Hosea 1:1-11
Hosea 1:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Bwana lililomjia Hosea mwana wa Beeri, nyakati za Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli. Mwenyezi-Mungu alipoanza kuongea na Waisraeli kwa njia ya Hosea, alimwambia hivi: “Nenda ukaoe mwanamke mzinzi, uzae naye watoto wa uzinzi, maana watu wa nchi hii wanafanya uzinzi mwingi kwa kuniacha mimi.” Basi, Hosea akaenda, akamwoa Gomeri, binti Diblaimu. Gomeri akapata mimba, akamzalia Hosea mtoto wa kiume. Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Yezreeli’, maana bado kitambo kidogo tu, nami nitaiadhibu jamaa ya Yehu kwa mauaji aliyoyafanya bondeni Yezreeli. Nitaufutilia mbali ufalme katika taifa la Israeli. Siku hiyo, nitazivunja nguvu za kijeshi za Israeli huko bondeni Yezreeli.” Gomeri alipata mimba tena, akazaa mtoto wa kike. Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Asiyehurumiwa’, maana sitawahurumia tena Waisraeli wala sitawasamehe. Lakini nitawahurumia watu wa Yuda na kuwaokoa. Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, nitawaokoa, lakini si kwa nguvu za kijeshi, au pinde, au panga, au farasi au wapandafarasi.” Gomeri alipomwachisha kunyonya “Asiyehurumiwa,” alipata mimba tena, akamzalia Hosea mtoto mwingine wa kiume. Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Siwangu,’ maana nyinyi si watu wangu, wala mimi si wenu.” Lakini idadi ya Waisraeli itakuwa kubwa kama mchanga wa pwani ambao haupimiki wala hauhesabiki. Pale ambapo Mungu aliwaambia, “Nyinyi si watu wangu,” sasa atawaambia, “Nyinyi ni watoto wa Mungu aliye hai.” Watu wa Yuda na wa Israeli wataungana pamoja na kumchagua kiongozi wao mmoja; nao watastawi katika nchi yao. Hiyo itakuwa siku maarufu ya Yezreeli.
Hosea 1:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hili ndilo neno la BWANA lililomjia Hosea, mwana wa Beeri, siku za Uzia, na Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli. Hapo kwanza BWANA aliponena kwa kinywa cha Hosea, BWANA alimwambia Hosea, Nenda ukatwae mke wa uzinzi, na watoto wa uzinzi; kwa maana nchi hii inafanya uzinzi mwingi, kwa kumwacha BWANA. Basi akaenda akamwoa Gomeri, binti Diblaimu; naye akachukua mimba, akamzalia mtoto wa kiume. BWANA akamwambia, Mwite jina lake Yezreeli; kwa maana bado kitambo kidogo, nitaipatiliza nyumba ya Yehu damu ya Yezreeli, na kuukomesha ufalme wa nyumba ya Israeli. Tena itakuwa siku ile, nitauvunja upinde wa Israeli katika bonde la Yezreeli. Akachukua mimba tena, akazaa mtoto wa kike, BWANA akamwambia, Mwite jina lake Lo-ruhama; kwa maana sitairehemu nyumba ya Israeli tena, nisije nikawasamehe kwa njia yoyote. Lakini nitairehemu nyumba ya Yuda; nitawaokoa kwa BWANA, Mungu wao; wala sitawaokoa kwa upinde, wala kwa upanga, wala kwa silaha, wala kwa farasi, wala kwa wapanda farasi. Basi, akiisha kumwachisha Lo-ruhama kunyonya, akachukua mimba, akazaa mtoto wa kiume. BWANA akasema, Mwite jina lake Lo-ami; kwa maana ninyi si watu wangu, wala mimi sitakuwa Mungu wenu. Tena itakuwa ya kwamba hesabu ya wana wa Israeli itafanana na mchanga wa bahari, usioweza kupimwa wala kuhesabiwa; tena itakuwa, badala ya kuambiwa, Ninyi si watu wangu, wataambiwa, Ninyi ndio wana wa Mungu aliye hai. Na wana wa Yuda na wana wa Israeli watakusanyika pamoja, nao watajichagulia kiongozi mmoja, nao watakwea watoke katika nchi hii; kwa maana siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.
Hosea 1:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hili ndilo neno la BWANA lililomjia Hosea, mwana wa Beeri, siku za Uzia, na Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli. Hapo kwanza BWANA aliponena kwa kinywa cha Hosea, BWANA alimwambia Hosea, Enenda ukatwae mke wa uzinzi, na watoto wa uzinzi; kwa maana nchi hii inafanya uzinzi mwingi, kwa kumwacha BWANA. Basi akaenda akamwoa Gomeri, binti Diblaimu; naye akachukua mimba, akamzalia mtoto mwanamume. BWANA akamwambia, Mwite jina lake Yezreeli; kwa maana bado kitambo kidogo, nitaipatiliza nyumba ya Yehu damu ya Yezreeli, na kuukomesha ufalme wa nyumba ya Israeli. Tena itakuwa siku ile, nitauvunja upinde wa Israeli katika bonde la Yezreeli. Akachukua mimba tena, akazaa mtoto mwanamke. BWANA akamwambia, Mwite jina lake Lo-ruhama; kwa maana sitairehemu nyumba ya Israeli tena, nisije nikawasamehe kwa njia yo yote. Lakini nitairehemu nyumba ya Yuda; nitawaokoa kwa BWANA, Mungu wao; wala sitawaokoa kwa upinde, wala kwa upanga, wala kwa silaha, wala kwa farasi, wala kwa wapanda farasi. Basi, akiisha kumwachisha Lo-ruhama, akachukua mimba, akazaa mtoto mwanamume. BWANA akasema, Mwite jina lake Lo-ami; kwa maana ninyi si watu wangu, wala mimi sitakuwa Mungu wenu. Tena itakuwa ya kwamba hesabu ya wana wa Israeli itafanana na mchanga wa bahari, usioweza kupimwa wala kuhesabiwa; tena itakuwa, badala ya kuambiwa, Ninyi si watu wangu, wataambiwa, Ninyi ndio wana wa Mungu aliye hai. Na wana wa Yuda na wana wa Israeli watakusanyika pamoja, nao watajiwekea kichwa kimoja, nao watakwea watoke katika nchi hii; kwa maana siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.
Hosea 1:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno la BWANA lililomjia Hosea mwana wa Beeri wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na wakati wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi, mfalme wa Israeli. BWANA alipoanza kuzungumza kupitia Hosea, BWANA alimwambia, “Nenda ukajitwalie mwanamke wa uzinzi na watoto wa uzinzi, kwa sababu nchi ina hatia ya uzinzi wa kupindukia kwa kumwacha BWANA.” Kwa hiyo alimwoa Gomeri binti Diblaimu, naye akachukua mimba na kumzalia Hosea mwana. Kisha BWANA akamwambia Hosea, “Mwite jina Yezreeli, kwa kuwa kitambo kidogo nitaiadhibu nyumba ya Yehu kwa ajili ya mauaji ya kule Yezreeli, nami nitaukomesha ufalme wa Israeli. Katika siku ile nitavunja upinde wa Israeli katika Bonde la Yezreeli.” Gomeri akachukua tena mimba akamzaa binti. Kisha BWANA akamwambia Hosea, “Mwite Lo-Ruhama, kwa maana sitaonesha tena upendo kwa nyumba ya Israeli, kwamba nisije kabisa nikawasamehe. Hata hivyo nitaonesha upendo kwa nyumba ya Yuda, nami nitawaokoa si kwa upinde, upanga au vita, wala kwa farasi na wapanda farasi, bali kupitia BWANA Mungu wao.” Baada ya Gomeri kumwachisha Lo-Ruhama kunyonya, Gomeri alipata mwana mwingine. Kisha BWANA akasema, “Mwite Lo-Ami kwa maana ninyi si watu wangu, nami si Mungu wenu. “Hata hivyo Waisraeli watakuwa kama mchanga kando ya bahari, ambao hauwezi kupimika wala kuhesabiwa. Mahali pale walipoambiwa, ‘Ninyi si watu wangu,’ wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai’. Watu wa Yuda na watu wa Israeli wataunganishwa tena, nao watamchagua kiongozi mmoja nao watakwea watoke katika nchi, kwa kuwa siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.