Hagai 2:1-23
Hagai 2:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo siku ya ishirini na moja, mwezi wa saba mwaka huohuo, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia nabii Hagai. Alimwambia Hagai aongee na mkuu wa Yuda, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki na watu wote waliorudi kutoka uhamishoni awaambie hivi: “Je, kuna yeyote kati yenu asiyekumbuka jinsi hekalu hili lilivyokuwa la fahari? Sasa mnalionaje? Bila shaka sasa mnaliona kama si kitu! Hata hivyo, usife moyo, ewe Zerubabeli. Jipe moyo, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Jipeni moyo nanyi watu wote wa nchi hii. Fanyeni kazi, maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nipo pamoja nanyi. Mlipotoka Misri niliwaahidi kwamba daima nitakuwa pamoja nanyi. Basi, ningali pamoja nanyi, kwa hiyo, msiogope kitu. “Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema, hivi karibuni nitazitikisa mbingu na dunia, bahari na nchi kavu. Nitayatikisa mataifa yote na hazina zao zote zitaletwa humu, nami nitalifanya hekalu hili kuwa la fahari. Mimi nimesema. Fedha na dhahabu yote duniani ni mali yangu. Hekalu jipya litakuwa lenye fahari zaidi kuliko lile la awali, na mahali hapo ndipo nitakapowapa watu wangu fanaka.” Asema Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi lilimjia nabii Hagai, akamwambia: “Waambie makuhani watoe uamuzi juu ya jambo hili: Kama mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa vazi lake, kisha akagusa kwa upindo wa vazi hilo mkate au chakula kilichopikwa, au divai, au mafuta au chakula cha aina yoyote ile, je, chakula hicho kitakuwa kitakatifu?” Makuhani wakamjibu, “La, hasha.” Hagai akawauliza tena, “Je, mtu aliye najisi kwa kugusa maiti, akigusa baadhi ya vyakula hivi, chakula hicho kitakuwa najisi?” Makuhani wakamjibu, “Ndiyo, kitakuwa najisi.” Hapo Hagai akawaambia, “Mwenyezi-Mungu asema kwamba, hivyo ndivyo ilivyo kwa watu wa taifa hili na kila kitu wanachofanya; kadhalika na kila wanachotoa madhabahuni ni najisi. “Lakini sasa angalieni mambo yatakayotukia. Kabla ya kuanza kujenga upya hekalu langu, hali yenu ilikuwaje? Mliliendea fungu la nafaka mkitarajia kupata vipimo ishirini, lakini kulikuwa na vipimo kumi tu. Mliliendea pipa la divai mkitarajia kujaza vyombo hamsini, lakini mlikuta ishirini tu. Niliwapiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, nikaharibu kila mlichojaribu kupanda, lakini hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Leo ni siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, siku ambayo msingi wa hekalu umekamilika. Basi, ngojeni mwone yale yatakayotokea tangu leo. Ingawa sasa hamna nafaka ghalani, nayo mizabibu, mitini, mikomamanga na mizeituni haijazaa kitu, lakini tangu leo, nitawabariki.” Siku hiyohiyo ya ishirini na nne, mwezi wa tisa, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Hagai mara ya pili: “Ongea na Zerubabeli mkuu wa Yuda, umwambie hivi: Niko karibu kuzitikisa mbingu na dunia, kuangusha falme na kukomesha nguvu zao. Nitayapindua magari yao ya farasi na wapandafarasi wake, nao wataanguka na kuuana wao kwa wao. Siku hiyo, nitakuchukua wewe mtumishi wangu Zerubabeli mwana wa Shealtieli, na kukuteua ili utawale kwa jina langu. Wewe ndiwe niliyekuchagua.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amesema.
Hagai 2:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hao watu waliokuwa wamebaki, ukisema, Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu? Lakini sasa uwe jasiri, Ee Zerubabeli, asema BWANA; nawe uwe jasiri, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni jasiri, enyi watu wote wa nchi hii, asema BWANA; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema BWANA wa majeshi; kama ilivyo ahadi niliyowawekea mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope. Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Kwa mara nyingine, kitambo kidogo tu, nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu; nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema BWANA wa majeshi. Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema BWANA wa majeshi. Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema BWANA wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema BWANA wa majeshi. Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Waulizeni sasa makuhani kuhusu sheria, mkisema, Mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa nguo yake, naye kwa upindo wake akagusa mkate, au ugali, au divai, au mafuta, au chakula chochote, je, Kitu hicho kitakuwa kitakatifu? Makuhani wakajibu, wakasema, La. Ndipo Hagai akasema, Kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti, akigusa kimojawapo cha vitu hivi, je, Kitakuwa najisi? Makuhani wakajibu, wakasema, Kitakuwa najisi. Ndipo Hagai akajibu, akasema, Hivyo ndivyo walivyo watu hawa, na hivyo ndivyo lilivyo taifa hili mbele zangu, asema BWANA; na hivyo ndivyo ilivyo kila kazi ya mikono yao; na kitu hicho wakitoacho sadaka huko ni najisi. Na sasa nawaomba, tafakarini; tangu siku hii na siku zilizopita; kabla jiwe halijatiwa juu ya jiwe katika nyumba ya BWANA; katika wakati huo wote, mtu alipofikia rundo la vipimo ishirini, palikuwa na vipimo kumi tu; na mtu alipofikia pipa kubwa apate kuteka divai ya vyombo hamsini, palikuwa na divai ya vyombo ishirini tu. Niliwapiga kwa ukavu, na ukungu, na mvua ya mawe, katika kazi zote za mikono yenu; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la BWANA tafakarini haya. Je, Mbegu ingali ghalani? Naam, huo mzabibu, wala mtini, wala mkomamanga, wala mzeituni, haikuzaa kitu; tangu siku hii ya leo nitawabariki. Kisha neno la BWANA likamjia Hagai mara ya pili, siku ya ishirini na nne ya mwezi, kusema, Sema na Zerubabeli, mtawala wa Yuda, ukisema, Nitazitikisa mbingu na dunia; nami nitakipindua kiti cha enzi cha falme, nami nitaziharibu nguvu za falme za mataifa; nami nitayapindua magari, na hao wapandao ndani yake; farasi na hao wawapandao wataanguka chini; kila mtu kwa upanga wa ndugu yake. Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, nitakutwaa wewe, Ee Zerubabeli, mtumishi wangu, mwana wa Shealtieli, asema BWANA, nami nitakufanya kuwa kama pete yenye mhuri; kwa kuwa nimekuchagua, asema BWANA wa majeshi.
Hagai 2:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema, Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hayo mabaki ya watu, ukisema, Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu? Lakini sasa uwe hodari, Ee Zerubabeli, asema BWANA; nawe uwe hodari, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni hodari, enyi watu wote wa nchi hii, asema BWANA; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema BWANA wa majeshi; kama neno lile nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope. Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Mara moja tena, ni kitambo kidogo tu, nami nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu; nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema BWANA wa majeshi. Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema BWANA wa majeshi. Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema BWANA wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema BWANA wa majeshi. Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa kenda, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Waulizeni sasa makuhani katika habari ya sheria, mkisema, Mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa nguo yake, naye akagusa kwa upindo wake mkate, au ugali, au divai, au mafuta, au chakula cho chote, je! Kitu hicho kitakuwa kitakatifu? Makuhani wakajibu, wakasema, La. Ndipo Hagai akasema, Kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti, akigusa kimojawapo cha vitu hivi, je! Kitakuwa najisi? Makuhani wakajibu, wakasema, Kitakuwa najisi. Ndipo Hagai akajibu, akasema, Hivyo ndivyo walivyo watu hawa, na hivyo ndivyo lilivyo taifa hili mbele zangu, asema BWANA; na hivyo ndivyo ilivyo kila kazi ya mikono yao; na kitu hicho wakitoacho sadaka huko ni najisi. Na sasa nawaomba, tafakarini; tangu siku hii na siku zilizopita; kabla halijatiwa bado jiwe juu ya jiwe katika nyumba ya BWANA; katika wakati huo wote, mtu alipofikia chungu ya vipimo ishirini, palikuwa na vipimo kumi tu; na mtu alipofikia shinikizo apate kuteka divai ya vyombo hamsini, palikuwa na divai ya vyombo ishirini tu. Naliwapiga kwa ukavu, na ukungu, na mvua ya mawe, katika kazi zote za mikono yenu; lakini hamkunielekea mimi, asema BWANA. Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kenda, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la BWANA tafakarini haya. Je! Mbegu ingali ghalani? Naam, huo mzabibu, wala mtini, wala mkomamanga, wala mzeituni, haikuzaa kitu; tangu siku hii ya leo nitawabariki. Kisha neno la BWANA likamjia Hagai mara ya pili, siku ya ishirini na nne ya mwezi, kusema, Sema na Zerubabeli, liwali wa Yuda, ukisema, Nitazitikisa mbingu na dunia; nami nitakipindua kiti cha enzi cha falme, nami nitaziharibu nguvu za falme za mataifa; nami nitayapindua magari, na hao wapandao ndani yake; farasi na hao wawapandao wataanguka chini; kila mtu kwa upanga wa ndugu yake. Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, nitakutwaa wewe, Ee Zerubabeli, mtumishi wangu, mwana wa Shealtieli, asema BWANA, nami nitakufanya kuwa kama pete yenye muhuri; kwa kuwa nimekuchagua, asema BWANA wa majeshi.
Hagai 2:1-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika siku ya ishirini na moja ya mwezi wa saba, neno la BWANA lilikuja kupitia nabii Hagai, kusema: “Sema na Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, na mabaki ya watu. Uwaulize, ‘Ni nani miongoni mwenu aliyebaki ambaye aliiona hii nyumba katika utukufu wake wa mwanzo? Sasa inaonekanaje kwenu? Je, haionekani kwenu kama si kitu? Lakini sasa uwe imara, ee Zerubabeli,’ asema BWANA. ‘Kuwa imara, ee kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Mwe imara, enyi watu wote wa nchi,’ asema BWANA, ‘na mfanye kazi. Kwa kuwa mimi nipo pamoja nanyi,’ asema BWANA wa majeshi. ‘Hili ndilo nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri. Pia Roho wangu anadumu kati yenu. Msiogope.’ “Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: ‘Baada ya muda kidogo kwa mara nyingine nitazitikisa mbingu na nchi, bahari na nchi kavu. Nitatikisa mataifa yote, nacho kile kinachotamaniwa na mataifa yote kitakuja, nami nitaujaza utukufu katika nyumba hii,’ asema BWANA wa majeshi. ‘Fedha ni mali yangu na dhahabu ni mali yangu,’ asema BWANA wa majeshi. ‘Utukufu wa nyumba hii ya sasa utakuwa mkubwa kuliko utukufu wa ile nyumba ya mwanzoni,’ asema BWANA wa majeshi. ‘Na mahali hapa nitawapa amani,’ asema BWANA wa majeshi.” Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la BWANA lilikuja kwa nabii Hagai: “Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: ‘Ulizeni makuhani jinsi sheria inavyosema: Kama mtu akibeba nyama iliyowekwa wakfu katika pindo la vazi lake, kisha lile pindo likagusa mkate au mchuzi, divai, mafuta au chakula kingine, je, kitu hicho kitakuwa kimewekwa wakfu?’ ” Makuhani wakajibu, “La.” Kisha Hagai akasema, “Je, kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti akigusa mojawapo ya vitu hivi, kitu hicho kitakuwa kimetiwa unajisi?” Makuhani wakajibu, “Ndiyo, huwa kimenajisiwa.” Kisha Hagai akasema, “ ‘Basi ndivyo walivyo machoni pangu hawa watu na taifa hili,’ asema BWANA. ‘Lolote wafanyalo na chochote watoacho hapo ni najisi. “ ‘Sasa fikirini kwa uangalifu kuanzia leo na kuendelea: tafakarini jinsi mambo yalivyokuwa kabla halijawekwa jiwe moja juu ya lingine katika Hekalu la BWANA. Mtu alipoendea lundo la nafaka la vipimo ishirini, kulikuwa na vipimo kumi tu. Mtu alipoendea pipa la mvinyo ili kuchota vipimo hamsini, kulikuwa na vipimo ishirini tu. Kazi zenu zote za mikono nilizipiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, lakini hata hivyo, hamkunigeukia mimi,’ asema BWANA. ‘Tangu leo na kuendelea, kuanzia siku hii ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, tafakarini siku ambayo msingi wa Hekalu la BWANA uliwekwa. Tafakarini: Je, bado kuna mbegu iliyobakia ghalani? Hadi sasa, hakuna mzabibu au mtini, mkomamanga wala mzeituni uliozaa tunda. “ ‘Kuanzia leo na kuendelea, nitawabariki.’ ” BWANA Neno la BWANA likamjia Hagai kwa mara ya pili katika siku ya ishirini na nne ya mwezi kusema: “Mwambie Zerubabeli mtawala wa Yuda kwamba nitazitikisa mbingu na nchi. Nitapindua viti vya falme, na kuziharibu kabisa nguvu za falme za kigeni. Nitapindua magari ya vita pamoja na waendeshaji wake; farasi na wapanda farasi wataanguka, kila mmoja kwa upanga wa ndugu yake. “ ‘Katika siku ile,’ asema BWANA wa majeshi, ‘nitakuchukua wewe, mtumishi wangu Zerubabeli mwana wa Shealtieli,’ asema BWANA. ‘Nitakufanya kama pete yangu ya muhuri, kwa kuwa nimekuchagua,’ asema BWANA wa majeshi.”