Waebrania 6:1-8
Waebrania 6:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, tuyaache nyuma yale mafundisho ya mwanzomwanzo juu ya Kristo, tusonge mbele kwa yale yaliyokomaa, na sio kuendelea kuweka msingi kuhusu kuachana na matendo ya kifo, na juu ya kumwamini Mungu; mafundisho juu ya ubatizo na kuwekewa mikono; ufufuo wa wafu na hukumu ya milele. Hilo tutafanya, Mungu akipenda. Maana watu waliokwisha kuangaziwa, wakaonja zawadi za mbinguni, wakashirikishwa Roho Mtakatifu na kuonja wema wa neno la Mungu na nguvu za ulimwengu ujao, kisha wakaiasi imani yao, haiwezekani kuwarudisha hao watubu tena. Hao wanamsulubisha tena Mwana wa Mungu kwa makusudi na kumwaibisha hadharani. Ardhi ambayo huipokea mvua inayoinyeshea mara kwa mara na kuotesha mimea ya faida kwa mkulima imebarikiwa na Mungu. Ardhi ikiota miti ya miiba na magugu, haina faida; karibu italaaniwa na Mungu na mwisho wake ni kuchomwa moto.
Waebrania 6:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, na wa mafundisho ya ubatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. Na hayo tutafanya Mungu akitujalia. Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu, na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za wakati ujao, wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulubisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumtweza hadharani kwa dhahiri. Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao inalimwa, hupokea baraka zitokazo kwa Mungu; bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa.
Waebrania 6:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. Na hayo tutafanya Mungu akitujalia. Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu, na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo, wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri. Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao yalimwa, hushiriki baraka zitokazo kwa Mungu; bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa.
Waebrania 6:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa hiyo, tukiachana na mafundisho yale ya awali kuhusu Kristo na tukisonga mbele ili tufikie utimilifu, tusiweke tena msingi wa mafundisho ya kuzitubia kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu, mafundisho kuhusu aina za ubatizo, kuwekea watu mikono, ufufuo wa wafu, na hukumu ya milele. Mungu akitujalia tutafanya hivyo. Kwa kuwa ni vigumu kwa wale ambao wakati fulani walishapata nuru, ambao walishaonja kipawa cha mbinguni, ambao wamekwisha kushiriki katika Roho Mtakatifu, ambao wameonja uzuri wa neno la Mungu na nguvu za wakati ujao, kisha wakianguka, kuwarejesha tena katika toba. Kwa kuwa wanamsulubisha Mwana wa Mungu tena na kumdhalilisha hadharani, nayo ikawa hasara kwao. Ardhi inayopokea mvua inayonyesha mara kwa mara juu yake na baadaye inatoa mazao ya kuwanufaisha wale ambao inalimwa kwa ajili yao, hupokea baraka za Mungu. Lakini ardhi ikizaa miiba na mibaruti, haina thamani na iko hatarini kulaaniwa. Mwisho wake ni kuchomwa moto.