Waebrania 7:1-10
Waebrania 7:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Huyo Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme, Melkisedeki alikutana naye, akambariki, naye Abrahamu akampa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina Melkisedeki ni “Mfalme wa Uadilifu;” na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina maana ya “Mfalme wa Amani.”) Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi; haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima. Basi, mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Babu Abrahamu alimpa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyoteka nyara vitani. Tunajua pia kwamba kufuatana na sheria, wazawa wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo haki ya kuchukua sehemu moja ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao ni wazawa wa Abrahamu. Lakini huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya Mungu. Hakuna mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu kuliko yule anayebarikiwa. Tena, hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi. Twaweza, basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye wazawa wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia. Maana Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake, Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye.
Waebrania 7:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Abrahamu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; ambaye Abrahamu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele. Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Abrahamu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara. Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani, ndugu zao, kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika uzao wa Abrahamu. Bali yeye, ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Abrahamu, akambariki yeye aliye na ile ahadi. Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa. Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi; bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yuko hai. Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Abrahamu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi; kwa maana alikuwa katika viuno vya baba yake, hapo Melkizedeki alipokutana naye.
Waebrania 7:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele. Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara. Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani, ndugu zao, kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika viuno vya Ibrahimu. Bali yeye, ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Ibrahimu, akambariki yeye aliye na ile ahadi. Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa. Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi; bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yu hai. Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi; kwa maana alikuwa katika viuno vya baba yake, hapo Melkizedeki alipokutana naye.
Waebrania 7:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa kuwa huyu Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. Alipokutana na Abrahamu akirudi kutoka kuwashinda wafalme, Melkizedeki alimbariki, naye Abrahamu alimpa sehemu ya kumi ya kila kitu. Kwanza, jina hilo Melkizedeki maana yake ni “mfalme wa haki”. Na pia “mfalme wa Salemu” maana yake ni “mfalme wa amani”. Hana baba wala mama, hana ukoo, hana mwanzo wala mwisho wa siku zake, kama Mwana wa Mungu. Yeye adumu akiwa kuhani milele. Tazama jinsi alivyokuwa mkuu: Hata Abrahamu, baba yetu wa zamani, alimpa sehemu ya kumi ya nyara zake. Basi sheria inawaagiza wana wa Lawi ambao hufanyika makuhani kupokea sehemu ya kumi kutoka kwa watu ambao ni ndugu zao, ingawa ndugu zao ni wazao wa Abrahamu. Huyu Melkizedeki, ingawa hakufuatia ukoo wake kutoka kwa Lawi, lakini alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu na kumbariki yeye aliyekuwa na zile ahadi. Wala hakuna shaka kwamba mdogo hubarikiwa na aliye mkuu kuliko yeye. Kwa upande mmoja, sehemu ya kumi hupokelewa na watu ambao hufa; lakini kwa upande mwingine hupokelewa na yeye ambaye hushuhudiwa kuwa yu hai. Mtu anaweza hata kusema kwamba Lawi, ambaye hupokea sehemu ya kumi, alitoa hiyo sehemu ya kumi kupitia kwa Abrahamu, kwa sababu Melkizedeki alipokutana na Abrahamu, Lawi alikuwa bado katika viuno vya baba yake wa zamani.