Waebrania 7:1-28
Waebrania 7:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Huyo Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme, Melkisedeki alikutana naye, akambariki, naye Abrahamu akampa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina Melkisedeki ni “Mfalme wa Uadilifu;” na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina maana ya “Mfalme wa Amani.”) Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi; haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima. Basi, mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Babu Abrahamu alimpa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyoteka nyara vitani. Tunajua pia kwamba kufuatana na sheria, wazawa wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo haki ya kuchukua sehemu moja ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao ni wazawa wa Abrahamu. Lakini huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya Mungu. Hakuna mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu kuliko yule anayebarikiwa. Tena, hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi. Twaweza, basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye wazawa wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia. Maana Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake, Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye. Kutokana na ukuhani wa Walawi, watu wa Israeli walipewa sheria. Sasa, kama huduma ya Walawi ingalikuwa kamilifu, hapangekuwa tena na haja ya kutokea ukuhani mwingine tofauti, na ambao umefuata utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki, na si ule wa Aroni. Maana ukuhani ukibadilika, ni lazima sheria nayo ibadilike. Naye Bwana wetu ambaye mambo hayo yote yanasemwa juu yake, alikuwa wa kabila lingine, na wala hakuna hata mmoja wa kabila lake aliyepata kutumikia madhabahuni akiwa kuhani. Inafahamika wazi kwamba yeye alizaliwa katika kabila la Yuda ambalo Mose hakulitaja alipokuwa anasema juu ya makuhani. Tena jambo hili ni dhahiri zaidi: Kuhani mwingine anayefanana na Melkisedeki amekwisha tokea. Yeye hakufanywa kuhani kwa sheria na maagizo ya kibinadamu, bali kwa nguvu ya uhai ambao hauna mwisho. Maana Maandiko yasema: “Wewe ni kuhani milele, kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.” Basi, ile amri ya zamani ilifutwa kwa sababu ilikuwa hafifu na isiyofaa kitu. Maana sheria ya Mose haikuweza kukamilisha jambo lolote. Lakini sasa, mahali pake pamewekwa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo tunaweza kumkaribia Mungu. Zaidi ya hayo, hapa pana kiapo cha Mungu. Wakati wale wengine walipofanywa makuhani hapakuwako kiapo. Lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia: “Bwana ameapa, wala hatabadili nia yake: ‘Wewe ni kuhani milele.’” Basi, kutokana na tofauti hii, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi. Tena: Hao makuhani wengine walikuwa wengi kwa sababu walikufa na hawakuweza kuendelea na kazi yao. Lakini Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake. Hivyo, yeye anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu. Basi, ilikuwa jambo la kufaa sana kwetu kuwa na kuhani kama huyo, mtakatifu, asiye na hatia wala dhambi ndani yake; ametenganishwa mbali na wenye dhambi, na ameinuliwa juu ya mbingu. Tofauti na makuhani wengine, yeye hahitaji kutoa tambiko kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Yeye alifanya hivyo mara moja kwa ajili ya watu wote, alipojitoa yeye mwenyewe, na hiyo yatosha kwa nyakati zote. Sheria huwateua watu walio dhaifu kuwa makuhani wakuu; lakini ahadi ya Mungu aliyoifanya kwa kiapo na ambayo imefika baada ya sheria imemteua Mwana ambaye amefanywa mkamilifu milele.
Waebrania 7:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Abrahamu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; ambaye Abrahamu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele. Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Abrahamu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara. Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani, ndugu zao, kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika uzao wa Abrahamu. Bali yeye, ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Abrahamu, akambariki yeye aliye na ile ahadi. Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa. Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi; bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yuko hai. Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Abrahamu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi; kwa maana alikuwa katika viuno vya baba yake, hapo Melkizedeki alipokutana naye. Basi, kama ukamilifu ulikuwapo kwa ukuhani wa Lawi; (maana watu wale waliipata sheria kwa huo); kulikuwa na haja gani tena ya kuhani mwingine awepo, kwa mfano wa Melkizedeki, wala asihesabiwe kwa mfano wa Haruni? Maana ukuhani ule ukibadilika, hapana budi sheria nayo ibadilike. Maana yeye aliyenenwa hayo alikuwa mshirika wa kabila nyingine, ambayo hapana mtu wa kabila hilo aliyeihudumia madhabahu. Maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika Yuda, kabila ambalo Musa hakunena neno lolote juu yake katika mambo ya ukuhani. Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine kama Melkizedeki; asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na kikomo; maana ameshuhudiwa kwamba, Wewe u kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki. Maana, kuna kubatiliwa kwa ile amri iliyotangulia, kwa sababu ya udhaifu wake, na kutokufaa kwake; (kwa maana ile sheria haikukamilisha neno); na pamoja na hayo kuliingizwa matumaini yaliyo mazuri zaidi, ambayo kwa hayo tunamkaribia Mungu. Na kwa kuwa haikuwa pasipo kiapo, (maana wale walifanywa makuhani pasipo kiapo; bali yeye, pamoja na kiapo, kwa yeye aliyemwambia, Bwana ameapa wala hataghairi, Wewe u kuhani milele;) basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi. Tena wale walifanywa makuhani wengi, kwa sababu walizuiliwa na mauti wasikae; bali yeye, kwa kuwa anakaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, anaweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lolote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake. Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliyekamilika hata milele.
Waebrania 7:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele. Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara. Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani, ndugu zao, kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika viuno vya Ibrahimu. Bali yeye, ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Ibrahimu, akambariki yeye aliye na ile ahadi. Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa. Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi; bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yu hai. Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi; kwa maana alikuwa katika viuno vya baba yake, hapo Melkizedeki alipokutana naye. Basi, kama ukamilifu ulikuwapo kwa ukuhani wa Lawi; (maana watu wale waliipata sheria kwa huo); kulikuwa na haja gani tena ya kuhani mwingine ainuke, kwa mfano wa Melkizedeki, wala asihesabiwe kwa mfano wa Haruni? Maana ukuhani ule ukibadilika, hapana budi sheria nayo ibadilike. Maana yeye aliyenenwa hayo alikuwa mshirika wa kabila nyingine, ambayo hapana mtu wa kabila hiyo aliyeihudumia madhabahu. Maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika Yuda, kabila ambayo Musa hakunena neno lo lote juu yake katika mambo ya ukuhani. Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine mithili ya Melkizedeki; asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo; maana ameshuhudiwa kwamba, Wewe u kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki. Maana, kuna kubatiliwa kwa ile amri iliyotangulia, kwa sababu ya udhaifu wake, na kutokufaa kwake; (kwa maana ile sheria haikukamilisha neno); na pamoja na hayo kuliingizwa matumaini yaliyo mazuri zaidi, ambayo kwa hayo twamkaribia Mungu. Na kwa kuwa haikuwa pasipo kiapo, (maana wale walifanywa makuhani pasipo kiapo; bali yeye, pamoja na kiapo, kwa yeye aliyemwambia, Bwana ameapa wala hataghairi, Wewe u kuhani milele;) basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi. Tena wale walifanywa makuhani wengi, kwa sababu wazuiliwa na mauti wasikae; bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake. Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliyekamilika hata milele.
Waebrania 7:1-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa kuwa huyu Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. Alipokutana na Abrahamu akirudi kutoka kuwashinda wafalme, Melkizedeki alimbariki, naye Abrahamu alimpa sehemu ya kumi ya kila kitu. Kwanza, jina hilo Melkizedeki maana yake ni “mfalme wa haki”. Na pia “mfalme wa Salemu” maana yake ni “mfalme wa amani”. Hana baba wala mama, hana ukoo, hana mwanzo wala mwisho wa siku zake, kama Mwana wa Mungu. Yeye adumu akiwa kuhani milele. Tazama jinsi alivyokuwa mkuu: Hata Abrahamu, baba yetu wa zamani, alimpa sehemu ya kumi ya nyara zake. Basi sheria inawaagiza wana wa Lawi ambao hufanyika makuhani kupokea sehemu ya kumi kutoka kwa watu ambao ni ndugu zao, ingawa ndugu zao ni wazao wa Abrahamu. Huyu Melkizedeki, ingawa hakufuatia ukoo wake kutoka kwa Lawi, lakini alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu na kumbariki yeye aliyekuwa na zile ahadi. Wala hakuna shaka kwamba mdogo hubarikiwa na aliye mkuu kuliko yeye. Kwa upande mmoja, sehemu ya kumi hupokelewa na watu ambao hufa; lakini kwa upande mwingine hupokelewa na yeye ambaye hushuhudiwa kuwa yu hai. Mtu anaweza hata kusema kwamba Lawi, ambaye hupokea sehemu ya kumi, alitoa hiyo sehemu ya kumi kupitia kwa Abrahamu, kwa sababu Melkizedeki alipokutana na Abrahamu, Lawi alikuwa bado katika viuno vya baba yake wa zamani. Kama ukamilifu ungeweza kupatikana kupitia kwa ukuhani wa Walawi (kwa kuwa katika msingi huo, sheria ilitolewa kwa watu), kwa nini basi kulikuwa na haja ya kuja kuhani mwingine: kuhani kwa mfano wa Melkizedeki, wala si kwa mfano wa Haruni? Kwa kuwa ukuhani ukibadilika, lazima sheria nayo ibadilike. Yeye ambaye mambo haya yanasemwa alikuwa wa kabila lingine, na hakuna mtu wa kabila hilo aliyewahi kuhudumu katika madhabahu. Kwa maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika uzao wa Yuda, tena kuhusu kabila hilo Musa hakusema lolote kwa habari za makuhani. Tena hayo tuliyosema yako wazi zaidi kama akitokea kuhani mwingine kama Melkizedeki, yeye ambaye amefanyika kuhani si kwa misingi ya sheria kama ilivyokuwa kwa baba zake, bali kwa misingi ya uwezo wa uzima usioharibika. Kwa maana imeshuhudiwa kwamba: “Wewe ni kuhani milele, kwa mfano wa Melkizedeki.” Kwa upande mmoja, ile amri ya mwanzo isiyofaa na dhaifu imebatilishwa (kwa maana sheria haikufanya kitu chochote kuwa kikamilifu). Kwa upande mwingine, tumeletewa tumaini lililo bora zaidi ambalo linatuleta karibu na Mungu. Nalo tumaini hilo halikutolewa pasipo kiapo! Wengine walikuwa makuhani pasipo kiapo chochote, lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alimwambia: “Bwana ameapa naye hatabadilisha mawazo yake: ‘Wewe ni kuhani milele.’” Kwa ajili ya kiapo hiki, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi. Basi kumekuwa na makuhani wengi wa aina hiyo, kwa kuwa kifo kiliwazuia kuendelea na huduma yao ya ukuhani. Lakini kwa sababu Yesu anaishi milele, anao ukuhani wa kudumu. Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kabisa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake, kwa sababu yeye adumu daima kuomba kwa ajili yao. Kwa kuwa ilitupasa tuwe na Kuhani Mkuu wa namna hii, yaani aliye mtakatifu, asiye na lawama, asiye na dosari, aliyetengwa na wenye dhambi na kuinuliwa juu ya mbingu. Yeye hahitaji kutoa dhabihu siku kwa siku kwa ajili ya dhambi, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu kama wale makuhani wakuu wengine. Yeye alitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zao mara moja tu, alipojitoa mwenyewe. Kwa kuwa sheria huwaweka makuhani wakuu watu ambao ni dhaifu; lakini lile neno la kiapo, lililokuja baada ya sheria, lilimweka Mwana, ambaye amefanywa kuwa mkamilifu milele.