinyume nami, kinyume na msaidizi wako. Yuko wapi mfalme wako, ili apate kukuokoa? Wako wapi watawala wako katika miji yako yote ambao ulisema kuwahusu, ‘Nipe mfalme na wakuu’? Hivyo katika hasira yangu nilikupa mfalme na katika ghadhabu yangu nilimwondoa. Kosa la Efraimu limehifadhiwa, dhambi zake zimewekwa katika kumbukumbu. Uchungu kama wa mwanamke anayejifungua mtoto humjia, lakini yeye ni mtoto asiyekuwa na hekima; wakati utakapowadia hatatoka katika tumbo la mama yake. “Nitawakomboa watu hawa kutoka nguvu za kaburi, nitawakomboa kutoka mautini. Yako wapi, ee mauti, mateso yako? Uko wapi, ee Kuzimu, uharibifu wako? “Sitakuwa na huruma, hata ingawa Efraimu atastawi miongoni mwa ndugu zake. Upepo wa mashariki kutoka kwa BWANA utakuja, ukivuma kutoka jangwani, chemchemi yake haitatoa maji na kisima chake kitakauka. Ghala lake litatekwa hazina zake zote. Watu wa Samaria ni lazima wabebe hatia yao, kwa sababu wameasi dhidi ya Mungu wao. Wataanguka kwa upanga; watoto wao wadogo watatupwa kwa nguvu ardhini, wanawake wao walio na mimba watatumbuliwa.”