Hagai 1:1-6
Hagai 1:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya kwanza ya mwezi wa sita mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario wa Persia, Mwenyezi-Mungu alimpa Hagai ujumbe aupeleke kwa Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mkuu wa Yuda, na kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Hagai akasema: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: Watu hawa wanasema kwamba wakati wa kulijenga upya hekalu langu haujafika.” Lakini Mwenyezi-Mungu ameniambia mimi nabii Hagai, “Je, ni sawa kwenu kukaa katika majumba yenu ya fahari hali hekalu langu ni magofu matupu?” Sasa, asema hivi Mwenyezi-Mungu: “Fikirini kama mnafanya sawa! Nyinyi mmepanda mbegu kwa wingi, lakini mmevuna kidogo; mnakula, lakini hamshibi; mnakunywa divai, lakini hamtosheki; mnavaa nguo, lakini bado mnasikia baridi; mfanyakazi mshahara wake huwa kama umetumbukizwa katika mfuko uliotoboka.”
Hagai 1:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake nabii Hagai, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Wakati wa kuijenga upya nyumba ya BWANA haujafika. Ndipo neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamtosheki na vinywaji; mnajivika nguo lakini hampati joto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotobokatoboka.
Hagai 1:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwaka wa pili wa Dario mfalme, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake Hagai nabii, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujenga nyumba ya BWANA. Ndipo neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka.
Hagai 1:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario wa Uajemi, katika siku ya kwanza ya mwezi wa sita, neno la BWANA lilikuja kupitia kwa nabii Hagai kwenda kwa Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda na kwa Yoshua mwana wa kuhani mkuu Yehosadaki: Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Hawa watu husema, ‘Wakati haujawadia wa kujenga nyumba ya BWANA.’ ” Kisha neno la BWANA likaja kupitia kwa nabii Hagai: “Je, ni wakati wenu ninyi wa kuishi katika nyumba zenu zilizojengwa vizuri, wakati hii nyumba ikibaki, gofu?” Sasa hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Zitafakarini vyema njia zenu. Mmepanda vingi, lakini mmevuna haba. Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa, lakini hamtosheki. Mnavaa nguo, lakini hamsikii joto. Mnapata mishahara, lakini inatoweka kama imewekwa kwenye mfuko uliotobokatoboka.”