Waebrania 12:3-6
Waebrania 12:3-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa. Maana katika kupambana na dhambi, nyinyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu. Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja nyinyi kuwa wanawe? “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usife moyo anapokukanya. Maana Bwana humpa nidhamu kila anayempenda, humwadhibu kila anayekubali kuwa mwanawe.”
Waebrania 12:3-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili upinzani mkuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi; tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau maonyo ya Bwana, Wala usife moyo ukiadhibiwa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humuonya Naye humpiga kila mwana amkubaliye.
Waebrania 12:3-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi; tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye.
Waebrania 12:3-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa. Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu. Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema: “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usikate tamaa akikukemea, kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao, na humwadhibu kila mmoja anayemkubali kuwa mwana.”