Waebrania 2:1-18
Waebrania 2:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa hiyo tunapaswa kuzingatia kwa makini yote tuliyosikia, tusije tukayakosa. Ujumbe ule waliopewa wazee wetu na malaika ulioneshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili. Basi, sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu, na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli. Mungu pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu, na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake. Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake. Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko: “Mtu ni nini, hata umfikirie; mwanadamu ni nini hata umjali? Ulimfanya tu kidogo kuwa chini ya malaika; umemvika taji ya utukufu na heshima, ukaweka kila kitu chini ya miguu yake.” Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote, yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa. Lakini twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini kuliko malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote. Sasa tunamwona ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka. Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu. Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao, ndugu zake; kama asemavyo: “Ee Mungu, nitawasimulia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao.” Tena asema: “Nitamwekea Mungu tumaini langu.” Na tena: “Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu.” Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili, kwa njia ya kifo chake, amwangamize Ibilisi ambaye ana mamlaka juu ya kifo, na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya kifo. Maana ni wazi kwamba yeye hakuja kuwasaidia malaika, bali kama yasemavyo Maandiko: “Anawasaidia wazawa wa Abrahamu.” Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake kwa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe. Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa.
Waebrania 2:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa hiyo imetupasa kuyaangalia zaidi hayo tuliyoyasikia tusije tukayakosa. Kwa maana, ikiwa lile neno lililonenwa na malaika lilikuwa imara, na kila kosa na uasi ulipata ujira wa haki, sisi je! Tutapataje kupona, tukipuuza wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliomsikia; Mungu naye akishuhudia pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa karama za Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe. Maana hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema, Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo kwa muda kuliko malaika, Umemvika taji la utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakubakiza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hamjaona vitu vyote kutiwa chini yake, ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo kwa muda kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji la utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake; akisema, Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu; Katikati ya kanisa nitakuimbia sifa. Na tena, Nitakuwa nimemtumaini yeye. Na tena, Tazama, mimi nipo hapa na watoto niliopewa na Mungu. Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao katika maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Abrahamu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye kafara ya suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.
Waebrania 2:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo imetupasa kuyaangalia zaidi hayo yaliyosikiwa tusije tukayakosa. Kwa maana, ikiwa lile neno lililonenwa na malaika lilikuwa imara, na kila kosa na uasi ulipata ujira wa haki, sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia; Mungu naye akishuhudu pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa magawanyo ya Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe. Maana hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema, Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hamjaona vitu vyote kutiwa chini yake, ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake; akisema, Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu; Katikati ya kanisa nitakuimbia sifa. Na tena, Nitakuwa nimemtumaini yeye. Na tena, Tazama, mimi nipo hapa na watoto niliopewa na Mungu. Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.
Waebrania 2:1-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa hiyo, imetupasa kuwa waangalifu sana kuhusu kile tulichosikia, ili tusije tukakiacha. Kwa kuwa kama ujumbe ulionenwa na malaika ulikuwa imara, na kila uasi na kutokutii kulipata adhabu ya haki, je, sisi tutapataje kupona kama tusipojali wokovu mkuu namna hii? Wokovu huu, ambao mwanzo ulitangazwa na Bwana, ulithibitishwa kwetu na wale waliomsikia. Pia Mungu aliushuhudia kwa ishara, maajabu, na kwa miujiza mbalimbali, na karama za Roho Mtakatifu alizozigawa kulingana na mapenzi yake. Mungu hakuuweka ulimwengu ujao ambao tunanena habari zake chini ya malaika. Lakini kuna mahali mtu mmoja ameshuhudia, akisema: “Mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria, binadamu ni nani hata unamjali? Umemfanya chini kidogo kuliko malaika; ukamvika taji la utukufu na heshima, nawe umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Kwa kuweka vitu vyote chini yake, Mungu hakuacha kitu chochote ambacho hakukiweka chini ya mwanadamu. Lakini kwa sasa, hatuoni kwamba kila kitu kiko chini yake. Lakini twamwona Yesu, aliyefanywa chini kidogo kuliko malaika, sasa akiwa amevikwa taji la utukufu na heshima kwa sababu alistahimili mauti, ili kwa neema ya Mungu apate kuonja mauti kwa ajili ya kila mtu. Ili kuwaleta wana wengi katika utukufu, ilifaa kwamba Mungu, ambaye ni kwa ajili yake na kupitia kwake kila kitu kimekuwepo, amkamilishe mwanzilishi wa wokovu wao kupitia kwa mateso yake. Yeye awafanyaye watu kuwa watakatifu, pamoja na hao ambao hufanywa watakatifu, wote hutoka katika jamaa moja. Hivyo Yesu haoni aibu kuwaita ndugu zake. Yeye anasema, “Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu; mbele ya kusanyiko nitaimba sifa zako.” Tena, “Nitaweka tumaini langu kwake.” Tena anasema, “Niko hapa, pamoja na watoto ambao Mungu amenipa.” Basi kwa kuwa watoto wana mwili na damu, yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani ibilisi, na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti. Kwa kuwa ni dhahiri kwamba hakuja kusaidia malaika, bali uzao wa Abrahamu. Kwa sababu hii ilibidi afanane na ndugu zake kwa kila hali, ili apate kuwa Kuhani Mkuu mwenye huruma na mwaminifu katika kumtumikia Mungu, ili pia apate kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za watu. Kwa kuwa yeye mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa.